Hosea 4

Hosea 4

Mungu awalaumu watu wake

1Msikilizeni Mwenyezi-Mungu,

enyi Waisraeli.

Mwenyezi-Mungu anawashutumu wakazi wa nchi hii.

“Hamna tena uaminifu wala wema nchini;

hamna anayemjua Mungu katika nchi hii.

2Kuapa, uongo, mauaji, wizi na uzinzi huzuka humo.

Umwagaji damu hufuatana mfululizo.

3Kwa hiyo, nchi yote ni kame,

wakazi wake wote wanaangamia

pamoja na wanyama wa porini na ndege;

hata samaki wa baharini wanaangamizwa.

Mungu anawashutumu makuhani

4“Lakini watu wasilaumiwe, wasishutumiwe;

maana mimi nakushutumu wewe kuhani.

5Wewe utajikwaa mchana,

naye nabii atajikwaa pamoja nawe usiku.

Nitamwangamiza mama yako Israeli.

6Watu wangu wameangamia kwa kutonijua,

maana wewe kuhani umekataa mafundisho.

Nimekukataa kuwa kuhani wangu.

Kwa kuwa umeisahau sheria ya Mungu wako,

nami pia nitawasahau watoto wako.

7“Kadiri makuhani walivyoongezeka,

ndivyo wote walivyozidi kuniasi.

Basi, nitaigeuza fahari yao kuwa aibu.

8Wanajishibisha kwa sadaka za watu wangu wenye dhambi.

Wana hamu sana ya kuwaona wametenda dhambi.

9Lakini yatakayowapata watu yatawapata makuhani;

nitawaadhibu kwa sababu ya mwenendo wao,

nitawalipiza matendo yao wenyewe.

10Watakula, lakini hawatashiba;

watazini, lakini hawatapata watoto,

kwa sababu wameniacha mimi Mwenyezi-Mungu,

na kufuata miungu mingine.

Mungu alaani ibada za miungu

11“Divai mpya na ya zamani

huondoa maarifa.

12Watu wangu huomba shauri kutoka kwa mti;[#4:12 Nabii hapa anatumia lugha ya dhihaka kudhihaki mungu wa uongo “mti” na “kijiti”. Neno “mti” hapa laweza kuwa linatumiwa kutaja kinyago cha mungu kama katika Kumb 4:28. Lakini hapa huenda ni mti wa kweli ambao uliwakilisha mungu wa kike Ashera ambaye alikuwa mke wa mungu Baali. Na hicho “kijiti” kilitumiwa kujaribu kujua matakwa ya Mungu.]

kijiti chao cha ramli ndicho kinachowapa kauli.

Nia ya kufanya uzinzi imewapotosha;

wamefanya uzinzi kwa kufuata miungu mingine,

wakaniacha mimi Mungu wao.

13Wanatambikia kwenye vilele vya milima;

naam, wanatoa tambiko vilimani,

chini ya mialoni, migude na mikwaju,

maana kivuli chao ni kizuri.

“Kwa hiyo binti zenu hufanya uzinzi,

na bibiarusi wenu hufanya uasherati.

14Lakini sitawaadhibu binti zenu wanapofanya uzinzi,[#4:14 Neno la Kiebrania la uzinzi ni “zenah”. Ndiyo kusema, neno letu la Kiswahili la “mzinzi” limetufikia katika msamiati wetu kutokana na lugha ya awali ya dhambi hiyo, labda kwa kupitia Kiarabu.]

wala bibi arusi wenu wanapofanya uasherati,

maana, wanaume wenyewe ndio wanaofuatana na wazinzi,

na kutambikia pamoja nao katika ibada za uzinzi.

Watu hawa watovu wa akili hakika wataangamia!

15“Ama kweli nyinyi Waisraeli ni wazinzi!

Lakini, msiwafanye watu wa Yuda wawe na hatia!

Msiende mahali patakatifu huko Gilgali,

wala msiende kule Beth-aveni.

Wala msiape mkisema,

‘Kama Mwenyezi-Mungu aishivyo!’”

16Waisraeli ni wakaidi kama punda.

Kwa nini basi Mungu ashughulike kuwachunga,

kama kondoo kwenye malisho mapana?

17“Watu wa Efraimu wamejifunga na sanamu.[#4:17 Taz Yos 16:4-10. Kabila la Waisraeli lililokuwa kaskazini. Walikugeuka wakaabudu sanamu ya ndama wa dhahabu. (Taz 8:5, 13:2; 1Fal 12:28). Mungu wa Baali (Hos 2:8,13).]

Haya! Waache waendelee tu!

18Kama vile genge la walevi,[#4:18 Aya hii katika makala ya Kiebrania si dhahiri.; #4:18 Au, “Kundi la walevi”.]

wanajitosa wenyewe katika uzinzi;

wanapendelea aibu kuliko heshima yao.

19Basi, kimbunga kitawapeperusha,[#4:19 Taz Zab 18:10; 104:3; Jer 4:11-12. Huonesha hali ya ugomvi utakaoletwa na mashujaa watakaoiteka Israeli. Hatimaye wapate kutambua miungu waliyoifuata haina uwezo wowote. Taz Hos 10:6. Ling aya ya 16.]

na watayaonea aibu matambiko yao kwa miungu ya uongo.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania