The chat will start when you send the first message.
1Mwenyezi-Mungu aliniambia hivi: “Chukua ubao mkubwa, uandike juu yake maneno yanayosomeka kwa urahisi: ‘TEKA-HARAKA-POKONYA-UPESI.’”[#8:1 Tafsiri yamkini ya makala ngumu ya Kiebrania.; #8:1 Katika Kiebrania ni “Maher-shalal-hash-bazi” ambalo ni jina la mmoja wa watoto wa Isaya (8:3).]
2Basi, nikajipatia mashahidi wawili waaminifu ambao wangenishuhudia: Kuhani Uria na Zekaria, mwana wa Yeberekia.[#8:2 Uria alikuwa kuhani wakati wa mfalme Ahazi (2Fal 16:10-16) naye Zekaria huenda alikuwa baba mkwe wa Ahazi (2Fal 18:2).]
3Nililala na mke wangu ambaye pia ni nabii, akapata mimba, akajifungua mtoto wa kiume. Mwenyezi-Mungu akaniambia, “Mpe mtoto huyo jina ‘Teka-haraka-pokonya-upesi.’[#8:3 Mkewe Isaya naye pia ni nabii. Wafafanuzi wengi wa Maandiko wanahisi kwamba huyu ni sawa na yule anayeitwa “msichana” katika 7:14. Ikiwa ni huyohuyo, basi haikupita muda mrefu sana kati ya kuzaliwa kwa Imanueli (7:14) na huyo “Maher-shalal-hash-baz” na majina yao yanagusia mazingira yaleyale ya uvamizi wa mwaka 732 uliofanywa na Waashuru dhidi ya Israeli (yaani utawala wa kaskazini) na Siria.]
4Maana kabla mtoto huyu hajafikia umri wa kuweza kutamka: ‘Baba’ au ‘Mama,’ utajiri wa Damasko na nyara walizoteka huko Samaria zitapelekwa kwa mfalme wa Ashuru.”
5Mwenyezi-Mungu aliongea nami tena, akaniambia,
6“Kwa kuwa watu hawa wameyakataa maji ya Shiloa yatiririkayo polepole, wakafa moyo mbele ya mfalme Resini na mfalme Peka mwana wa Remalia,[#8:6 Mfereji uliotengenezwa kuleta maji mjini Yerusalemu kutoka chemchemi ya Gihoni.]
7basi, mimi Bwana nitawaletea mafuriko makuu ya maji ya mto Eufrate yaani mfalme wa Ashuru na nguvu zake zote; yatafurika na kupita kingo zake.
8Utaingia nchini Yuda kwa nguvu na kufurika na kupanda mpaka shingoni; utaenea juu ya nchi yako yote, ee Emanueli!”[#8:8 Taz 7:14.]
9Unganeni enyi watu wa mataifa nanyi mtafedheheshwa!
Sikilizeni enyi nchi za mbali duniani!
Jiwekeni tayari na kufedheheshwa;
naam, kaeni tayari na kufedheheshwa.
10Shaurianeni pamoja lakini itakuwa bure;
fanyeni mipango lakini haitafaulu,
maana Mungu yu pamoja nasi.
11Mwenyezi-Mungu alinionya kwa nguvu nisifuate njia za watu hawa, akaniambia,
12“Usijumuike nao katika njama zao, wala usiogope yale wanayoyaogopa wala kuwa na hofu.
13Nitambue mimi peke yangu, Mwenyezi-Mungu wa majeshi, kuwa mtakatifu; utaniogopa na kunicha mimi peke yangu.
14Mimi nitakuwa kimbilio, nitakuwa pia kama jiwe la kujikwaa, mwamba wa kuziangusha falme za Israeli na Yuda; nitakuwa mtego wa kuwatega na kuwanasa wakazi wa Yerusalemu.
15Watu wengi watajikwaa, wataanguka na kupondeka; watanaswa katika mtego huo na kuchukuliwa mateka.”
16Nitalihifadhi agizo hilo na kulifunga fundisho hilo miongoni mwa wafuasi wangu.[#8:16 Maaguzi ya nabii yaliandikwa katika vitabu mviringo na kutiwa mhuri. Wafuasi wake Isaya walihifadhi maaguzi hayo hadi wakati yalipotimia (taz pia Isa 29:11; Yer 32:8-15).]
17Nitamngojea Mwenyezi-Mungu ambaye amejificha mbali na wazawa wa Yakobo; nitamtumainia.
18Mimi pamoja na watoto alionipa Mwenyezi-Mungu ni ishara na alama katika Israeli kwa jina la Mwenyezi-Mungu wa majeshi akaaye mlimani Siyoni.[#8:18 Taz maelezo ya 7:3,14; 8:3.]
19Baadhi watawaambieni: “Nendeni mkatake shauri kwa mizimu na mizuka iliayo kama ndege; kwani ni kawaida watu kutaka shauri kwa miungu yao, na kutaka shauri kwa wafu kwa ajili ya walio hai.”[#8:19 Juu ya marufuku ya kushauriana na mizimu taz Kumb 18:10-14.]
20Hakika anayesema hivyo hajapata kuona mwanga. Lakini nyinyi shikilieni lile agizo na fundisho la Mungu.
21Watu watatangatanga nchini wamefadhaika sana na wenye njaa. Na wakiwa na njaa, hasira zitawawaka na kumlaani mfalme wao kadhalika na Mungu wao. Watatazama juu mbinguni[#8:21-22 Picha tunayopewa hapa ni ya kutisha na isiyo na matumaini kabisa. Kisehemu hiki kinafanana na Isa 5:30.]
22na kuiangalia dunia, lakini wataona tu taabu, giza na mauzauza ya shida. Hakuna atakayeliepa giza hilo kuu.