Yobu 1

Yobu 1

Shetani amjaribu Yobu

1Palikuwa na mtu mmoja nchini Usi, aitwaye Yobu. Mtu huyo alikuwa mwema na mnyofu; mtu mcha Mungu na mwenye kuepukana na uovu.[#1:1—2:13 Kisehemu hiki ni utangulizi wa kitabu chote cha Yobu. Kisehemu chenyewe kimeandikwa kwa mtungo wa kawaida (siyo shairi). Kinatupatia habari ya kukutana kwa Shetani na Mungu kwa mara ya kwanza, kukutana ambako ni mazingira muafaka ya Shetani kutoa hoja juu ya wema wake Yobu.; #1:1 Kadiri ya Omb 4:21 “Usi” ni eneo huko Edomu na hivyo ni nje ya eneo la Waisraeli. Katika Mwa 22:21 jina “Usi” linatumika kumtaja mwana wa Nahori, nduguye Abrahamu.; #1:1 Rejea Eze 14:14; Yak 5:11. Kwa vile msimulizi au mwandishi wa kisa hiki cha Yobu hakukihusisha na matukio ya kihistoria, kisa hicho kinaafiki ulimwengu wote; Yobu ni mkasa wa binadamu wote.; #1:1 Hizi ni sifa za mtu mwadilifu. Anatajwa katika Eze 14:14,20 kama mtu mwenye hali ya juu sana ya uadilifu. Kwamba huyu hakuwa Mwisraeli yamkini inaonekana kwamba hata nje ya watu wa Mungu uchaji wa Mungu ulikuwako, tena wa hali ya juu.]

2Yobu alikuwa na watoto saba wa kiume na watatu wa kike;[#1:2 Tarakimu “saba” mara nyingi katika Biblia hutumika kiishara, kuonesha ukamilifu wa jammbo au kitu. Taz Mwa 4:23-24 na Zab 79:12.]

3alikuwa na kondoo 7,000, ngamia 3,000, jozi 500 za ng'ombe na punda majike 500; na watumishi wengi sana; yeye alikuwa mashuhuri kuliko watu wote huko mashariki.

4Mara kwa mara, wanawe Yobu walifanya karamu nyumbani kwa kila mmoja wao kwa zamu; waliwaalika dada zao kula na kunywa pamoja nao.

5Kila baada ya karamu, Yobu aliwaita wanawe ili awatakase. Aliamka asubuhi na mapema baada ya karamu, akatoa tambiko za kuteketezwa kwa ajili ya kila mmoja wao kwani aliwaza, “Huenda wanangu wametenda dhambi na kumtukana Mungu mioyoni mwao.”[#1:5 Yobu kama mkuu wa hiyo jamaa aliona anawajibika mbele ya Mungu kwa mienendo ya jamaa yake.; #1:5 Neno linalotumika katika Kiebrania ni “kumbariki Mungu” nalo latumika badala ya neno halisi la “kumkufuru” Mungu au “kumtukana” kulingana na matumizi ya maandishi ya kuepa kutaja neno hilo kwa Mungu. Namna hiyohiyo ya kusema inatumika pia katika Yobu 1:11; 2:5,9.]

6Basi, ikatokia siku moja malaika wa Mungu walikwenda kukutana mbele ya Mwenyezi-Mungu, naye Shetani, akajitokeza pia pamoja nao.[#1:6 Au, neno kwa neno: “wana wa Mungu”. Hiyo ni mojawapo ya namna za kuwataja wale ambao ni kama washiriki katika baraza la kimungu na ambao kwa wingi hutajwa pengine kama malaika, au jeshi la Mungu, viumbe vya Mungu, watakatifu wa Mungu na hata miungu. Rejea 1Fal 22:19; Job 38:7; Zab 29:1; 82:1; 89:7. (Rejea pia 1Fal 22:19; Yobu 38:7; Zab 29:1; 82:1; 89:7).; #1:6 Ingawa sifa mbaya za Shetani kama ajulikanavyo katika A.J. hazijitokezi hapa moja kwa moja, kutokea kwake kwa ghafla na si kama mmojawapo wa wale viumbe vya mbinguni ambao hukutana na Mungu, kunamwonesha kama kiumbe mdadisi na mchongezi au mshtaki; sifa ambazo zimo pia katika Biblia. Katika 1:9 tuna swali ambalo linajieleza lenyewe: “…anamcha Mwenyezi-Mungu bure?” Shetani hasemi kwamba Yobu si mtu mnyofu na mwema, ila anatoa hapa kigezo cha kumcha Mungu bila matazamio ya kupata faida au tuzo (taz aya 10-11).]

7Mwenyezi-Mungu akamwuliza Shetani, “Umetoka wapi wewe?” Naye Shetani akamjibu Mwenyezi-Mungu, “Nimetoka kutembeatembea na kuzungukazunguka duniani.”

8Mwenyezi-Mungu akamwambia Shetani, “Bila shaka umemtambua mtumishi wangu Yobu. Duniani kote hamna mwingine aliye kama yeye. Yeye ni mtu mnyofu, mcha Mungu na mwenye kujiepusha na uovu.”

9Shetani akamjibu Mwenyezi-Mungu, “Je, Yobu anamcha Mwenyezi-Mungu bure?

10Je, si dhahiri kwamba wewe unamlinda pande zote pamoja na jamaa yake na kila kitu alicho nacho? Wewe umembariki na mali yake imeongezeka katika nchi.

11Lakini sasa, hebu nyosha tu mkono wako uiguse mali yake kama hutaona akikutukana waziwazi!”

12Mwenyezi-Mungu akamwambia Shetani, “Haya, waweza kufanya chochote uwezacho juu ya mali yake; ila tu yeye mwenyewe usimguse.” Basi, Shetani akaondoka mbele ya Mwenyezi-Mungu.

Jaribio la kwanza la Yobu

13Ikawa siku moja, watoto wa kiume na wa kike wa Yobu walikuwa wanakula na kunywa pamoja nyumbani kwa kaka yao mkubwa.

14Basi, mtumishi akafika kwa Yobu, akamwambia, “Tulikuwa tunalima kwa majembe ya kukokotwa na ng'ombe. Punda nao walikuwa wanakula hapo karibu.

15Basi Wasabea wakatuvamia na kuwachukua wanyama na kuwaua watumishi kwa upanga. Mimi peke yangu nimenusurika ili kuja kukuarifu.”[#1:15 Kabila katili la Bedui katika nchi ya Arabia.]

16Kabla hajamaliza kusema, mwingine akawasili, akasema, “Umeme wa radi umewachoma na kuwateketeza kondoo na watumishi, mimi tu peke yangu nimenusurika ili kuja kukuarifu.”

17Huyo naye kabla hajamaliza kusema, mwingine akawasili, akasema, “Wakaldayo walijipanga makundi matatu wakashambulia ngamia, wakawachukua, na kuwaua watumishi wako kwa upanga! Mimi peke yangu nimenusurika ili kuja kukuarifu.”[#1:17 Watu walioishi kusini mwa Mesopotamia, eneo ambalo linatajwa pia kama nchi ya awali ya Abrahamu. Taz Mwa 11:28-31. Kutajwa kwa hao watu wa makabila hayo mawili, (Wasabea aya 15 na Wakaldayo aya 17), labda kunafanywa ili kuonesha kwamba Yobu amekabiliwa na maafa kutoka kila upande.]

18Kabla hajamaliza kusema, akaja mwingine, akasema, “Watoto wako wa kiume na wa kike walikuwa wanakula na kunywa divai nyumbani kwa kaka yao mkubwa.

19Mara kimbunga kikavuma kutoka jangwani, kikaipiga nyumba hiyo kila upande nayo ikawaangukia, na vijana wote wamekufa, mimi peke yangu nimenusurika ili kuja kukuarifu.”

20Kisha Yobu akasimama, akararua mavazi yake, akanyoa nywele zake, akajitupa chini na kumwabudu Mungu.[#1:20 Ishara ya huzuni. Rejea Mwa 37:34; 2Sam 1:11; Yer 7:29.]

21Akasema,

“Uchi nilikuja duniani,

uchi nitaondoka duniani;

Mwenyezi-Mungu amenipa,

Mwenyezi-Mungu amechukua;

litukuzwe jina lake Mwenyezi-Mungu.”

22Katika mambo haya yote Yobu hakutenda dhambi wala hakumfikiria Mungu kuwa ana kosa.[#1:22 Katika Kut 22:28 imekatazwa kumlaani Mungu, yaani kumfikiria ana kosa. Adhabu ya kumlaani Mungu ilikuwa kifo (Law 24:15-16; taz pia Yobu 2:9).]

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania