Isaya 14

Isaya 14

Kurudi kutoka uhamishoni

1Mwenyezi-Mungu atawahurumia tena watu wa Yakobo, atawateua tena Waisraeli. Atawarudisha katika nchi yao wenyewe, na wageni watakuja na kukaa pamoja na watu wa Yakobo.[#14:1-2 Huu ni ujumbe mfupi wa matumaini mema ambao unawaahidi wale watakaorudi kutoka uhamishoni kwamba wataweza kuwatawala hao ambao hapo awali walikuwa wamewafanya kuwa watumwa (taz Isa 60:1-16; 51:5-7).]

2Watu wa mataifa watawasaidia Waisraeli kurudi katika nchi waliyopewa na Mwenyezi-Mungu. Na hapo watawatumikia Waisraeli kama watumwa. Wale waliowateka sasa watatekwa na Waisraeli, na watawatawala wale waliowadhulumu.

Mfalme wa Babuloni miongoni mwa wafu

3Ewe Israeli, wakati Mwenyezi-Mungu atakapokufariji baada ya mateso, misukosuko na utumwa uliofanyiwa,[#14:3 Lugha inayotumika hapa kuelezea hali ya maisha ya Waisraeli waliorudi kutoka uhamishoni Babuloni inafanana na ile inayotumiwa kueleza hali ya maisha utumwani Misri (rejea Kut 1:13-14).; #14:3-23 Aya 3-4 zinatanguliza utenzi wa kishairi wa aya 4-21 kwa kuonesha dhahiri kwamba utenzi huo wamhusu mfalme wa Babuloni.]

4utaimba utenzi huu wa kumdhihaki mfalme wa Babuloni:[#14:4 Huyu labda ni mfalme wa Ashuru aitwaye Sargoni II ambaye aliuawa vitani mwaka 705 K.K. au ni mfalme Senakeribu ambaye jeshi lake lilishindwa mwaka 701 katika vita vilivyotishia mji wa Yerusalemu (Isa 37:36) na ambaye watoto wake walimuua baadaye (Isa 37:37-38). Wakati wa Isaya hao wafalme wa Ashuru waliitwa pia wafalme wa Babuloni kwa vile Babuloni wakati huo ulikuwa chini ya mamlaka ya Ashuru.]

“Jinsi gani mdhalimu alivyokomeshwa!

Ujeuri wake umekomeshwa!

5Mwenyezi-Mungu amelivunja gongo la waovu,

ameivunja fimbo ya kifalme ya watawala,

6ambao walipiga nayo watu kwa hasira bila kukoma,

na kuwatawala kwa udhalimu bila huruma.

7Sasa dunia yote ina utulivu na amani,

kila mtu anaimba kwa furaha.

8Misonobari inafurahia kuanguka kwako,[#14:8 Labda hapa katika sehemu ya kwanza ya aya hii inagusiwa kitendo ambacho hao wafalme walizidi mno katika kuikata misitu kupata miti ya kujengea majumba yao. Kuanguka kwa utawala huo kutaleta nafuu katika hali ya hifadhi ya mazingira!]

nayo mierezi ya Lebanoni pamoja yasema:

‘Kwa vile sasa umeangushwa,

hakuna mkata miti atakayekuja dhidi yetu!’

9“Kuzimu nako kumechangamka,[#14:9 Taz Orodha ya Maneno. Rejea Eze 32:17-32.]

ili kukulaki wakati utakapokuja.

Kunaiamsha mizimu ije kukusalimu

na wote waliokuwa wakuu wa dunia;

huwaamsha kutoka viti vyao vya enzi

wote waliokuwa wafalme wa mataifa.

10Wote kwa pamoja watakuambia:

‘Nawe pia umedhoofika kama sisi!

Umekuwa kama sisi wenyewe!

11Fahari yako imeteremshwa kuzimu

pamoja na muziki wa vinubi vyako.

Chini mabuu ndio kitanda chako,

na wadudu ndio blanketi lako!’

12“Jinsi gani ulivyoporomoshwa toka mbinguni,

wewe uliyekuwa nyota angavu ya alfajiri.

Jinsi gani ulivyoangushwa chini,

wewe uliyeyashinda mataifa!

13Wewe ulijisemea moyoni mwako:

‘Nitapanda mpaka mbinguni;

nitaweka kiti changu juu ya nyota za Mungu,

nitaketi juu ya mlima wakutanapo miungu,

huko mbali pande za kaskazini.

14Nitapanda vilele vya mawingu

nitajifanya kuwa sawa na Mungu Mkuu.’

15Lakini umeporomoshwa hadi kuzimu;[#14:13-15 Mat 11:23; Luka 10:15 (juu ya Kafarnaumu). Taz hasa Ufu 18:10,21.]

umeshushwa chini kabisa shimoni.

16“Watakaokuona watakukodolea macho,

watakushangaa wakisema:

‘Je, huyu ndiye aliyetetemesha dunia

na kuzitikisa falme,

17aliyegeuza dunia kuwa kama jangwa,

akaangamiza miji yake,

na kuwanyima wafungwa wake kurudi kwao?’

18Wafalme wote wa mataifa wamezikwa kwa heshima

kila mmoja ndani ya kaburi lake.

19Lakini wewe umetupwa nje ya kaburi lako;

kama mtoto wa kuchukiza aliyezaliwa mfu

maiti yako imekanyagwakanyagwa,

umerundikiwa maiti za waliouawa kwa upanga,

waliotupwa mashimoni penye mawe.

20Lakini wewe hutaunganishwa nao katika mazishi,

maana uliiharibu nchi yako,

wewe uliwaua watu wako.

Wazawa wa waovu na wasahaulike kabisa!

21Kaeni tayari kuwachinja watoto wake

kwa sababu ya makosa ya baba zao,

wasije wakaamka na kuimiliki nchi,

na kuijaza dunia yote miji yao.”

Mungu ataangamiza Babuloni

22Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: “Nitaushambulia mji wa Babuloni na kuuangamiza kabisa. Nitaharibu kila kitu, mji wote, watoto na yeyote aliyebaki hai. Mimi Mwenyezi-Mungu nimenena.

23Nitaufanya kuwa makao ya nungunungu, na utakuwa madimbwi ya maji. Nami nitaufagilia mbali kwa ufagio wa maangamizi. Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nimenena.”

Mwisho wa udhalimu wote

24Mwenyezi-Mungu wa majeshi ameapa:

“Kama nilivyopanga,

ndivyo itakavyokuwa;

kama nilivyokusudia,

ndivyo itakavyokamilika.

25Nitauvunja uwezo wa Waashuru nchini mwangu;

nitawakanyagakanyaga katika milima yangu.

Nitawaondolea watu wangu nira ya dhuluma yao,

na mzigo wa mateso yao.”

26Huu ndio uamuzi wake Mwenyezi-Mungu

kuhusu dunia yote;

hii ndiyo adhabu atakayotoa

juu ya mataifa yote.

27Kama Mwenyezi-Mungu wa majeshi ameamua,

nani atakayeweza kubatilisha uamuzi wake?

Kama amepania kutoa adhabu,

ni nani atakayempinga?

Mungu atawaangamiza Wafilisti

28Mwaka alipofariki mfalme Ahazi, Mungu alitoa kauli hii:[#14:28 Yapata mwaka 716 K.K. (2Fal 16:20; 2Nya 28:27).]

29“Msishangilie enyi Wafilisti wote,

kwamba Ashuru, fimbo iliyowapiga, imevunjika;

maana, nyoka wa kawaida atazaa nyoka mwenye sumu,

na nyoka mwenye sumu atazaa joka lirukalo.

30Wazaliwa wa kwanza wa maskini watashiba,

na fukara watakaa kwa usalama.

Lakini chipukizi wenu nitawaua kwa njaa;

na yeyote wenu atakayebaki nitamuua.

31Piga yowe ewe lango; lia ewe mji;

yeyuka kwa hofu ewe nchi yote ya Filistia.

Maana moshi wa askari waja kutoka kaskazini,

wala hakuna atakayechelewa katika majeshi yake.”

32Basi watapewa jibu gani wajumbe wa taifa hilo?

Wataambiwa: Mwenyezi-Mungu ameijenga imara Siyoni,

na maskini wa watu wake watakimbilia usalama huko.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania