The chat will start when you send the first message.
1Ndipo Yobu akajibu:[#12:1—14:22 Sehemu hii ya hoja za Yobu inamalizia duru ya kwanza ya mazungumzo ambayo ilifunguliwa na Yobu katika sura ya 3, ikafuatiwa na hoja ya Elifazi (sura 4—5), kisha Bildadi (sura 8) na Sofari (sura 11). Hapa, basi, Yobu ataongea tena (sura 12—14) kabla rafiki zake kufuata tena na hoja zao katika duru ya pili. 12:2-6 Katika aya hizi Yobu anatamka kwamba rafiki zake hawampiti kwa jambo la ujuzi na hekima (taz pia 13:2).]
2“Sawa! Nyinyi ni watu wa hekima.
Hekima itakufa wakati ule mtakapokufa.
3Mimi nami ni mwelewa kama nyinyi.
Mimi si mtu duni kuliko nyinyi.
Yote mliyosema kila mtu anajua.
4Nimekuwa kichekesho kwa rafiki zangu:
mimi niliyemwomba Mungu na akanijibu;
mimi niliye mwadilifu na bila lawama,
nimekuwa kichekesho kwa watu.
5Mtu anayestarehe hudharau msiba;
kwake, msiba huwajia wale wanaoteleza.
6Makao ya wanyang'anyi yana amani;
wenye kumchokoza Mungu wako salama,
nguvu yao ni mungu wao.
7Lakini waulize wanyama nao watakufunza;
waulize ndege nao watakuambia.
8Au iulize mimea nayo itakufundisha;
sema na samaki nao watakuarifu.
9Nani kati ya viumbe hivyo,
asiyejua kwamba Mwenyezi-Mungu ametenda hayo?
10Uhai wa kila kiumbe hai umo mikononi mwake;
kadhalika na pumzi ya uhai wa binadamu.
11Je, sikio haliyapimi maneno
kama ulimi uonjavyo chakula?
12Hekima iko kwa watu wazee,
maarifa kwao walioishi muda mrefu.
13Lakini hekima na uwezo ni vyake Mungu,
yeye ana maarifa na ujuzi.
14Akibomoa, hakuna awezaye kujenga upya;
akimfunga mtu, hakuna awezaye kumfungua.
15Akizuia mvua, twapata ukame;
akiifungulia, nchi hupata mafuriko.
16Yeye ana nguvu na hekima;
wanaodanganywa na wanaodanganya ni wake.
17Huwaacha washauri waende zao uchi,[#12:17 Tafsiri yamkini ya makala ngumu ya Kiebrania. Kuanzia hapa na kuendelea hadi 12:25 Yobu anasema juu ya kitendo cha Mungu cha kupindua bahati na fanaka za watu ambao waliheshimika na wenye nguvu katika jumuiya kama vile Yobu mwenyewe.]
huwafanya waamuzi kuwa wapumbavu.
18Huwavua wafalme vilemba vyao;
na kuwafunga viunoni kamba za wafungwa;
19Huwaacha makuhani waende uchi;
na kuwaangusha wenye nguvu.
20Huwanyang'anya washauri kipawa chao cha kuongea,
huwapokonya wazee hekima yao.
21Huwamwagia wakuu aibu,
huwaondolea wenye uwezo nguvu zao.
22Huvifunua vilindi vya giza,
na kuleta mwangani yaliyokuwa gizani.
23Huyakuza mataifa kisha huyaangamiza,
huyafanya yapanuke kisha huyatawanya.
24Huwaondolea viongozi wa watu ujuzi wao,
huwafanya watangetange nyikani kusiko na njia,
25wakapapasapapasa gizani kusiko na mwanga;
na kuwafanya wapepesuke kama walevi.