The chat will start when you send the first message.
1Lakini nchi ile iliyokuwa imekumbwa na huzuni haitabaki daima katika giza hilo kuu. Hapo awali Mungu alizifedhehesha nchi za Zebuluni na Naftali, lakini siku za usoni ataifanikisha sehemu hii ya baharini na nchi iliyo ng'ambo ya Yordani na hata Galilaya wanamoishi watu wa mataifa.[#9:1 Mfululizo wa aya hapa unahitilafiana na ule unaotumika katika Biblia ya Kiebrania. 9:1-21 zinawiana na 8:23—9:20 katika makala ya Kiebrania.; #9:1-6 Tofauti na aya za mwisho za sura iliyotangulia, hapa panafuata maelezo yenye kuleta matumaini ya mema (taz maelezo ya 4:2-6).; #9:1 Makabila ya Zebuluni na Naftali yalikuwa katika eneo la kaskazini-mashariki ya Galilaya. Makabila haya mawili ndiyo hasa yaliyoteseka zaidi wakati majeshi ya mfalme Tiglath-pileseri wa Ashuru yalipovamia Palestina mnamo mwaka 733 K.K. (2Fal 15:29).]
2Watu waliotembea gizani
wameona mwanga mkubwa.
Watu walioishi katika nchi ya giza kuu,
sasa mwanga umewaangazia.
3Wewe, ee Mungu, umelikuza taifa,
umeiongeza furaha yake.
Watu wanafurahi mbele yako,
wana furaha kama wakati wa mavuno,
kama wafurahivyo wanaogawana nyara.
4Maana nira nzito walizobeba,
nira walizokuwa wamefungwa,
na fimbo ya wanyapara wao,
umezivunjavunja kama wakati wa Wamidiani.
5Viatu vyote vya washambulizi vitani
na mavazi yote yenye madoa ya damu
yatateketezwa kama kuni za kuwasha moto.
6Maana mtoto amezaliwa kwa ajili yetu,
tumepewa mtoto wa kiume.
Naye atapewa mamlaka ya kutawala.
Ataitwa: “Mshauri wa Ajabu”.
“Mungu Mwenye Nguvu”,
“Baba wa Milele”,
“Mfalme wa Amani”.
7Utawala wake utastawi daima,
amani ya ufalme wake haitakoma.
Atachukua wadhifa wa mfalme Daudi
na kutawala juu ya ufalme wake;
ataustawisha na kuuimarisha,
kwa haki na uadilifu,
tangu sasa na hata milele.
Hayo atayafanya Mwenyezi-Mungu wa majeshi.
8Mwenyezi-Mungu ametoa tamko dhidi ya Yakobo
nalo litampata Israeli.
9Watu wote watatambua,
ukoo wote wa Efraimu
na wakazi wa Samaria.
Kwa kiburi na majivuno wanasema:
10“Kuta za matofali zimeanguka
lakini sisi tutazijenga kwa mawe yaliyochongwa!
Nyumba za boriti za mikuyu zimeharibiwa
lakini mahali pake tutajenga za mierezi.”
11Basi, Mwenyezi-Mungu atawaletea wapinzani
na kuwachochea maadui zao.
12Waaramu upande wa mashariki,[#9:12 Hili ni jina lingine la watu wa Siria ambao ni maadui wa jadi wa Waisraeli upande wa kaskazini mwa Palestina.]
Wafilisti upande wa magharibi,
wamepanua vinywa vyao kuimeza Israeli.
Hata hivyo, hasira yake haijatulia,
bado ameunyosha mkono wake.
13Ingawa aliwaadhibu watu,
hawakumrudia Mwenyezi-Mungu wa majeshi.
14Basi kwa muda wa siku moja tu,
Mwenyezi-Mungu atakata katika Israeli vichwa na mikia,
tawi la mtende na nyasi:
15Vichwa ndio wazee na waheshimiwa,
mikia ndio manabii wafundishao uongo.
16Wale wanaoongoza watu hawa wamewapotosha,
na hao wanaoongozwa nao wamepotoka.
17Kwa hiyo, Mwenyezi-Mungu hawahurumii vijana wao,[#9:17 Kadiri ya makala nyingine ya kale. Kiebrania: “hapendezwi”.]
hana huruma juu ya yatima na wajane wao;
kwani hakuna hata mmoja amchaye Mungu,
kila mtu husema uongo.
Hata hivyo, hasira yake haijatulia,
bado ameunyosha mkono wake.
18Uovu huwaka kama moto
uteketezao mbigili na miiba;
huwaka kama moto msituni,
na kutoa moshi mzito upandao angani juu.
19Kwa ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu wa majeshi
nchi imechomwa moto,
na watu ni kama kuni za kuuwasha.
Hakuna mtu anayemhurumia ndugu yake;
20wananyang'anya upande mmoja na hawatosheki;
wanakula upande mwingine lakini hawashibi.
Kila mmoja anamshambulia mwenzake.
21Manase dhidi ya Efraimu,[#9:21 Makabila mawili ya kaskazini ambayo yalitokana na watoto wawili wa Yosefu (Mwa 46:19-22; 48:5-6). Uhasama huo unaotajwa hapa waweza kuhusu wakati wa Waamuzi (Amu 12:1-6), au wakati wa wafalme Shalumu na Peka (2Fal 15:13-16,23-25).]
Efraimu dhidi ya Manase
na wote wawili dhidi ya Yuda.
Hata hivyo, hasira ya Mwenyezi-Mungu haijatulia,
bado ameunyosha mkono wake.