Isaya 13

Isaya 13

Mungu ataiadhibu Babuloni

1Kauli ya Mungu dhidi ya Babuloni ambayo Isaya, mwana wa Amozi, alipewa katika maono:[#13:1 Neno la Kiebrania linalotafsiriwa hapa ni “masa” ambalo laweza kutafsiriwa neno kwa neno kama “kuinua sauti” au kubeba “mzigo”. Mara nyingi katika maandishi ya manabii neno hilo latumika kuanzisha ujumbe wa kinabiii (taz hasa 15:1; 17:1; 19:1; 21:1 n.k.). Mahali pengine linafuatiwa moja kwa moja na “Neno la Mwenyezi Mungu”. Si rahisi kujua kikamilifu mazingira ya kihistoria ambayo yanahusu au yanaendana na ujumbe huu dhidi ya “Babuloni”. Wakati wa Isaya Babuloni ulikuwa chini ya mamlaka ya Ashuru. Mnamo miaka 708 - 689 Ashuru ilibidi kuzima maasi manne tofauti yaliyoongozwa na viongozi Wakaldayo wa Babuloni (taz 13:19).; #13—23 Sehemu hii kubwa yahusu maaguzi dhidi ya mataifa mengine ambayo yalikuwa kwa namna moja au nyingine maadui wa Waisraeli. Maaguzi ya namna hiyohiyo yanapatikana pia katika Yer 46—51; Eze 25—32 na Amo 1:3-2:6.]

2Mungu asema:

“Twekeni bendera juu ya mlima usio na miti.

Wapaazieni sauti askari

wapungieni watu mkono

waingie malango ya mji wa wakuu.

3Mimi nimewaamuru wateule wangu,

nimewaita mashujaa wangu,

hao wenye kunitukuza wakishangilia,

waje kutekeleza lengo la hasira yangu.”

4Sikilizeni kelele milimani

kama za kundi kubwa la watu!

Sikilizeni kelele za falme,

na mataifa yanayokusanyika!

Mwenyezi-Mungu wa majeshi

analikagua jeshi linalokwenda vitani.

5Wanakuja kutoka nchi za mbali,

wanatoka hata miisho ya dunia:

Mwenyezi-Mungu na silaha za hasira yake

anakuja kuiangamiza dunia.

6Lieni maana siku ya Mwenyezi-Mungu imekaribia;

inakuja kama maafa kutoka kwa Mungu Mwenye Nguvu.

7Kwa hiyo mikono ya kila mtu italegea,

kila mtu atakufa moyo.

8Watu watafadhaika,

watashikwa na hofu na maumivu,

watakuwa na uchungu kama mama anayejifungua.

Watatazamana kwa mashaka,

nyuso zao zitawaiva kwa haya.

9Siku ya Mwenyezi-Mungu inakuja,

siku kali, ya ghadhabu na hasira kali.

Itaifanya nchi kuwa uharibifu,

itawaangamiza wenye dhambi wake.

10Nyota na vilimia vyake angani hazitaangaza;

jua linapochomoza litakuwa giza,

na mwezi hautatoa mwanga wake.

11Mwenyezi-Mungu asema hivi:

“Nitauadhibu ulimwengu kwa uovu wake,

waovu kwa sababu ya makosa yao.

Nitakikomesha kiburi cha wenye majivuno,

na kuporomosha ubaradhuli wa watu katili.

12Nitawafanya watu kuwa wachache kuliko dhahabu safi;

binadamu watakuwa wachache kuliko dhahabu ya Ofiri.

13Nitazitetemesha mbingu

nayo nchi itatikisika katika misingi yake

kwa sababu ya ghadhabu yangu Mwenyezi-Mungu

siku ile ya hasira yangu kali.

14“Kama swala anayewindwa,

kama kondoo wasio na mchungaji,

kila mmoja atajiunga na watu wake

kila mtu atakimbilia nchini mwake.

15Yeyote atakayeonekana atatumbuliwa,

atakayekamatwa atauawa kwa upanga.

16Watoto wao wachanga watapondwapondwa mbele yao,

watanyang'anywa nyumba zao,

na wake zao watanajisiwa.

17“Ninawachochea Wamedi dhidi yao;[#13:17 Hao walikuwa watu wa taifa moja, kaskazini mwa Babuloni. Wakati wa Isaya Wamedi walikuwa chini ya mamlaka ya Ashuru lakini baadaye walijiunga na Wababuloni, wakawashinda Waashuru yapata mwaka 612-609 K.K.]

watu ambao hawajali fedha

wala hawavutiwi na dhahabu.

18Mishale yao itawaua vijana,

hawatakuwa na huruma kwa watoto,

wala kuwahurumia watoto wachanga.

19Babuloni johari ya falme zote

na umaarufu wa kiburi cha Wakaldayo

utakuwa kama Sodoma na Gomora,

wakati Mungu alipoiangamiza.

20Kamwe hautakaliwa tena na watu,

watu hawataishi humo katika vizazi vyote.

Hakuna Mwarabu atakayepiga hema lake humo,

wala mchungaji atakayechunga wanyama wake humo.

21Badala yake watakuwamo wanyama wakali wa porini,

bundi watajaa katika nyumba zake.

Mbuni wataishi humo,

na majini yatachezea humo.

22Mbwamwitu watalia ndani ya ngome zake,

mbweha wataonekana ndani ya nyumba zao za anasa.

Wakati wa Babuloni umekaribia,

wala siku zake hazitaongezwa.”

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania