Baruku 4

Baruku 4

1Hekima ni kitabu cha amri za Mungu,

yeye ni sheria idumuyo milele.

Wanaomshikilia Hekima wataishi,

lakini watakaomwacha watakufa.

2Geuka, ewe Yakobo, umchukue Hekima;

tembea kuelekea mng'ao wa mwanga wake.

3Usimpe mtu mwingine fahari yako;

usiwape mataifa ya kigeni mapato yako.

4Heri yetu sisi, ee Israeli,

kwa maana tumejulishwa yampendezayo Mungu.

Ombolezo na matumaini ya Yerusalemu

5Jipeni moyo enyi watu wangu;

watu mnaolidumisha jina la Israeli.

6Nyinyi hamkuuzwa kwa watu wa mataifa muangamie,

bali mlitiwa mikononi mwa maadui zenu

kwa sababu mlimkasirisha Mungu.

7Mlimchokoza yeye aliyewaumba nyinyi,

kwa kutoa tambiko kwa pepo badala ya Mungu,

8Mlimsahau Mungu wa milele aliyewalea[#4:8 Jina “Mungu wa milele” ambalo lilitumiwa katika Mwa 21:33 na Isa 40:28 linatumiwa mara nyingi zaidi katika Biblia ya Kigiriki, na mara kwa mara katika kifupi kama “yeye aliye milele”, yaani: Mungu wa milele (taz Bar 4:10,14,20,22,24,35; 5:2; rejea pia 2Mak 1:25; Dan 13:42 (Kigiriki) na Rom 16:26).]

mkauhuzunisha mji wa Yerusalemu uliowatunzeni.

9Mji huo uliiona ghadhabu iliyokujia kutoka kwa Mungu,

ukasema: “Sikilizeni enyi jirani za Siyoni.

Mungu ameniletea huzuni kubwa,

10kwa maana nimeuona uhamisho wa watoto wangu,

ambao Mungu wa milele amewaletea.

11Mimi niliwalea kwa furaha,

lakini nikawaacha waende kwa machozi na huzuni.

12Mtu na asifurahie mkasa wangu mimi mjane,

mimi niliyefiwa na watoto wengi.

Niliachwa mkiwa kwa sababu ya dhambi za wanangu,

kwa sababu waligeuka wakaiacha sheria ya Mungu.

13Hawakuzijali kanuni zake,

hawakufuata njia za amri za Mungu,

wala kupita katika njia ya uadilifu uliowaonesha.

14“Enyi jirani zake Siyoni, njoni.

Kumbukeni uhamisho wa wanangu, wa kiume na wa kike,

uhamisho aliowaletea Mungu wa milele.

15Maana alileta dhidi yao taifa la mbali,

taifa la watu katili na wa lugha ngeni,

wasio na heshima kwa wazee

wala huruma kwa watoto.

16Waliwachukua mbali wavulana wapenzi wa mjane,

wakaniacha pweke nimefiwa na binti zangu.

17Lakini mimi nawezaje kuwasaidieni?

18Ni yule tu aliyewaleteeni balaa hilo

ndiye awezaye kuwaokoeni mikononi mwa maadui zenu.

19Nendeni, watoto wangu, nendeni tu!

Mimi nimeachwa mpweke.

20Nimevua vazi la amani,

nimevaa vazi la gunia la kuomba.

Nitamlilia Mungu wa milele siku zangu zote.

21Jipeni moyo enyi watoto wangu! Mlilieni Mungu

naye atawaokoeni makuchani mwa maadui.

22Maana namtumainia Mungu wa milele awaokoeni.

na furaha imenijia kutoka kwake huyo Mtakatifu,

kwa sababu ya huruma itakayowajia karibuni,

kutoka kwa Mwokozi wenu, Mungu wa milele.

23Kwa huzuni na machozi niliwaacheni mwende,

lakini Mungu atawarejesha kwangu kwa shangwe na furaha ya milele.

24Kama jirani za Siyoni walishuhudia kutekwa kwenu,

sasa wataona mkipata wokovu kutoka kwa Mungu,

wokovu utakaowajieni kwa utukufu mkubwa,

kwa fahari ya Mungu wa milele.

25Wanangu, vumilieni ghadhabu hiyo iliyowajieni kutoka kwa Mungu.

Maadui zenu wamewatesa,

lakini mtashuhudia karibuni kuangamizwa kwao,

nanyi mtakanyaga shingo zao kwa miguu yenu.

26Wanangu wapendwa, mmetembea katika njia za taabu;

mlichukuliwa kama kundi la kondoo lililochukuliwa na maadui wakali.

27Jipeni moyo, wanangu, na kumlilia Mungu,

kwani yeye aliyewaleteeni jambo hilo atawakumbukeni.

28Kama vile mlivyokusudia kwenda mbali na Mungu,

vivyo hivyo rudini na kumtafuta kwa hamu mara kumi zaidi.

29Hivyo, huyo aliyewaleteeni balaa hizi

atawaokoeni na kuwaleteeni furaha ya kudumu milele.”

30“Jipe moyo, ee Yerusalemu.

Mungu aliyekupa jina lako atakufariji.

31Ole wao wale waliokutesa,

na waliofurahia kuanguka kwako!

32Miji ile waliyoitumikia watoto wako kama watumwa itakuwa hali mbaya;

Mji ule uliowapokea watoto wako utapata balaa!

33Kama mji huo ulivyoshangilia kuanguka kwako,

na kufurahia kuangamia kwako,

vivyo hivyo nao utapatwa na uchungu kwa kuangamia kwake.

34Nitaondolea mbali majivuno yake juu ya wingi wa watu wake,

na kiburi chake kitageuka kuwa masikitiko.

35Mimi Mungu wa milele nitamshushia moto utakaowaka kwa siku nyingi;

utakuwa makazi ya pepo kwa muda mrefu.

36“Angalia upande wa mashariki, ee Yerusalemu,

uione furaha inayokujia kutoka kwa Mungu!

37Tazama, watoto wako uliowaacha waende wanakuja nyumbani.

wanakuja pamoja kutoka mashariki na magharibi,

Kwa amri ya Mungu Mtakatifu,

wanakuja wakishangilia utukufu wake.”

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania