The chat will start when you send the first message.
1Kutatokea chipukizi katika kisiki cha Yese,[#11:1 Yese alikuwa baba yake Daudi na chimbuko (kisiki) la ukoo wake (1Sam 16:1-20). Kutoka chimbuko hilohilo kutatokea “chipukizi” au “mche” maalumu. Picha hii inakaririwa katika Roma 15:12; Ufu 5:5; 22:16 (na kwa maneno yanayofanana katika Yer 23:5; 33:15; Zek 3:8; 6:12).]
tawi litachipua mizizini mwake.
2Roho ya Mwenyezi-Mungu itakaa kwake,[#11:2 Yaani nguvu na msaada wa pekee wa Mungu. Katika nabii Ezekieli mara nyingi msemo “roho ya Mwenyezi-Mungu ilikuwa juu yangu” unatumiwa kuonesha nguvu yake Mwenyezi-Mungu ambayo inamwongoza na kumwezesha. Hapa roho ya Mwenyezi-Mungu itampa uwezo wa kutawala. Maneno “roho ya hekima” yana lengo la kuonesha kwamba hekima ni muhimu katika kutawala vema (1Fal 3:8-9) na ni mojawapo ya sifa za mfalme mzuri.]
roho ya hekima na maarifa,
roho ya shauri jema na nguvu,
roho ya ujuzi na ya kumcha Mwenyezi-Mungu.
3Atafurahia kumcha Mwenyezi-Mungu.
Hatahukumu kadiri ya mambo ya njenje,
wala kuamua kufuatana na yale anayosikia.
4Atawapatia haki watu maskini,
atawaamulia sawasawa wanyonge nchini.
Kwa neno lake ataiadhibu dunia,
kwa tamko lake atawaua waovu.
5Haki itakuwa kama mkanda wa kujifunga,
uaminifu utakaa naye kama mkanda kiunoni.
6Mbwamwitu ataishi pamoja na mwanakondoo,
chui watapumzika pamoja na mwanambuzi.
Ndama na wanasimba watakula pamoja,
na mtoto mdogo atawaongoza.
7Ng'ombe na dubu watakula pamoja,
ndama wao watapumzika pamoja;
na simba atakula majani kama ng'ombe.
8Mtoto mchanga atacheza kwenye shimo la nyoka
mtoto ataweza kutia mkono shimoni mwa nyoka wa sumu.
9Katika mlima mtakatifu wa Mungu[#11:9 Taz Zab 2:6.]
hakutakuwa na madhara wala uharibifu.
Maana kumjua Mwenyezi-Mungu kutaenea pote nchini,
kama vile maji yajaavyo baharini.
10Siku ile chipukizi wa Yese atakuwa ishara kwa mataifa; mataifa yatamtafuta na makazi yake yatatukuka.
11Siku hiyo, Bwana ataunyosha mkono wake tena kuwarejesha watu wake waliosalia huko Ashuru, Misri, Pathrosi, Kushi, Elamu, Shinari, Hamathi na sehemu za pwani.[#11:11-16 Kisehemu hiki chagusia kurudi kwa wale Waisraeli waliopelekwa uhamishoni Babuloni (11-12 taz Mika 7:12; Zek 10:8-10). Wazo hili kuu au dhamira ni jambo muhimu katika Isa 40—55.; #11:11 Sehemu ya kusini mwa Misri. “Kushi” ni eneo kusini mwa Misri ambalo kwa sasa lajumuisha Ethiopia, Sudani, Eritrea na hata sehemu za kaskazini za Afrika Mashariki. “Elamu” ilikuwa sehemu ya kusini-mashariki ya Mesopotamia ambapo kwa sasa ni nchi ya Irani. “Shinari” ni jina lingine la Babuloni na “Hamathi” ulikuwa mji wa Siria. Ashuru iliwateka maelfu ya Wayahudi kutoka utawala wa kaskazini (Israeli) katika miaka ya 722-720 K.K. na kutoka utawala wa kusini (Yuda) mnamo mwaka 701 K.K. Huenda pia kwamba wengi pia walitorokea Misri na Kushi (eneo la sasa Ethiopia na Sudani). Kwa upande mwingine Babuloni nayo iliiteka Yuda na kuwahamisha wakazi wake wengi na kuwapeleka katika sehemu mbalimbali zilizokuwa chini ya utawala wa Wababuloni.]
12Naye atatweka bendera kuwaashiria mataifa,
kuwakusanya Waisraeli waliodharauliwa,
kuwaleta pamoja watu wa Yuda waliotawanywa,
na kuwarudisha toka pembe nne za dunia.
13Wivu wa Efraimu juu ya Yuda utakoma,
hakutakuwa tena na uadui kati ya Yuda na Efraimu.
14Wote pamoja watawavamia Wafilisti walio magharibi,
pamoja watawapora watu wakaao mashariki.
Watawashinda Waedomu na Wamoabu,
nao Waamoni watawatii.
15Mwenyezi-Mungu atakausha ghuba ya bahari ya Shamu,[#11:15 Kiebrania ni “bahari ya Misri”. Picha tunayopewa hapa inatoa wazo kwamba kama vile wakati ule wa kutoka Misri ambapo Mungu alikausha maji Waisraeli wakapita pakavu, vivyo hivyo na sasa, “Kutoka Kupya”, atawafanya warudi makwao (taz Kut 14; Yer 23:7-8 na Ufu 16:12).]
kwa pumzi yake ichomayo atakausha mto Eufrate,
nao utagawanyika katika vijito saba,
watu wavuke humo miguu mikavu.
16Tena, kutakuwa na barabara kuu toka Ashuru
kwa ajili ya watu wake waliobaki humo
kama ilivyokuwa kwa Waisraeli
wakati walipotoka nchini Misri.