Isaya 52

Isaya 52

Mungu ataikomboa Yerusalemu

1Amka! Amka!

Jipe nguvu zako ewe mji wa Siyoni!

Jivike mavazi yako mazuri,

ewe Yerusalemu, mji mtakatifu.

Maana hawataingia tena kwako

watu wasiotahiriwa na walio najisi.

2Jikung'ute mavumbi, uinuke

ewe Yerusalemu uliyetekwa nyara!

Jifungue minyororo yako shingoni,

ewe binti Siyoni uliyechukuliwa mateka.

3Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Nyinyi mliuzwa utumwani bila malipo yoyote, na mtakombolewa bila kulipa hata senti moja.[#52:3 Mwenyezi-Mungu hakuwauza Waisraeli utumwani na atawakomboa bila kumlipa mtu yeyote kitu chochote.]

4Tena mwanzoni nyinyi watu wangu mlikimbilia Misri mkakaa huko. Halafu baadaye Waashuru waliwakandamiza bila sababu yoyote.

5Katika hali ya sasa napata faida gani kuwaona watu wangu wamepelekwa utumwani? Hao wanaowatawala wanajitapa. Nalo jina langu laendelea kudharauliwa kila siku.[#52:5 Rejea Zab 137; Rom 2:24.]

6Kwa hiyo watu wangu watajua mimi ni nani; siku hiyo watajua kwamba ni mimi ninayesema: Niko!”

7Tazama inavyopendeza

kumwona mjumbe akitokea mlimani,

ambaye anatangaza amani,

ambaye analeta habari njema,

na kutangaza ukombozi!

Anauambia mji wa Siyoni:

“Mungu wako anatawala!”

8Sikiliza sauti ya walinzi wako;

wanaimba pamoja kwa furaha,

maana wanaona kwa macho yao wenyewe,

kurudi kwa Mwenyezi-Mungu mjini Siyoni.

9Pazeni sauti za shangwe, enyi magofu ya Yerusalemu!

Mwenyezi-Mungu amewafariji watu wake,

ameukomboa mji wa Yerusalemu.

10Mwenyezi-Mungu ameonesha nguvu yake tukufu,

mbele ya mataifa yote.

Atawaokoa watu wake,

na ulimwengu wote utashuhudia.

11Ondokeni! Ondokeni! Tokeni hapa;

msiguse kitu chochote najisi!

Ondokeni huku Babuloni!

Jitakaseni enyi mbebao vyombo vya Mwenyezi-Mungu.

12Safari hii hamtatoka kwa haraka,[#52:12 Safari ya kwanza ambapo walitoka kwa haraka haraka ni Kut 12:11,33-34; Kumb 16:3. Kuondoka Babuloni hakutakuwa kuondoka kwa hivihivi ila kutakuwa kuondoka na kurudi Yerusalemu kwa ushindi. Rejea Isa 41:17.]

wala hamtaondoka mbiombio!

Maana Mwenyezi-Mungu atawatangulieni,

Mungu wa Israeli atawalinda kutoka nyuma.

Mtumishi wa Mwenyezi-Mungu

13Mungu asema hivi:

“Mtumishi wangu atafanikiwa;

atatukuzwa na kupewa cheo,

atapata heshima kuu.

14Wengi waliomwona walishtuka,

kwa vile sura yake ilikuwa imeharibiwa;

hakuwa tena na umbo la kibinadamu!

15Lakini sasa ameyashangaza mataifa mengi.

Wafalme wanaduwaa kwa sababu yake,

maana wataona mambo ambayo hawajapata kuambiwa,

na kufahamu mambo ambayo hawajapata kusikia.”

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania