The chat will start when you send the first message.
1Watu walipoona kuwa Mose amechelewa kurudi kutoka mlimani, walikusanyika mbele ya Aroni na kumwambia, “Haya! Tutengenezee miungu itakayotuongoza maana hatujui lililompata huyo Mose aliyetutoa nchini Misri.”[#32:1—34:35 Sura hizi zinaendeleza lile simulizi lililowekwa kando katika Kut 24:18. Wazo kiini katika sehemu hii ni kuvunjwa kwa lile agano na kurekebishwa kwake (rejea 24:8; 34:10; taz 32:19). Katika simulizi hili Mwenyezi-Mungu anajidhihirisha kuwa mwenye huruma na mwenye kusamehe dhambi.; #32:1 Yaani sanamu au vinyago vya mungu (32:4). Kufanya hivyo ilikuwa kuvunja amri ya Mungu (20:3-5; taz pia Eze 20:16; Kut 24:18; Kumb 9:6-29; Isa 41:6-7; Mate 7:40).]
2Aroni akawajibu, “Chukueni vipuli vya dhahabu masikioni mwa wake zenu, wana wenu na binti zenu, mniletee.”
3Basi, watu wote wakatoa vipuli vyote vya dhahabu masikioni mwao, wakamletea Aroni.
4Naye akavichukua akaviyeyusha, akatengeneza ndama wa kusubu. Watu wakapaza sauti, “Ee Israeli, huyu ndiye mungu wetu aliyetutoa nchini Misri.”[#32:4 Sanamu hiyo ilikuwa mfano wa fahali (labda aliyefanana na fahali-mungu Apis aliyeabudiwa kule Misri au nchini Kanaani). Miaka mingi baadaye naye Yeroboamu mfalme wa utawala wa kaskazini alitengeneza fahali wawili wa kuabudiwa mjini Betheli na Dani (1Fal 12:26-30).]
5Kisha Aroni akamjengea huyo ndama madhabahu, halafu akatangaza, “Kesho kutakuwa na sikukuu kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu.”
6Kesho yake watu waliamka mapema wakatoa sadaka za kuteketezwa, na sadaka za amani. Watu wakaketi chini kula na kunywa; kisha wakasimama na kucheza.
7Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Teremka chini kwa maana watu wako uliowaleta kutoka nchini Misri wamejipotosha wenyewe;
8wameiacha mara moja njia niliyowaamuru, wakajifanyia ndama wa kusubu, nao wamemwabudu na kumtolea tambiko wakisema, ‘Ee Israeli, huyu ndiye mungu wetu aliyetutoa nchini Misri!’
9Nawafahamu watu hawa; wao wana vichwa vigumu.
10Sasa, usijaribu kunizuia. Niache niwaangamize kwa ghadhabu kali; kisha kutokana nawe nitaunda taifa kubwa.”
11Lakini Mose akamsihi Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, akisema, “Ee Mwenyezi-Mungu, kwa nini hasira yako inawaka vikali dhidi ya watu wako uliowatoa nchini Misri kwa uwezo mkuu na mkono wenye nguvu?
12Ukifanya hivyo, hakika Wamisri watasema, ‘Aliwatoa kwa nia mbaya ili kuwaulia mlimani na kuwateketeza kabisa duniani.’ Ee Mwenyezi-Mungu, tuliza hasira yako kali na kuacha jambo hilo baya ulilokusudia kufanya dhidi ya watu wako.
13Wakumbuke watumishi wako, Abrahamu, Isaka na Israeli, ambao uliwaapia kwa nafsi yako mwenyewe, ukisema, ‘Nitawazidisha wazawa wenu kama nyota za mbinguni na nchi yote hii niliyowaahidia nitawapa vizazi vyenu wairithi milele.’”
14Basi, Mwenyezi-Mungu akaacha kuwafanyia watu wake lile jambo baya alilokuwa amesema.[#32:11-14 Kwa mara nyingine maombi ya Mose yanawapatia Waisraeli msamaha kutoka kwa Mwenyezi-Mungu. Taz Hes 14:13-19; Kumb 9:25-29.]
15Kisha Mose akashuka kutoka mlimani akiwa na vibao viwili vya mawe mikononi mwake, vimeandikwa amri za Mungu pande zote.
16Vibao hivyo vilikuwa kazi yake Mungu mwenyewe na maandishi hayo aliyachora Mungu mwenyewe.[#32:16 Taz Kut 31:18. Aya hii yamkini inabainisha kati ya kazi yake Mungu mwenyewe ambayo aliifanya kwa kusimika agano lake na kazi waliyoifanya hao watu kwa kujitengenezea mungu wao.]
17Yoshua aliposikia kelele za watu, akamwambia Mose, “Kuna kelele za vita kambini.”[#32:17 Taz Kut 17:9. Yeye alikuwa amekwenda mlimani pamoja na Mose (24:18).]
18Lakini Mose akamjibu, “Si kelele ya ushindi au kushindwa, bali kelele ninayosikia ni kelele ya watu wanaoimba.”
19Mara tu walipoikaribia kambi walipomwona yule ndama na watu wakicheza; hapo hasira ya Mose ikawaka kama moto, akavitupa chini vile vibao kutoka mikononi mwake na kuvivunja pale chini ya mlima.[#32:19 Ingawa aya hii inaonesha kwamba kuvunjwa kwa vile vibao viwili vya mawe vilivyoandikwa zile amri kumi kulisababishwa na hasira ya Mose, wafafanuzi wengi wanaona hapa kitendo cha ishara kinachoashiria kuvunjwa kwa lile agano au mkataba kati ya Mungu na watu wake. Ndivyo inavyoonekana licha ya kwamba katika aya ya 14 Mose alikwisha waombea na kuwapatia msamaha kutoka kwa Mwenyezi-Mungu.]
20Basi, akamchukua yule ndama akamchoma moto, akamsaga mpaka akawa unga, akaukoroga unga huo katika maji na kuwalazimisha Waisraeli wanywe.[#32:20 Kuwanyweshwa maji hayo kulikuwa ni adhabu kwa dhambi waliyotenda na pia kulikuwa ni njia au namna ya kuangamiza kabisa dalili yoyote ya yule ndama wa dhahabu. Hao hao walioitengeneza ndio hao hao wanaowajibika kuiangamiza.]
21Mose akamwuliza Aroni, “Walikufanya nini watu hawa hata ukawaingiza katika dhambi kubwa hivyo?”
22Aroni akamjibu, “Nakuomba ee bwana wangu hasira yako isiniwakie mimi mtumishi wako. Unawafahamu jinsi watu hawa walivyo tayari kutenda maovu.[#32:22-24 Yamkini Aroni anajitetea kuwa alipofanya alichokifanya, huyo ndama alitokea mwenyewe, kisingizio mithili ya kile cha Adamu katika Mwa 3:12.]
23Walikuja wakaniambia, ‘Tufanyie miungu ambayo itatuongoza kwani huyo Mose aliyetutoa nchini Misri hatujui lililompata’.
24Nami nikawaambia, kila mmoja aliye na vito vya dhahabu na avilete. Basi, wakaniletea, nami nikaviyeyusha motoni na huyu ndama akatokea.”
25Basi, Mose alipoona kuwa watu wameasi na kufanya wapendavyo (kwa kuwa Aroni aliwafanya waasi na kufanya wapendavyo, na kujiletea aibu mbele ya adui zao),
26Mose akasimama mbele ya lango la kambi na kuuliza, “Ni nani aliye upande wa Mwenyezi-Mungu? Na aje kwangu.” Wana wote wa Lawi wakakusanyika pamoja mbele yake.
27Akawaambia, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, anasema hivi: ‘Kila mtu na ajifunge upanga wake kiunoni, azunguke kila mahali kambini, kutoka lango moja hadi lingine, na kila mmoja amuue ndugu yake, rafiki yake na jirani yake.’”
28Wana wa Lawi wakafanya kama Mose alivyowaagiza. Siku hiyo waliuawa watu wapatao 3,000.
29Mose akasema, “Leo mmejiweka wakfu nyinyi wenyewe kumhudumia Mwenyezi-Mungu, kwa vile hamkusita hata kuwaua watoto wenu au ndugu zenu. Mungu awajalie baraka leo hii.”[#32:29 Neno la Kiebrania lililotafsiriwa “kuweka wakfu” au “kutenga kwa ajili ya dini” au kwa ajili ya Mungu, ni lile lile linalotumiwa kwa makuhani au makasisi wa A.K. Lakini kulingana na mapokeo, Walawi hawakuwekwa wakfu wote, ila ni wale tu waliokuwa wa ukoo wa Aroni (taz Kut 29:9). Taz pia Hes 18:20-32.]
30Kesho yake Mose akawaambia watu, “Mmetenda dhambi kubwa! Sasa nitamwendea Mwenyezi-Mungu juu mlimani; labda nitafanya upatanisho kwa ajili ya dhambi yenu.”
31Hivyo Mose akarudi kwa Mwenyezi-Mungu, akamwambia, “Nasikitika! Watu hawa wametenda dhambi kubwa; wamejifanyia wenyewe miungu ya dhahabu.
32Lakini sasa, nakuomba uwasamehe dhambi yao. Ikiwa hutawasamehe, nakusihi unifute mimi katika kitabu chako ulichowaandika watu wako.”[#32:32 Maneno yanayoonesha moyo wa huruma wa Mose; yu tayari kufa kwa ajili ya wengine. Na kuhusu kitabu cha Mungu, iliaminiwa kwamba kuna kitabu ambamo matendo ya binadamu yameandikwa (taz pia Zab 56:8; 69:28; 139:16; Isa 34:16; Dan 7:10; 9:2; 12:1; Mal 3:16). Katika Agano Jipya kitabu hicho kinajulikana kama “kitabu cha uhai” Fil 4:3; Ufu 3:5; 5:1-5,7-9; 10:2,8-10; 13:8; 17:8; 20:12,15; 21:27; taz pia Ufu 22:19.]
33Lakini Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Nitamfuta katika kitabu changu mtu yeyote aliyenitendea dhambi.
34Lakini sasa nenda ukawaongoze watu mpaka mahali nilipokuambia. Tazama, malaika wangu atakutangulia. Hata hivyo, siku nitakapowajia, nitawaadhibu kwa sababu ya dhambi yao.”[#32:34 Hapa, ile ahadi ya Kut 23:20 inarudiwa tena. Lakini dhambi ya Waisraeli na kuvunjwa kwa lile agano vinasababisha mabadiliko ya kimsingi kuhusu uhusiano wa Waisraeli na Mungu (taz aya 10). Hivyo malaika au mjumbe hapa hatumiki tena kama ishara ya kuweko kwa Mungu mwenyewe kati ya watu wake (taz Kut 33:3) ila anatumika kuonesha umbali wa kiasi kati ya Mungu na hao watu, maaana kuweko kwa Mungu karibu na hao watu kutamfanya awaangamize hao wenye dhambi (Kut 33:5).]
35Mwenyezi-Mungu akawapelekea watu ugonjwa wa tauni, kwa kuwa walimwomba Aroni awafanyie yule ndama wa dhahabu.