The chat will start when you send the first message.
1Katika mwaka wa pili wa utawala wa Ahasuero, mfalme mkuu wa Persia, katika siku ya kwanza ya mwezi wa Nisani, Mordekai mwana wa Yairi, mwana wa Shemi, mwana wa Kishi kutoka katika kabila la Benyamini, aliota ndoto.[#A:1—2:23 Sura hizi za kwanza zinatumika hapa kama utangulizi na kuonesha jinsi Esta alivyopata kuwa malkia katika nchi ya Persia. Katika tafsiri ya Kilatini (Makala ya Vulgata) Nyongeza A - E zilichukuliwa na Yeronimo kama zisizokuwa katika Makala ya Kiebrania na hivyo akaziweka baada ya makala ya Kiebrania ya Esta kama zilivyo sasa katika tafsiri ya Vulgata.; #A:1 Taz pia 2:6. Jina hili linatumika katika makala za Kiebrania. Katika Kigiriki tuna “Artashasta”, jina la mfalme mwingine aliyetawala baada yake. Ahasuero alikuwa mfalme wa milki ya Persia tangu mwaka 486 mpaka 465 K.K. Persia ilikuwa mojawapo ya milki maarufu sana nyakati hizo za kale na ilienea tangu bara la India mpaka Kushi, yaani mahali ambapo sasa ni eneo la Afrika hususani nchi za Ethiopia, Eritrea na Sudani.; #A:1 Mwandishi akifuata desturi ya kutaja nasaba ya watu mashuhuri katika historia ya Waisraeli anamtaja pia Mordekai na nasaba yake. Jina Mordekai laweza kuwa na uhusiano na jina la mungu wa Wababuloni aitwaye “Marduki”.; #A:1 Maana kamili ya hiyo ndoto ya Mordekai inatolewa katika F:1-10. Kama vile mara kadhaa katika Biblia, “ndoto” inamweka mhusika katika tukio lenye maana kubwa (rejea k.m. Mwa 37:5-10; Dan 7; Mat 1:20-24; Mate 16:9-10).]
2Mordekai alikuwa Myahudi na aliishi katika mji mkuu wa Susa. Yeye alikuwa mtu maarufu na mtumishi katika ikulu ya mfalme Ahasuero.[#A:2 Huu ulikuwa mojawapo ya miji mikuu sana ya milki hiyo ya Persia na ulikuwa mashariki mwa nchi ya sasa ya Irani.; #A:2 Neno kwa neno: “aliketi” au “alikaa kwenye lango la mfalme” yaani alikuwa na mamlaka fulani kwenye ukumbi wa mfalme au hata alikuwa mtumishi wa cheo fulani.]
3Mordekai alikuwa mmoja wa mateka ambao mfalme Nebukadneza wa Babuloni aliwahamisha kutoka Yerusalemu akawapeleka hadi Babuloni pamoja na mfalme Yekonia wa Yudea.[#A:3 Taz 2:6 maelezo.]
Ndoto aliyoota Mordekai ilikuwa hivi:
4Mordekai aliota kuna kelele, ghasia, ngurumo na mtetemeko wa ardhi, pamoja na machafuko duniani.[#A:4 Kuhusu mtetemeko wa ardhi, rejea Yoe 4:16.]
5Kisha kukatokea majoka mawili makubwa yaliyokuwa tayari kupigana, nayo yalitoa mlio wa kutisha.[#A:5 Majoka hayo mawili ni mfano wa wema na uovu, hali ambazo katika makala ya Kigiriki zinawakilisha Mordekai na Hamani.]
6Kwa mlio wao huo mataifa yote yakajiandaa kupigana vita na watu wa Mungu, taifa adilifu.
7Siku hiyo ilikuwa ya giza na huzuni, majonzi na udhia, msiba na fujo duniani kote.
8Taifa lile lote adilifu lilisumbuliwa, likihofia maovu yatakayolikumba. Watu wakajiandaa kufa.
9Basi, wakamlilia Mungu, na kwa kilio chao, mto mkubwa uliotiririka maji mengi ukatokea kutoka kitu kilichoonekana kama kijito tu.
10Kulipopambazuka, jua lilichomoza, na wale wanyonge wakapata nguvu, wakawaangamiza adui zao waheshimiwa.[#A:10 Taz 1 Sam 2:8; Luka 1:52.]
11Kwa ndoto hiyo, Mordekai aliona yale aliyodhamiria Mungu kuyafanya. Baada ya kuamka, alikuwa nayo akilini mwake na akatamani kujua kinaganaga maana ya ndoto hiyo siku nzima.
12Mordekai alipokuwa akipumzika kwenye ua wa ikulu pamoja na Gabatha na Thara, matowashi wawili wa mfalme, walinzi wa uani,
13aliwasikia hao matowashi wakizungumza. Akasikiliza kwa makini kile walichokuwa wakizungumzia, kumbe, walikuwa wanakula njama kumuua mfalme. Basi, Mordekai akamwendea mfalme Ahasuero na kumweleza njama za matowashi hao wawili.
14Mfalme akaagiza wahojiwe, na walipokiri njama yao, wakatolewa nje na kunyongwa.
15Mfalme aliamuru kumbukumbu juu ya tukio hilo iandikwe katika kitabu cha kumbukumbu za kifalme, naye Mordekai ndiye aliyeliandika.
16Kisha, mfalme akamweka Mordekai kuwa mhudumu kwenye ua na akampa zawadi kutokana na kuzifichua njama hizo.
17Lakini Hamani mwana wa Hamedatha, wa ukoo wa Bouga, mtu aliyeheshimiwa sana na mfalme, akaanza kutafuta njia ya kumdhuru Mordekai na Wayahudi wengine kwa sababu ndiye aliyehusika na vifo vya wale matowashi wawili wa mfalme.