The chat will start when you send the first message.
1Mfalme Nebukadneza alitengeneza sanamu ya dhahabu, yenye kimo mita ishirini na nane na upana mita tatu. Aliisimamisha katika sehemu tambarare ya Dura, mkoani Babuloni.[#3:1 Au: sanamu iliyopakwa dhahabu na sio sanamu yote ya dhahabu tupu. Sanamu hiyo henda hapo awali iliwakilisha mungu wa Wababuloni aitwaye “Beli”.; #3:1 Haijulikani mahali au mji huo ulikuwa wapi lakini huenda ulikuwa kusini mwa mji wa Babuloni (taz 4:28-31). Maana ya jina hilo ni “ngome”.]
2Kisha mfalme akaamuru maliwali, wasimamizi, wakuu wa mikoa, washauri, watunza hazina, majaji, mahakimu na maofisa wote wa mikoa wahudhurie sherehe ya kuzindua rasmi sanamu aliyoisimamisha.
3Basi, maliwali, wasimamizi, wakuu wa mikoa, washauri, watunza hazina, majaji, mahakimu na maofisa wote wa mikoa wakakusanyika tayari kwa uzinduzi wa sanamu aliyosimamisha mfalme Nebukadneza.
4Mpiga mbiu akatangaza kwa sauti kubwa, “Enyi watu wa makabila yote, mataifa yote na lugha zote, mnaamriwa kwamba[#3:4 Namna ya mtindo kawaida uliotumika kwa ajili ya kutoa ilani au tangazo rasmi na ambao ulilipa tangazo lenyewe umaarufu wake. Taz Dan 3:29; 4:1; 5:19; 7:14; Esta 1:22; 8:9; Ufu 5:9; 7:9.]
5mkisikia sauti ya baragumu, filimbi, kinubi, zeze, santuri, zumari na sauti za ala nyingine za muziki, lazima mwiname chini na kuiabudu sanamu ya dhahabu aliyosimamisha mfalme Nebukadneza.[#3:5 Ala za muziki, kama vile ngoma n.k., zilikuwa sehemu moja muhimu katika shehere na sikukuu za kidini katika utamaduni wa wakati huo na hata katika nchi zetu.]
6Na yeyote ambaye hatainama chini na kuiabudu, atatupwa mara moja katika tanuri ya moto mkali.”[#3:6 Amri hiyo ya kuiabudu ile sanamu ilimtia Danieli na wenzake katika hali ngumu kwa vile sheria yao ilitamka dhahiri: “Usiabudu miungu wengine isipokuwa mimi” (Kut 20:2-17).]
7Kwa hiyo, watu wote, mara waliposikia sauti za baragumu, filimbi, kinubi, zeze, santuri, zumari na sauti za ala nyingine za muziki, walianguka kifudifudi na kuiabudu ile sanamu ya dhahabu ambayo mfalme Nebukadneza aliisimamisha.
8Wakati huo, baadhi ya Wakaldayo wakajitokeza na kuwashtaki Wayahudi. Walimwambia mfalme Nebukadneza,
9“Uishi, ee mfalme!
10Wewe, ee mfalme, ulitoa amri kuwa kila mtu anaposikia sauti ya baragumu, filimbi, kinubi, zeze, santuri, zumari na kila aina ya muziki, ainame chini na kuiabudu ile sanamu ya dhahabu.
11Na kwamba mtu yeyote asiyeinama chini na kuiabudu sanamu hiyo, atupwe ndani ya tanuri ya moto mkali.
12Sasa, kuna Wayahudi fulani uliowateua kushughulikia mambo ya utawala wa mkoa wa Babuloni, yaani Shadraki, Meshaki na Abednego; watu hawa, ee mfalme, hawakuitii amri yako. Wanakataa kuitumikia miungu yako na kuiabudu ile sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.”
13Hapo mfalme Nebukadneza, huku akiwaka hasira, akaamuru Shadraki, Meshaki na Abednego waletwe mbele yake. Nao wakawaleta mbele ya mfalme.
14Mfalme Nebukadneza akawauliza, “Je, ni kweli kwamba wewe Shadraki, wewe Meshaki na wewe Abednego, hamuitumikii miungu yangu wala kuiabudu ile sanamu ya dhahabu niliyoisimamisha?
15Basi, mtakaposikia tena sauti ya baragumu, filimbi, kinubi, zeze, santuri, zumari na sauti za ala nyingine za muziki, je, mko tayari kuinama chini na kuiabudu sanamu niliyotengeneza? Kama mkikataa, mtatupwa mara moja katika tanuri ya moto mkali. Je, ni mungu gani anayeweza kuwaokoa mikononi mwangu?”
16Shadraki, Meshaki na Abednego wakamjibu mfalme, “Ee Nebukadneza, sisi hatuhitaji kukujibu kuhusu jambo hilo.
17Ikiwa ndivyo, Mungu wetu ambaye tunamtumikia aweza kutuokoa katika tanuri ya moto mkali; tena atatuokoa mikononi mwako, ee mfalme.[#3:17 Tamko hili ni wazo muhimu sana katika kitabu cha Danieli. Taz pia Dan 6:16,26-27; 12:1-2.]
18Lakini, hata kama haitafanyika hivyo, ujue wazi, ee mfalme, kwamba sisi hatutaitumikia miungu yako wala kuiabudu sanamu ya dhahabu uliyosimamisha.”
19Hapo, mfalme Nebukadneza akawaka hasira, sura yake ikabadilika kwa chuki dhidi ya Shadraki, Meshaki na Abednego. Akaamuru mwako wa moto wa tanuri uongezwe mara saba kuliko kawaida yake.
20Akaamuru watu fulani wenye nguvu kabisa katika jeshi lake wawafunge Shadraki, Meshaki na Abednego na kuwatupa katika ile tanuri ya moto mkali.
21Basi, vijana hao wakafungwa hali wamevaa makoti yao, kanzu zao, kofia na mavazi yao mengine, wakatupwa katikati ya ile tanuri ya moto mkali.
22Kwa vile amri ya mfalme ilikuwa kali, ule moto ulikuwa umewashwa ukawa mkali sana, hata ndimi za moto zikawateketeza wale watu waliowapeleka Shadraki, Meshaki na Abednego.
23Ndipo Shadraki, Meshaki na Abednego, wakiwa wamefungwa, wakatumbukia katika ile tanuri ya moto mkali.[#3:23 Katika tafsiri ya Kigiriki ya Septuaginta (LXX), baada ya aya hii na kabla ya 3:24 kuna nyongeza (katika toleo hili imechapishwa kwa italiki) inayohusu kwanza “Sala ya Azaria” na pili “Wimbo wa Vijana Watatu” na ambayo haipo katika Biblia ya Kiebrania.]
24Vijana wale watatu, Hanania, Mishaeli na Azaria, walitembeatembea katikati ya moto, wakimsifu na kumtukuza Bwana Mungu.[#Az 1-22 Haya ndio majina ya asili ya Shadraki, Meshaki na Abednego (taz Dan 1:6-7).]
25Kisha, Azaria akasimama katikati ya moto, akaanza kuomba kwa sauti kubwa:
26“Utukuzwe na kusifiwa, ee Bwana, Mungu wa babu zetu!
Jina lako litukuzwe milele.
27Yote uyafanyayo, wayafanya kwa haki kabisa;
matendo yako yote ni mema, njia zako ni sawa,
na hukumu zako zote ni za haki.
28Wewe una haki kuhusu maafa yote uliyosababisha yatupate,
na yaupate Yerusalemu, mji mtakatifu wa babu zetu.
Kwa sababu ya dhambi zetu tuliyastahili yote uliyotuletea.
29Naam, sisi tumekuacha wewe,
tukatenda dhambi, tukavunja sheria zako.
Katika mambo yote sisi tumekukosea sana,
wala hatukuzitii amri zako;
30hatukuyashika hayo,
kama ulivyotuamuru, ili tufanikiwe.
31Basi, yote uliyotuletea,
na yote uliyotutenda,
umeyatenda kwa haki kabisa.
32Umetutia mikononi mwa adui zetu,
watu ambao hawajali sheria,
watu wasiotaka kujua lolote juu ya Mungu;
umetutia mikononi mwa mfalme mbaya,
mfalme mwovu kupita wote ulimwenguni.
33Sasa hatuthubutu hata kulalamika,
aibu na fedheha vimetupata sisi watumishi wako wakuabuduo.
34Kwa ajili ya jina lako, usitutupe kabisa!
Usilitangue agano lako ulilofanya nasi.
35Utuonee huruma,
kwa ajili ya Abrahamu mpendwa wako,
kwa ajili ya Isaka mtumishi wako
na Israeli mtakatifu wako.
36Ukumbuke kwamba uliwapa ahadi,
kwamba wazawa wao watakuwa wengi kama nyota za mbinguni,
naam, wengi kama mchanga wa pwani.
37Maana sasa ee Bwana, tu wachache kuliko mataifa yote;
kwa dhambi zetu twadhulumiwa duniani kote mpaka leo.
38Hatuna tena mfalme, wala nabii, wala kiongozi;
hatuna sadaka za kuteketezwa, wala tambiko, kafara, wala ubani;
hatuna pa kukutolea sadaka na kupata rehema zako.
39Lakini twakujia kwa moyo wa toba na roho ya unyenyekevu,
utukubali kama vile tungekujia na sadaka ya kuteketezwa za kondoo dume na mafahali,
au na maelfu ya wanakondoo wanono.
40Ikubali toba yetu kama sadaka yetu leo,
ili tuweze kukutii kwa moyo wote,
maana, anayekutumaini wewe hataabiki kamwe.
41Sasa twataka kukutii kwa moyo wote;
twataka kukucha na kukutafuta.
42Usikubali tuaibike!
Ututendee kadiri ya uvumilivu wako,
na wingi wa huruma yako!
43Tukomboe kwa matendo yako makuu;
lifanye jina lako kuu litukuke, ee Bwana!
Wote wanaowaudhi watumishi wako waaibishwe.
44Na wafedheheshwe.
na wapokonywe uwezo wao,
nguvu zao na zivunjiliwe mbali;
45wapate kujua kwamba wewe ndiwe Bwana, ndiwe Mungu peke yako,
mtukufu juu ya ulimwengu wote.”
46Wakati huo wote watumishi wa mfalme ambao waliwatupa hao vijana ndani ya tanuri la moto, walizidisha juhudi zao za kuufanya ule moto uwake kwa ukali zaidi, kwa kumimina humo mafuta na lami, vifuu vya nazi na kuni.[#Az 23 Si yamkini ni mafuta gani (naftha); lakini namna ya mafuta kama vile petroli kama inavyotajwa katika 2Mak 1:20-22,30-36 huenda ndiyo yanayohusika.]
47Hapo, miali ya moto ikapanda juu zaidi ya mita ishirini na tano,
48ikaenea pande zote na kuwateketeza Wakaldayo waliokuwa wamesimama karibu.
49Malaika wa Bwana ambaye alikuwa ameingia katika tanuri pamoja na Azaria na wenzake, aliisukuma kando miali ya moto huo ndani ya tanuri,[#Az 26 Kuingia kwa malaika wa Bwana hapa na kazi yake, wakati hao watatu walikuwa wamekwisha kuwa ndani ya ile tanuri na kutembea humo (aya 24 ya toleo hili), ni tatizo na wengi wanafikiri kuna mchanganyiko wa mtiririko wa simulizi hapa.]
50akafanya katikati ya tanuri pawe na upepo wa baridi na unyevunyevu. Kwa hiyo, moto huo haukuwagusa kabisa, wala kuwadhuru, wala kuwasumbua vijana hao.
51Hapo, wote watatu wakiwa katikati ya tanuri, wakamwimbia Mungu wakamsifu na kumtukuza kwa sauti moja wakisema:
52“Twakusifu ee Bwana, Mungu wa babu zetu!
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele!
53Twalisifu jina lako kuu na takatifu;
lastahili kusifiwa na kutukuzwa milele!
54Twakusifu katika hekalu lako la fahari takatifu!
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele!
55Twakusifu wewe uketiye juu ya viumbe wenye mabawaj na kutazama chini vilindini![#Az 32 Maneno yanayofanana na maneno ya sifa zilizotamkwa kumwomba Mwenyezi-Mungu pale sanduku la agano lilipokuwa (1Sam 4:4).]
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele!
56Twakusifu ewe uketiaye kiti cha enzi cha ufalme wako!
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele!
57Twakusifu wewe ukaaye katika mawingu ya mbingu!
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele!
58“Msifuni Bwana enyi viumbe vyake vyote!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
59Msifuni Bwana enyi mbingu!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
60Msifuni Bwana enyi malaika wake!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
61Msifuni Bwana enyi maji yote juu ya mbingu!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
62Msifuni Bwana enyi wenye mamlaka!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
63Msifuni Bwana enyi jua na mwezi!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
64Msifuni Bwana enyi nyota za mbinguni!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
65Msifuni Bwana mvua yote na ukungu!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
66Msifuni Bwana enyi pepo zote!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
67Msifuni Bwana enyi moto na joto!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
68Msifuni Bwana enyi kipupwe na hari!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
69Msifuni Bwana enyi umande na theluji!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
70Msifuni Bwana enyi usiku na mchana!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
71Msifuni Bwana enyi mwanga na giza!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
72Msifuni Bwana enyi barafu na baridi!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
73Msifuni Bwana enyi ukungu na theluji!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
74Msifuni Bwana enyi umeme na mawingu!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
75“Dunia na imsifu Bwana!
Imsifu na kumtukuza milele!
76Msifuni Bwana enyi milima na vilima!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
77Msifuni Bwana enyi mimea yote duniani!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
78Msifuni Bwana enyi chemchemi za maji!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
79Msifuni Bwana enyi bahari na mito!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
80Msifuni Bwana enyi nyangumi na viumbe vyote majini!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
81Msifuni Bwana enyi ndege wote wa angani!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
82Msifuni Bwana enyi wanyama wa porini na wafugwao!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
83Msifuni Bwana enyi wanaadamu wote!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
84Msifuni Bwana enyi watu wa Israeli!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
85Msifuni Bwana enyi makuhani wake!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
86Msifuni Bwana enyi watumishi wake!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
87Msifuni Bwana enyi roho na nafsi za waadilifu!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
88Msifuni Bwana enyi watakatifu na wanyenyekevu wa moyo!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
89Msifuni Bwana enyi Hanania, Azaria na Mishaeli!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
Msifuni kwa maana ametuokoa kutoka Kuzimu,
ametuokoa kutoka nguvu za kifo,
ametuokoa ndani ya tanuri la moto mkali;
naam, ametuokoa kutoka katikati ya moto.
90Mshukuruni Bwana kwa maana ni mwema,
kwa maana huruma zake zadumu milele.
68 Msifuni enyi mnaomwabudu Bwana, Mungu wa miungu!
Mwimbieni sifa na kumshukuru,
kwa maana huruma zake zadumu milele!”
91Basi, mfalme Nebukadneza akashangaa, akainuka kwa haraka na kuwauliza washauri wake, “Je, hatukuwafunga watu watatu na kuwatupa motoni?” Nao wakamjibu mfalme, “Naam, mfalme! Ndivyo!”
92Kisha akauliza, “Lakini sasa mbona ninaona watu wanne wakitembeatembea humo motoni bila kufungwa na wala hawadhuriki, na mtu wa nne anaonekana kama mwana wa miungu?”[#3:25 Au: “mtu wa nne … kama malaika” (taz aya 28 ambapo Nebukadneza anamwita mtu huyo huyo “malaika”).]
93Basi, mfalme Nebukadneza akaukaribia mlango wa tanuri ya moto mkali, akaita, “Shadraki, Meshaki na Abednego, watumishi wa Mungu Mkuu, tokeni mje hapa!” Shadraki, Meshaki na Abednego wakatoka motoni.[#3:26 Nebukadneza anatumia jina hili hapa kumtaja Mungu wa Danieli, jina la sifa ambalo katika Biblia lilitumiwa siyo tu na Waisraeli bali pia na watu wa mataifa mengine. Katika Mwa 14:22 Abrahamu analitumia jina hili kwa Mwenyezi-Mungu. Taz pia Hes 24:16; Kumb 32:8; Zab 46:4; Mate 16:17.]
94Maliwali, wasimamizi, wakuu wa mikoa na washauri wa mfalme, wote wakakusanyika pamoja, wakaona ya kuwa ule moto haukuweza kuwaunguza hao watatu. Nywele zao hazikuungua, mavazi yao hayakuungua, wala hawakuwa na harufu yoyote ya moto.
95Basi, mfalme Nebukadneza akasema, “Na asifiwe Mungu wa Shadraki, Meshaki na Abednego kwa kuwa alimtuma malaika wake na kuwaokoa watumishi wake ambao wanamtegemea. Wao walikataa kutii amri yangu ya kifalme, wakaitoa mhanga miili yao badala ya kuabudu mungu mwingine, ila Mungu wao peke yake.[#3:28 Taz 3:25 maelezo. Jina malaika katika Kiebrania lina maana ya “mjumbe”. Katika Biblia malaika wanaonekana kuwa wajumbe na pia watumishi wa Mungu.]
96Kwa hiyo, naamuru kwamba watu wa kabila lolote, taifa lolote au lugha yoyote, watakaosema kitu chochote dhidi ya Mungu wa Shadraki, Meshaki na Abednego, watang'olewa viungo vyao kimojakimoja na nyumba zao zitabomolewa. Maana hakuna mungu mwingine awezaye kuokoa namna hii.”
97Basi, mfalme Nebukadneza akawapandisha vyeo Shadraki, Meshaki na Abednego katika mkoa wa Babuloni.