Isaya 38

Isaya 38

Mfalme Hezekia anaugua

(2 Fal 20:1-11; 2 Nya 32:24-26)

1Wakati huo, mfalme Hezekia aliugua sana karibu kufa. Ndipo nabii Isaya mwana wa Amozi, akamwendea, akamwambia, “Hivi ndivyo anavyosema Mwenyezi-Mungu: Panga mambo yako sawasawa katika nyumba yako kwa kuwa utakufa, hutapona.”[#38:1-20 Simulizi la aya 1-8 (ambalo linamalizika katika aya 21-22) linatofautiana na simulizi sawa na hilo katika 2Fal 20:1-11. Utenzi wa sifa katika aya 9-20 haupo katika 2Fal 20. Utenzi huu unafanana na Zab 6 ambayo ina maombi ya mwandishi wa Zaburi na kumalizia na sifa na shukrani kwa kuwa Mungu ametekeleza ahadi yake.]

2Hezekia akageukia upande wa ukuta na kumwomba Mwenyezi-Mungu,

3akisema, “Ee Mwenyezi-Mungu, nakusihi ukumbuke jinsi nilivyokutumikia kwa uaminifu na kwa moyo wangu wote, na kutenda yaliyo sawa mbele yako.” Hezekia akalia kwa uchungu sana.

4Kisha neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Isaya:

5“Nenda ukamwambie Hezekia, Mwenyezi-Mungu, Mungu wa baba yako Daudi, anasema hivi: Nimesikia ombi lako na nimeyaona machozi yako. Basi, nakuongezea miaka kumi na mitano ya kuishi.

6Nitakuokoa wewe pamoja na mji huu mikononi mwa mfalme wa Ashuru na kuulinda.”

21Basi, Isaya akasema, “Chukueni andazi la tini mkaliweke kwenye jipu lake, apate kupona.”[#38:21 Rejea 2Fal 20:7-8. Sura 38 aya 21-22 zimehamishiwa na kupelekwa mara baada ya aya ya sita na kabla ya aya ya saba ili kuwe na mtiririko wenye kueleweka vizuri zaidi (taz 2Fal 26:6-9).]

22Hezekia akauliza, “Ni ishara gani itakayonijulisha kwamba mimi nitakwenda katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu?”

7Isaya akamjibu, “Hii itakuwa ishara kwako kutoka kwa Mwenyezi-Mungu kwamba Mwenyezi-Mungu atafanya kama alivyoahidi.

8Nitafanya kivuli kwenye ngazi iliyojengwa na Ahazi, kirudi nyuma hatua kumi.” Nacho kivuli kikarudi nyuma hatua kumi.

9Kisha mfalme Hezekia alipopona, akatunga wimbo huu wa shukrani:

10“Nilisema: nikiwa mbichi kabisa,

inanibidi niage dunia.

Mimi nimepangiwa kwenda kuzimu

siku zote zilizonibakia.

11Nilisema sitamwona tena Mwenyezi-Mungu,

katika nchi ya walio hai;

wala sitamwona mtu yeyote tena,

miongoni mwa wakazi wa ulimwengu.

12Makao yangu yameng'olewa kwangu,

kama hema la mchungaji;

kama, mfumanguo nimefungasha maisha yangu;

Mungu amenikatilia mbali;

kabla hata mwisho wa siku amenikomesha.

13Usiku kucha nililia kuomba msaada;

kama simba, anavunjavunja mifupa yangu;

mchana na usiku ananikomesha.

14“Ninalia kama mbayuwayu,

nasononeka kama njiwa.

Macho yangu yamefifia kwa kuangalia juu.

Ee Bwana, nateseka;

uwe wewe usalama wangu!

15Lakini niseme nini:

yeye mwenyewe aliniambia,

naye mwenyewe ametenda hayo.

Usingizi wangu wote umenitoroka

kwa sababu ya uchungu moyoni mwangu.

16“Ee Bwana, Sisi twaishi kutokana na yote uliyotenda,

kwa hayo yote mimi binafsi pia ninaishi.

Nirudishie afya, uniwezeshe kuishi.

17Nilipata mateso makali kwa faida yangu;

lakini umeyaokoa maisha yangu

kutoka shimo la uharibifu,

maana umezitupa dhambi zangu nyuma yako.

18Huko kuzimu mtu hawezi kukushukuru wewe;

waliokufa hawawezi kukushukuru wewe.

Wala washukao huko shimoni

hawawezi tena kutumainia uaminifu wako.

19Walio hai ndio wanaokushukuru,

kama na mimi ninavyofanya leo.

Kina baba huwajulisha watoto wao uaminifu wako.

20“Mwenyezi-Mungu ataniokoa.

Nasi tutamsifu kwa nyimbo za vinubi

siku zote za maisha yetu,

nyumbani kwake Mwenyezi-Mungu.”

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania