Waefeso 1

Waefeso 1

1Mimi Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, nawaandikia nyinyi watu wa Mungu huko Efeso, mlio waaminifu katika kuungana na Kristo Yesu.[#1:1 Taz Rom 1:6-7.; #1:1 Mji maarufu sana wakati huo ambao ulikuwa karibu na pwani ya Magharibi ya Asia Ndogo. Hati nyingine za kale hazina maneno “mlioko Efeso”.; #1:1-2 Kuhusu salamu taz Rom 1:1-7 maelezo na pia Utangulizi kwa Barua za A.J.]

2Nawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo.

Baraka za kiroho katika Kristo

3Atukuzwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo! Maana, katika kuungana na Kristo ametubariki kwa kutujalia zawadi zote za kiroho mbinguni.[#1:3-14 Sehemu hii pamoja na 1:15-23 inajumuisha pia maneno ya shukrani na sifa kwa Mungu. Inaonekana kwamba muundo wa kisehemu hiki karibu ni wa kishairi na ambao labda ulikuwa sehemu ya utenzi wa imani ya kanisa (taz Kol 1:15,16,17,18,19,20 maelezo). Wenyewe ni muhtasari wa mpango wa wokovu ambao ulikamilika kwa njia ya Kristo.; #1:3 Zawadi hizo za kiroho ni pamoja na kuondolewa au kusamehewa dhambi (1:7,8), hekima na kumjua Mungu (1:17), imani (2:8) na zawadi ya kuwa mitume na manabii (4:11). Taz pia 6:10-17.]

4Kabla ya kuumbwa ulimwengu, Mungu alituteua tuwe wake katika kuungana na Kristo ili tuwe watakatifu na bila hitilafu mbele yake. Kwa sababu ya upendo wake,[#1:4 Au, “bila dosari” au, “doa”. Rejea Efe 5:27; Kol 1:22; Yuda 24. Neno hilo hutajwa pia kuhusu wanyama wa tambiko (Kut 12:5; Lawi 1:3, n.k.).; #1:4-5 Taz Rom 8:15 maelezo.]

5Mungu alikuwa ameazimia tangu zamani kutuleta kwake kama watoto wake kwa njia ya Yesu Kristo. Ndivyo alivyopenda na kunuia.

6Basi, tumsifu Mungu kwa sababu ya neema yake tukufu ambayo ametujalia katika Mwanae mpenzi![#1:6 Jina la sifa la Masiha au Kristo; Mat 3:17; 17:5; Kol 1:13.]

7Maana kwa damu yake Kristo sisi tunakombolewa, yaani dhambi zetu zinaondolewa. Ndivyo ulivyo ukuu wa neema yake[#1:7 Yaani, kwa kifo chake msalabani ili kutukomboa; rejea Kol 1:14; Ebr 9:11-14.; #1:7 Taz Rom 3:25 maelezo.]

8aliyotukirimia bila kipimo! Kwa hekima na ujuzi wake wote

9Mungu alitekeleza kile alichonuia, akatujulisha mpango wake uliofichika, ambao alikuwa ameazimia kuutekeleza kwa njia ya Kristo.[#1:9 Neno kwa neno “siri”. Yahusu mpango wa Mungu uliofichika lakini sasa unafunuliwa na ambao unatajwa wazi katika aya inayofuata. Rejea 1:22-23; Rom 16:25 na pia Kol 1:26.]

10Mpango huo ambao angeutimiza wakati utimiapo ni kukusanya pamoja viumbe vyote, kila kitu mbinguni na duniani, chini ya Kristo.

11Katika kuungana na Kristo, sisi tumerithishwa wokovu kama tulivyopangiwa kadiri ya azimio lake Mungu atekelezaye kila kitu kulingana na uamuzi na matakwa yake.[#1:11 Yaani tumepewa yale Mungu aliyoahidi kwa watoto wake. Rejea Rom 8:17; Gal 3:29; 4:7; Efe 1:14,18.]

12Basi, sisi tuliotangulia kumtumainia Kristo tunapaswa kuusifu utukufu wa Mungu![#1:12 Hapa na labda pia katika aya ya 11 yamaanisha Wayahudi, na ni tofauti na “Nanyi” katika aya ya 13 ambapo ni dhahiri yahusu watu wa mataifa mengine (rejea Efe 2:11; 3:1).; #1:12 Waliokuwa wa kwanza kumwamini Kristo walikuwa mitume ambao walikuwa Wayahudi.]

13Nanyi pia watu wa mataifa mengine, mliusikia ujumbe wa kweli yaani Habari Njema iliyowaletea wokovu, mkamwamini Kristo; naye Mungu, ili kuonesha kuwa nyinyi ni wake, akawapiga mhuri kwa kuwapeni yule Roho Mtakatifu aliyetuahidia.

14Huyu Roho ni dhamana ya kupata yote yale Mungu aliyowaahidia watu wake, na jambo hili latuhakikishia kwamba Mungu atawakomboa kabisa wote walio wake. Tuusifu utukufu wake![#1:14 Taz 2Kor 1:22 maelezo.]

Sala za Paulo

15Kwa sababu hiyo, tangu niliposikia juu ya imani yenu kwa Bwana Yesu, na mapendo yenu kwa watu wote wa Mungu,[#1:15 Kol 1:4.]

16sijaacha kamwe kumshukuru Mungu kwa ajili yenu. Ninawakumbuka katika sala zangu,

17ili Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba mtukufu, awajalieni Roho wake atakayewapa hekima na kuwafunulieni Mungu mpate kumjua.[#1:17 Taz Yoh 17:3 maelezo; rejea Kol 1:9.]

18Namwomba Mungu aifunue mioyo yenu iweze kuuona mwanga wake, mpate kutambua lile tumaini alilowaitieni na utukufu mkuu wa zawadi alizowawekea watu wake,

19mpate kutambua jinsi uwezo wake ulivyo mkuu mno kwa ajili yetu sisi tunaoamini. Uwezo huo unaofanya kazi ndani yetu ni sawa na nguvu ile kuu mno

20aliyomfufua nayo Kristo kutoka kwa wafu, akamketisha upande wake wa kulia mbinguni.[#1:20 Yaani mahali pa heshima na mamlaka (rejea Zab 110:1). Na kuhusu “mbinguni” taz Efe 1:3 maelezo.]

21Huko, Kristo anatawala juu ya kila tawala, mamlaka, enzi na ukuu; anatawala juu ya kila cheo kiwezacho kutajwa katika ulimwengu huu na katika ulimwengu ujao.[#1:21-22 Kol 1:16; 2:10; 1Pet 3:21-22; rejea Efe 6:12. Yahusu nguvu za kiroho ambazo zinautawala ulimwengu na ambazo sasa zimewekwa chini ya Kristo. Rejea Efe 3:10.]

22Mungu ameweka vitu vyote chini ya miguu yake, akamkabidhi kwa kanisa akiwa mkuu wa vitu vyote.

23Kanisa ni mwili wa Kristo, na ukamilifu wake yeye anayekamilisha vitu vyote kila mahali.[#1:22-23 Kol 1:18; rejea Rom 12:5; 1Kor 12:27.; #1:23 Yaani Kanisa linapokea kutoka kwa Kristo kila kitu, naye Kristo, kwa njia ya Kanisa, anatekeleza kitendo chake cha wokovu kila mahali.]

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania