Isaya 6

Isaya 6

Mungu amwita Isaya kuwa nabii

1Mnamo mwaka aliofariki mfalme Uzia, nilimwona Bwana ameketi katika kiti cha enzi kilicho juu na cha fahari. Pindo la vazi lake lilienea hekaluni mote,[#6:1 Yaani mwaka 740 K.K. (rejea 2Fal 15:7; 2Nya 26:23).; #6:1 Katika mahali patakatifu sana hekaluni kulikuwa na mahali pa kiti cha enzi cha Mungu asiyeonekana (Kut 25:21-22; Zab 99:1).]

2na juu yake walikuwa wamekaa malaika. Kila mmoja alikuwa na mabawa sita: mawili ya kufunika uso, mawili ya kufunika mwili na mawili ya kurukia.[#6:2 Au, “maserafi”, neno la Kiebrania lenye maana ya “enye kumetameta” au “wenye kuwakawaka” na linatumiwa tu hapa katika Biblia kuwataja viumbe hao wa mbinguni. Maneno “Mabawa mawili … ya kufunika mwili”, Kiebrania neno kwa neno, “mabawa mawili ya kufunika miguu”, yamkini ni msemo wa kuonesha heshima na adabu mbele ya Mungu.]

3Waliitana kila mmoja na mwenzake hivi:

“Mtakatifu, mtakatifu, mtakatifu,

ni Mwenyezi-Mungu wa majeshi!

Dunia yote imejaa utukufu wake.”

4Sauti yao iliitikisa misingi ya milango ya hekalu, nalo likajaa moshi.

5Basi, mimi nikasema, “Ole wangu! Mimi nimeangamia, maana, midomo yangu ni najisi, na watu ninaoishi nao ni najisi kama mimi. Hata hivyo, kwa macho yangu mwenyewe, nimemwona Mfalme, Mwenyezi-Mungu wa majeshi.”

6Basi, mmoja wa hao malaika akaruka kunijia, akiwa ameshika mkononi koleo lililokuwa na kaa la moto alilolitwaa madhabahuni.

7Naye akinigusa nalo mdomoni, akasema: “Tazama, kaa hili limekugusa mdomo; umeondolewa hatia yako, umesamehewa dhambi yako.”

8Kisha nikamsikia Mwenyezi-Mungu akisema, “Nimtume nani? Ni nani atakayekuwa mjumbe wetu?” Nami nikajibu, “Niko hapa! Nitume mimi.”[#6:8 Matumizi ya wingi hapa “wetu” ni ngumu; lakini huenda Mungu anajumuisha hapa wakazi wake wa mbinguni (rejea 1Fal 22:19; taz pia Zab 82:1).]

9Naye akaniambia, “Nenda ukawaambie watu hawa:

‘Mtasikiliza sana, lakini hamtaelewa;

mtatazama sana, lakini hamtaona.’”

10Kisha akaniambia,

“Zipumbaze akili za watu hawa,

masikio yao yasisikie,

macho yao yasione;

ili wasije wakaona kwa macho yao,

wakasikia kwa masikio yao,

wakaelewa kwa akili zao,

na kunigeukia, nao wakaponywa.”

11Mimi nikauliza,

“Bwana, mpaka lini?”

Naye akanijibu,

“Mpaka hapo miji itakapobaki tupu bila wakazi,

nyumba bila watu,

na nchi itakapoharibiwa kabisa.

12Nami Mwenyezi-Mungu nitawapeleka watu mbali,

na kuifanya nchi yote kuwa mahame.

13Hata wakibaki watu asilimia kumi,

nao pia watateketezwa.

Hao watakuwa kama mvinje au mwaloni

ambao kisiki chake kimebaki baada ya kukatwa.”

(Kisiki hicho ni mbegu takatifu ya chanzo kipya.)

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania