Waebrania 1

Waebrania 1

Mungu anasema kwa njia ya Mwanae

1Hapo zamani, Mungu alisema na babu zetu mara nyingi kwa namna nyingi kwa njia ya manabii,[#1:1 Yaani, vizazi vilivyotangulia nyakati za A.K.; #1:1 Kwa jumla ni waandishi wa A.K.]

2lakini siku hizi za mwisho, amesema nasi kwa njia ya Mwanae. Yeye ndiye ambaye kwa njia yake Mungu aliumba ulimwengu, akamteua avimiliki vitu vyote.[#1:2-3 Kama vile katika Yoh 1:1-3,14-18; 1Kor 8:6; Kol 1:15-17, Mwana wa Mungu ambaye kwa njia yake Mungu aliumba ulimwengu (aya ya 2) na kutegemeza vitu vyote, ndiye aliyeongea nasi akitufunulia habari za Mungu. Taz Yoh 1:1 maelezo.]

3Yeye ni mng'ao wa utukufu wa Mungu, na mfano kamili wa hali ya Mungu mwenyewe, akiutegemeza ulimwengu kwa neno lake lenye nguvu. Baada ya kuwatakasa binadamu dhambi zao, ameketi huko juu mbinguni, upande wa kulia wa Mungu Mkuu.[#1:3 Rejea Yoh 1:4-9,14.; #1:3 Yahusu kazi yake Yesu ya kikuhani, wazo ambalo mwandishi atalieleza kinaganaga katika Ebr 9:11—10:18.; #1:3 Mahali pa heshima, fahari na utukufu. Hii ni namna kawaida ya A.J. ya kusema juu ya kutukuzwa kwake Yesu Kristo (Marko 14:62; Luka 22:69; Mate 2:33). Msemo huo umepata msingi wake katika Zab 110:1 sehemu ambayo imenukuliwa pia katika Ebr 1:13; taz pia 8:1; 10:12; 12:2.]

Ukuu wa Mwana wa Mungu

4Mwana ni mkuu kuliko malaika, kama vile jina alilopewa na Mungu ni kuu kuliko jina lao.[#1:4 Kwa Wayahudi jina sio tu njia ya kumtambulisha mtu; jina lilihusu pia hali yote ya mtu na nafsi yake. Lilionesha cheo na kazi ya mtu. Rejea 1:2,5.]

5Maana Mungu hakumwambia kamwe hata mmoja wa malaika wake:[#1:5 Zab 2:7 (kulingana na LXX). Katika A.K. Zaburi hii ilihusu kutawazwa kwa mfalme wa Israeli wakati wa kutawazwa kwake, lakini sasa inatumika katika A.J. kuhusu Masiha (taz Mate 13:33).]

“Wewe ni Mwanangu;

mimi leo nimekuwa Baba yako.”

Wala hakusema juu ya malaika yeyote:

“Mimi nitakuwa Baba yake,

naye atakuwa Mwanangu.”

6Lakini Mungu alipokuwa anamtuma Mwanae, mzaliwa wa kwanza, ulimwenguni alisema:

“Malaika wote wa Mungu na wamwabudu.”

7Lakini kuhusu malaika, alisema:

“Amewafanya malaika wake kuwa upepo,

na wahudumu wake ndimi za moto.”

8Lakini kuhusu Mwana, Mungu alisema:

“Kiti chako cha enzi, ee Mungu, chadumu milele na milele!

Wewe wawatawala watu wako kwa haki.

9Wewe wapenda uadilifu na kuchukia uovu.

Ndiyo maana Mungu, Mungu wako, amekuweka wakfu

na kukumiminia furaha kubwa kuliko wenzako.”

10Na tena:

“Bwana, wewe uliumba dunia hapo mwanzo,

mbingu ni kazi ya mikono yako.

11Hizo zitatoweka, lakini wewe wabaki daima,

zote zitachakaa kama vazi.

12Utazikunjakunja kama koti,

nazo zitabadilishwa kama vazi.

Lakini wewe ni yuleyule daima,

na maisha yako hayatakoma.”

13Mungu hakumwambia kamwe hata mmoja wa malaika wake:

“Keti upande wangu wa kulia,

mpaka niwaweke adui zako chini ya miguu yako.”

14Malaika ni nini ila roho wanaomtumikia Mungu na ambao hutumwa kuwasaidia wale watakaopokea wokovu?[#1:5-14 Mwandishi ananukuu kwa mfululizo sehemu saba za A.K. ambazo anazichukua kama sehemu za kinabii zinazohusika na Masiha na kuonesha kwamba Yesu Kristo ni mkuu kuliko malaika na viumbe vyote.; #1:14 Rejea Zab 34:7; 91:11; Mat 4:11; Luka 1:19. Malaika katika Kiebrania lina maana ya mjumbe na hutaja viumbe wa mbinguni ambao wana uhusiano wa pekee na Mungu kama wajumbe wake. Mwandishi anasema kwamba Yesu naye pia alikuwa mjumbe wa Mungu lakini yeye ni mkuu kuwapita malaika na ndiyo maana wanamwabudu. Taz pia malaika katika Fahirisi.; #1:14 Ukombozi. Mwandishi ataendeleza wazo hili la ukombozi au wokovu katika Ebr 2:3-4,10,14-18; na kusimulia kazi ya Yesu Kristo ya ukombozi hasa katika sura 7—10.]

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania