The chat will start when you send the first message.
1Baadaye mwezi wa saba ulipofika, na watu wa Israeli wakiwa wamekwisha kaa katika miji yao, wote walikusanyika pamoja mjini Yerusalemu.[#3:1 Yapata tangu katikati ya mwezi Septemba mpaka katikati ya mwezi Oktoba katika kalenda yetu. Mwezi huo uliitwa Tishri katika kalenda ya Kiebrania na katika mwezi huo kulikuwa na sikukuu mbalimbali za kidini kama vile ile sikukuu ya vibanda (aya 4). Mwaka unaohusika bila shaka ulikuwa mwaka 538 K.K. ambao ulikuwa pia mwaka wa kwanza wa utawala wa Koreshi.]
2Yeshua, mwana wa Yosadaki, pamoja na makuhani wenzake, na Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, pamoja na jamaa zake, waliijenga upya madhabahu ya Mungu wa Israeli, ili waweze kumtolea sadaka za kuteketezwa kama ilivyoandikwa katika sheria ya Mose, mtu wa Mungu.
3Waliijenga madhabahu hiyo mahali palepale ilipokuwa hapo zamani, kwa kuwa waliwaogopa watu waliokuwa wanaishi katika nchi hiyo. Kisha wakawa wanamtolea Mwenyezi-Mungu sadaka za kuteketezwa juu yake kila siku asubuhi na jioni.[#3:3 Hao walikuwa wageni ambao Waashuru walikuwa wamewashurutisha kukaa katika eneo la Yerusalemu.]
4Waliiadhimisha sikukuu ya vibanda kama ilivyoandikwa katika sheria; kila siku walitoa sadaka za kuteketezwa zilizohitajika kwa ajili ya siku hiyo.
5Walitoa pia sadaka za kawaida ambazo ziliteketezwa nzima, sadaka zilizotolewa wakati wa sikukuu ya mwezi mpya na katika sikukuu nyingine zote alizoagiza Mwenyezi-Mungu. Pia, walitoa tambiko zote zilizotolewa kwa hiari.[#3:4-5 Sikukuu ya vibanda iliwakumbusha Waisraeli jinsi Mungu alivyowalinda wazee wao kule jangwani (taz Lawi 23:33-36; Hes 29:12-38). Sikukuu ya mwezi mpya iliadhimisha mwanzo wa mwezi katika kalenda ya Wayahudi (Hes 28:11-15).]
6Ingawa msingi wa hekalu la Mwenyezi-Mungu ulikuwa bado kuwekwa, watu walianza kutoa sadaka za kuteketezwa tangu siku ya kwanza ya mwezi wa saba.
7Watu walitoa fedha za kuwalipa maseremala na waashi, walitoa pia chakula, vinywaji na mafuta, ili vipelekwe katika miji ya Tiro na Sidoni kupata miti ya mierezi kutoka Lebanoni. Miti hiyo ililetwa kwa njia ya bahari hadi Yopa. Haya yote yalifanyika kwa msaada wa mfalme Koreshi wa Persia.[#3:7 Lugha inayotumiwa hapa inakumbusha vifaa na vitu vingine katika ile shughuli ya ujenzi wa hekalu la Solomoni (1 Nya 22:2-4; 2Nya 2:8-16).]
8Basi, watu walianza kazi mnamo mwezi wa pili wa mwaka wa pili baada ya kufikia nyumba ya Mungu mjini Yerusalemu. Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, Yeshua mwana wa Yosadaki, ndugu zao wengine, makuhani, Walawi na watu wengine wote waliorudi Yerusalemu kutoka uhamishoni, walijiunga nao katika kazi hiyo. Walawi wote waliokuwa na umri wa miaka ishirini au zaidi, waliteuliwa ili kusimamia kazi ya kuijenga upya nyumba ya Mwenyezi-Mungu.[#3:8 Mwezi wa pili katika kalenda ya Kiebrania ni yapata katikati ya mwezi Aprili mpaka katikati ya mwezi Mei katika kalenda yetu. Na mwaka wa pili ni mwaka 536 K.K.]
9Yeshua, wanawe na jamaa yake, pamoja na Kadmieli na wanawe, (wa ukoo wa Yuda) walishirikiana kusimamia ujenzi wa nyumba ya Mungu. Walisaidiwa na wazawa wa Henadadi na ndugu zao Walawi.
10Wajenzi walipoanza kuweka msingi wa hekalu la Mwenyezi-Mungu, makuhani wakiwa wamevalia mavazi yao rasmi, walisimama mahali pao na tarumbeta mikononi, nao Walawi wa ukoo wa Asafu wakisimama na matoazi yao; basi, walimtukuza Mwenyezi-Mungu kufuatana na maagizo ya mfalme Daudi wa Israeli.
11Waliimba kwa kupokezana, wakimsifu na kumtukuza Mwenyezi-Mungu:
“Kwa kuwa yu mwema,
fadhili zake kwa Israeli zadumu milele.”
Watu wote walipaza sauti kwa nguvu zao zote, wakamsifu Mwenyezi-Mungu kwa sababu ya kuanza kujengwa msingi wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu.
12Wengi wa makuhani, Walawi, na viongozi wa koo waliokuwa wazee na ambao walikuwa wameiona nyumba ya kwanza, walilia kwa sauti kubwa walipouona msingi wa nyumba hii mpya unawekwa, ingawa watu wengine wengi walipaza sauti kwa furaha.
13Watu hawakuweza kutofautisha kati ya sauti za furaha na za kilio kwa sababu zilikuwa nyingi na zilisikika mbali sana.