Hosea 1

Hosea 1

1Neno la Bwana lililomjia Hosea mwana wa Beeri, nyakati za Uzia, Yothamu, Ahazi na Hezekia, wafalme wa Yuda, na Yeroboamu mwana wa Yoashi, mfalme wa Israeli.[#1:1 Vitabu vingi vya manabii vinaanza kwa maneno kama hayo. Taz Isa 1:1 maelezo.]

Mke na watoto wa Hosea

2Mwenyezi-Mungu alipoanza kuongea na Waisraeli kwa njia ya Hosea, alimwambia hivi: “Nenda ukaoe mwanamke mzinzi, uzae naye watoto wa uzinzi, maana watu wa nchi hii wanafanya uzinzi mwingi kwa kuniacha mimi.”[#1:2 Manabii kadhaa wanatumia vitendo vya mfano kuwapa watu ujumbe wa Mungu. Hapa kitendo cha mfano au ishara cha Hosea kilikuwa na lengo la kuwaonya Waisraeli juu ya hali yao ya kukosa uaminifu kwa Mwenyezi-Mungu. Katika Kiebrania si dhahiri kwamba huyo mwanamke alikuwa mzinzi kabla ya kuolewa au baadaye.]

3Basi, Hosea akaenda, akamwoa Gomeri, binti Diblaimu. Gomeri akapata mimba, akamzalia Hosea mtoto wa kiume.

4Mwenyezi-Mungu akamwambia Hosea, “Mpe mtoto huyo jina ‘Yezreeli’, maana bado kitambo kidogo tu, nami nitaiadhibu jamaa ya Yehu kwa mauaji aliyoyafanya bondeni Yezreeli. Nitaufutilia mbali ufalme katika taifa la Israeli.[#1:4 Jina hili lina maana ya “Mungu hutawanya (mbegu)” na hapa linatumika kama tisho kwa Waisraeli: Mungu atawaadhibu na kuwatawanya kama mkulima anavyotawanya mbegu. Lakini jina hilo hilo linatumika katika mazingira ambayo linachukua maana nzuri ya baraka kama baraka ya mazao mengi ambapo mbegu zinatawanywa.; #1:4 Mnamo mwaka 722 Waashuru baada ya kuivamia nchi ya mfalme Hoshea (ufalme wa kaskazini), Samaria mji wake mkuu uliteketezwa na wakazi wake wengi wakapelekwa uhamishoni Ashuru (2Fal 17:5-6).]

5Siku hiyo, nitazivunja nguvu za kijeshi za Israeli huko bondeni Yezreeli.”

6Gomeri alipata mimba tena, akazaa mtoto wa kike. Mwenyezi-Mungu akamwambia Hosea, “Mpe mtoto huyo jina ‘Asiyehurumiwa’, maana sitawahurumia tena Waisraeli wala sitawasamehe.[#1:6 Jina hili la mfano ni picha ya kuelezea kwamba upendo wa Mungu na uangalizi wake kwa Waisraeli sasa umeondolewa.]

7Lakini nitawahurumia watu wa Yuda na kuwaokoa. Mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, nitawaokoa, lakini si kwa nguvu za kijeshi, au pinde, au panga, au farasi au wapandafarasi.”[#1:7 Ujumbe wa Hosea ulielekezwa hasa kwa utawala wa kaskazini wa Israeli. Kwamba hapa anataja ufalme wa kusini wa Yuda inawezekana kwamba ni jaribio la kuonesha mji wa Yerusalemu ulivyoepa kuteketezwa na majeshi ya Senakeribu mwaka 701 K.K. (Taz 2Fal 19:32-37).]

8Gomeri alipomwachisha kunyonya “Asiyehurumiwa,” alipata mimba tena, akamzalia Hosea mtoto mwingine wa kiume.

9Mwenyezi-Mungu akamwambia Hosea, “Mpe mtoto huyo jina ‘Siwangu,’ maana nyinyi si watu wangu, wala mimi si wenu.”[#1:9 Katika agano la Mungu na Waisraeli liliwafanya wawe watu wake Mungu na Mungu kuwa Mungu wao (Kut 6:7; Lawi 26:12; Kumb 26:17-19; Yer 7:23). Sasa uhusiano huo wa agano au “mma” unaondolewa kwa sababu ya utovu wa uaminifu wao.]

Hali ya Israeli itarekebishwa

10Lakini idadi ya Waisraeli itakuwa kubwa kama mchanga wa pwani ambao haupimiki wala hauhesabiki. Pale ambapo Mungu aliwaambia, “Nyinyi si watu wangu,” sasa atawaambia, “Nyinyi ni watoto wa Mungu aliye hai.”[#1:10-11 Hapa Hosea anaona wakati ujao ambapo Mungu atarekebisha tena hali ya watu wake na kuwaunganisha chini ya kiongozi mmoja (taz ahadi hiyo katika Mwa 22:17; 32:12). “Ninyi ni watoto wa Mungu aliye hai”: Fungu la maneno ambalo linakaririwa katika Rom 9:26.]

11Watu wa Yuda na wa Israeli wataungana pamoja na kumchagua kiongozi wao mmoja; nao watastawi katika nchi yao. Hiyo itakuwa siku maarufu ya Yezreeli.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania