The chat will start when you send the first message.
1Ikatokea tena siku nyingine, malaika wa Mungu walikwenda kukutana mbele ya Mwenyezi-Mungu, naye Shetani akajitokeza pia pamoja nao.
2Mwenyezi-Mungu akamwuliza Shetani, “Umetoka wapi wewe?” Naye Shetani akamjibu Mwenyezi-Mungu, “Nimetoka kutembeatembea na kuzungukazunguka duniani.”
3Mwenyezi-Mungu akamwambia Shetani, “Je, umemwangalia mtumishi wangu Yobu? Duniani hakuna mwingine aliye kama yeye. Yeye ni mtu mnyofu, mcha Mungu na mwenye kujiepusha na uovu. Yeye yuko imara katika unyofu wake, ingawa wewe umenichochea nimwangamize bure.”
4Shetani akamjibu Mwenyezi-Mungu, “Ngozi kwa ngozi! Mtu hutoa kila kitu alicho nacho ili aokoe uhai wake.[#2:4 Tafsiri yamkini ya makala ngumu ya Kiebrania. Msemo huu labda ni methali na maana yake inadhihirika katika sentensi inayofuata, yaani: mtu atatoa chochote kusalimisha maisha yake.; #2:4-5 Shetani anasisitiza bado kwamba unyofu wa Yobu si wa bure. Kwa hiyo anatoa jaribio lingine (rejea Yobu 1:9-11).]
5Lakini sasa hebu nyosha mkono wako umguse mwili wake; nakuambia atakutukana waziwazi.”
6Basi, Mwenyezi-Mungu akamwambia Shetani, “Haya! Waweza kumfanya utakavyo, walakini usimuue.”
7Hapo Shetani akaondoka mbele ya Mwenyezi-Mungu, akamtesa Yobu kwa madonda mabaya tangu wayo wa mguu wake mpaka utosini mwake.[#2:7 Tukio hili ni la pili na la mwisho la kukutana huko mbinguni. Yote yatakayofuata sasa, pamoja na kujionesha kwa Mungu mara ya mwisho, yanafanyika duniani (34-41).]
8Yobu akatwaa kigae, akajikuna nacho na kuketi kwenye majivu.
9Mkewe akamwambia, “Bado tu ungali ukishikilia unyofu wako? Mtukane Mungu, ufe.”[#2:9 Kulingana na imani za watu wakati huo ilifikiriwa kufanya hivyo kungesababisha kifo cha mhusika mara moja.]
10Yobu akamjibu mkewe, “Wewe unaongea kama wanawake wapumbavu. Tukipokea mema kutoka kwa Mungu, kwa nini tukatae kupokea pia mabaya kutoka kwake?” Katika mambo hayo yote, Yobu hakutamka neno lolote la kumkosea Mungu.
11Marafiki watatu wa Yobu: Elifazi kutoka Temani, Bildadi kutoka Shua na Sofari kutoka Naamathi, walisikia juu ya maafa yote yaliyompata Yobu. Basi, wakaamua kwa pamoja waende kumpa pole na kumfariji.[#2:11 Hawa watatu, rafikize Yobu, yamkini ni watu watatu mashuhuri wa huko Mashariki. Mahali au maeneo walimotoka ni moja tu yaani “Temani” linalotajwa katika Biblia (Yer 49:7; Eze 25:13; Amo 1:12; Oba 9; Hab 3:3).]
12Walipomwona kwa mbali hawakumtambua. Basi, wakaanza kupaza sauti na kulia; waliyararua mavazi yao, wakarusha mavumbi angani na juu ya vichwa vyao.[#2:12 Dokezo kuhusu jinsi ugonjwa wake ulivyoharibu sura yake.]
13Kisha wakaketi udongoni pamoja na Yobu kwa siku saba, mchana na usiku, bila kumwambia neno lolote kwani waliyaona mateso yake kuwa makubwa mno.