The chat will start when you send the first message.
1Kuhani Pashuri mwana wa Imeri, ambaye alikuwa ofisa mkuu wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu, alimsikia Yeremia akitoa unabii huo.[#20:1 Taz Yer 21:1-2 maelezo. Huenda alikuwa na wadhifa wa ulinzi wa hekalu. Baada ya kumsikiliza na vitendo vyake vya ishara au mifano dhidi ya Yerusalemu (sura 19) Pashuri aliamuru Yeremia apigwe na kufungwa minyororo.]
2Basi, Pashuri akampiga nabii Yeremia na kumtia kifungoni upande wa lango la juu la Benyamini, katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu.[#20:2 Lango hili si sawa na lile linalojulikana kama “Lango la Benyamini” linalotajwa katika Yer 37:13; 38:7 ambalo lilikuwa mojawapo ya malango ya kuingia mjini Yerusalemu. Labda lilikuwa lango la Kaskazini mwa mji kuelekea eneo la kabila la Benyamini na ambalo lilijengwa na mfalme Yothamu wa Yuda (rejea 2Fal 15:35; Eze 9:2).]
3Kesho yake asubuhi, Pashuri alipomtoa Yeremia katika mkatale huo, Yeremia alimwambia hivi: “Mwenyezi-Mungu hakuiti tena Pashuri, bali ‘Kitisho Pande Zote’.[#20:3 Kiebrania “Magor-misabib” yaweza kuwa jina lenye maana hiyo. Yeremia anampa Pashuri jina lipya, jina la maafa si la mema; Pashuri na jamaa yake watapelekwa uhamishoni wa kudumu ambapo wote watakufa.]
4Maana, Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Tazama, nitakufanya uwe kitisho kwako wewe mwenyewe na kwa rafiki zako wote. Wao watauawa vitani kwa upanga wa maadui zao huku ukiangalia. Nitawatia watu wote wa Yuda mikononi mwa mfalme wa Babuloni, naye atawachukua mateka hadi Babuloni na kuwaua kwa upanga.
5Zaidi ya hayo, utajiri wote wa mji, mapato yake yote, vitu vyake vyote vya thamani pamoja na hazina zote za wafalme wa Yuda, nitazitia mikononi mwa maadui zao ambao watazipora na kuchukua kila kitu hadi Babuloni.
6Na kwa upande wako wewe Pashuri, pamoja na nyumba yako yote, mtapelekwa utumwani; hakika mtakwenda Babuloni. Huko ndiko utakakofia na kuzikwa, kadhalika na rafiki zako wote ambao uliwatabiria uongo.’”
7Ee Mwenyezi-Mungu, wewe umenidanganya,[#20:7 Neno la Kiebrania linalotafsiriwa hapa kwa “kudanganya” linatumika katika mazingira mengine ya maandishi juu ya kubaka msichana (Kut 22:16); au kwa mwanamke anayetumia ujanja wake kumshawishi mwanamume (Amu 16:5); rejea pia Eze 14:9.]
nami kweli nikadanganyika;
wewe una nguvu kuliko mimi,
nawe umeshinda.
Kutwa nzima nimekuwa mtu wa kuchekwa,
kila mtu ananidhihaki.
8Kila ninaposema kitu, nalalamika,
napaza sauti, “Ukatili na uharibifu!”
Maana kwangu kutangaza neno la Mwenyezi-Mungu
kwanifanya nishutumiwe na kudhihakiwa kutwa nzima.
9Lakini nikisema, “Sitamtaja Mwenyezi-Mungu,
wala sitasema tena kwa jina lake,”
moyoni mwangu huwa na kitu kama moto uwakao,
uliofungiwa ndani ya mifupa yangu.
Najaribu sana kuuzuia humo,
lakini ninashindwa.
10Nasikia wengi wakinong'ona juu yangu.
Wananipanga jina: “Kitisho kila upande!”
Wengine wanasema:
“Nendeni mkamshtaki! Na tumshtaki!”
Hata rafiki zangu wote wapenzi wanangojea tu nianguke!
Wanasema “Labda atadanganyika, nasi tutalipiza kisasi.”
11Lakini wewe Mwenyezi-Mungu u pamoja nami
kwangu wewe ni kama shujaa wa kutisha;
kwa hiyo watesi wangu watajikwaa,
na hawataweza kunishinda.
Wataaibika kupindukia,
maana hawatafaulu.
Fedheha yao itakuwa ya daima;
kamwe haitasahaulika.
12Ee Mwenyezi-Mungu wa majeshi,
wewe humthibiti mtu mwadilifu,
huona yaliyo moyoni na akilini mwa watu,
unijalie kuona ukiwalipiza kisasi,
maana kwako nimekiweka kisa changu.
13Mwimbieni Mwenyezi-Mungu;
msifuni Mwenyezi-Mungu,
kwani ameyaokoa maisha ya mhitaji,
kutoka mikononi mwa watu waovu.
14Na ilaaniwe siku niliyozaliwa!
Siku hiyo mama aliponizaa,
isitakiwe baraka!
15Na alaaniwe aliyempelekea baba ujumbe:
“Umepata mtoto wa kiume”,
akamfanya ajae furaha.
16Mtu huyo na awe kama miji
aliyoiangusha Mwenyezi-Mungu bila huruma.
Mtu huyo na asikie kilio asubuhi,
na mchana kelele za vita,
17kwani hakuniua tumboni mwa mama yangu;
mama yangu angekuwa kaburi langu,
tumbo lake lingebaki kubwa daima.
18Kwa nini nilitoka tumboni mwa mama yangu?[#20:7-18 Katika sehemu hii tunakuta tena majibizano kati ya Yeremia na Mungu. Kwa mara nyingine tena, nabii anaonesha uchungu wake juu ya mateso aliyoyapata, tena malalamiko yake ni mazito sana. Yeremia anaonesha dhahiri jinsi ilivyo vigumu kuwa nabii. Lalamiko la Yeremia lina pande mbili: kwa upande mmoja ana imani sana na Mungu (20:11,13) na kwa upande mwingine anajihisi kwamba yuko katika hali ya kutojiweza kabisa; kutokuishi ni afadhali kuliko kuishi (15:10). Taz pia Yobu 3:1-19; Zab 22:1-22.]
Je, nilitoka ili nipate taabu na huzuni
na kuishi maisha ya aibu?