Waamuzi 12

Waamuzi 12

Mzozo kati ya Yeftha na kabila la Efraimu

1Watu wa kabila la Efraimu walikusanyika, wakavuka mto Yordani wakafika huko Zafoni. Kisha wakamwambia Yeftha, “Kwa nini hukutuita tuende pamoja nawe kupigana na Waamoni? Sasa tutaichoma nyumba yako nawe mwenyewe ndani yake.”[#12:1-5 Ushindi wa Yeftha ulizusha mzozo kwa kabila la Efraimu kwamba halikushirikishwa katika vita hivyo vya ushindi; labda kabila hilo lilitaka kupata sehemu yao katika vitu vilivyotekwa nyara. Watu wa Efraimu walisema pia kwamba watu wa Gileadi walikuwa wanaishi katika eneo ambalo lilikuwa mali ya Efraimu (12:4). Yeftha akakomesha tishio la watu wa Efraimu na kuweka ulinzi mashariki ya mto Yordani ili asitoke mtu yeyote kutoka eneo la Efraimu (mashariki ya mto Yordani) na kuingia Gileadi (magharibi ya mto Yordani) katika eneo ambalo lilikuwa la kabila la Gadi. Taz pia 8:1 maelezo.]

2Yeftha akawaambia, “Mimi pamoja na watu wangu tulikuwa na uadui mkubwa na Waamoni. Niliwaombeni mnisaidie lakini hamkuja kuniokoa.

3Nilipoona kwamba hamkuja kuniokoa, nilikwenda, roho mkononi, kupigana na Waamoni, naye Mwenyezi-Mungu akawatia mikononi mwangu. Kwa nini sasa mnakuja kupigana na mimi?”

4Basi, Yeftha akakusanya watu wote wa Gileadi, akapigana na watu wa Efraimu. Watu wa Gileadi wakawashinda watu wa Efraimu. Hawa Waefraimu ndio hao waliokuwa wamesema: “Nyinyi watu wa Gileadi ni wakimbizi wa kabila la Efraimu mliotoka katika kabila la Efraimu mkaenda kwa kabila la Manase.”

5Kisha watu wakavishika vivuko vya mto Yordani ili kuiziba njia ya watu wa Efraimu. Kila mara alipotokea mkimbizi akaomba kupita huko, watu wa Gileadi walimwuliza, “Je, wewe ni Mwefraimu?” Na kama alijibu, “La,”

6walimwambia: “Haya tamka neno ‘Shibolethi;’” lakini yeye hutamka “Sibolethi,” kwa sababu hakuweza kulitamka sawasawa. Hapo, walimkamata, wakamuua huko kwenye vivuko vya mto Yordani. Watu 42,000 wa Efraimu walipoteza maisha yao wakati huo.[#12:6 Ingawa tofauti za kutamka zilibainisha ni nani aliyekuwa Mgileadi na Mwefraimu, jambo muhimu hapa ni kwamba nyakati hizo kulikuwa na lahaja mbalimbali za lugha ya Kiebrania. Neno “Shibolethi” lina maana ya “suke la mahindi”.]

7Yeftha alikuwa mwamuzi katika Israeli kwa miaka sita. Kisha akafariki, akazikwa huko Gileadi katika mji wake.

Ibzani, Eloni, na Abdoni

8Baada ya Yeftha, Ibzani kutoka Bethlehemu akawa mwamuzi wa Israeli.[#12:8-10 Hapa inaanza orodha ya wale waitwao “waamuzi wadogo” na inaendelea pale orodha hiyo ilipokatizwa katika Amu 10:5; taz 10:1-5 maelezo.; #12:8 “Bethlehemu” hapa ni mji katika eneo la kabila la Zebuluni na ni tofauti na mji wa Bethlehemu katika Yuda.]

9Yeye alikuwa na watoto wa kiume thelathini na wa kike thelathini. Nao binti zake thelathini aliwaoza nje ya ukoo wake, na wana aliwaoza wasichana thelathini kutoka nje ya ukoo wake. Ibzani alikuwa mwamuzi wa Israeli kwa miaka saba.[#12:9 Kuwa na watoto wengi ilikuwa ishara ya utajiri na umaarufu wa mtu. Linganisha na Amu 10:3-5.]

10Akafariki, akazikwa mjini Bethlehemu.

11Baada ya Ibzani, Eloni wa kabila la Zebuluni, akawa mwamuzi wa Israeli kwa miaka kumi.

12Naye akafariki, akazikwa mjini Aiyaloni katika nchi ya kabila la Zebuluni.[#12:12 Huu ni tofauti na Aiyaloni ambao uko katika eneo la kabila la Efraimu au Manase (Amu 1:35).]

13Baada ya Eloni, Abdoni mwana wa Hileli kutoka Pirathoni akawa mwamuzi wa Israeli.[#12:13-15 Punda wakati huo walitumiwa kwa wingi kubeba mizigo. Kwamba kila mtoto wa Abdoni alikuwa na punda wake hiyo ilikuwa ishara ya kwamba familia yake ilikuwa tajiri. Yafaa kukumbuka kwamba farasi hawakutumiwa huko Palestina mpaka yapata mwaka 970 K.K. wakati wa mfalme Solomoni.]

14Yeye alikuwa na watoto wa kiume arubaini na wajukuu thelathini ambao walipanda punda sabini. Alikuwa mwamuzi wa Israeli kwa miaka minane.

15Kisha Abdoni akafariki, akazikwa mjini Pirathoni katika nchi ya kabila la Efraimu kwenye eneo la milima ya Waamaleki.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania