Yobu 40

Yobu 40

1Mwenyezi-Mungu akaendelea kumwambia Yobu:[#40—41 Tafsiri hii inafuata mfululizo wa aya katika Biblia ya Kiebrania, yaani sura ya 40 ina aya 32 na sura ya 41 ina aya 26. Katika baadhi ya tafsiri sura ya 40 ina aya 24. Ndiyo kusema tafsiri hizo zinaanza sura ya 41:1 pale ambapo Biblia ya Kiebrania (na tafsiri hii) ina sura ya 40:25.]

2“Je, wewe mwenye kuchunguza makosa utashindana na Mungu Mwenye Nguvu?

Wewe unayebishana nami Mungu, basi jibu mambo hayo!”

3Kisha Yobu akamjibu Mwenyezi-Mungu:[#40:3-5 Jibu la kwanza la Yobu lina shabaha ya kuonesha udogo wake mbele yake Mungu.]

4“Mimi sifai kitu nitakujibu nini?

Naufunga mdomo wangu.

5Nilithubutu kusema na sitasema tena.

Nilisisitiza lakini sitaendelea kusema zaidi.”

6Hapo Mwenyezi-Mungu akamjibu kutoka kimbunga:

7“Jikaze kama mwanamume.

Nitakuuliza, nawe utanijibu.

8Je, unataka kweli kubatilisha hukumu yangu,

kuniona nina hatia ili wewe usiwe na hatia?

9Je, una nguvu kama mimi Mungu?

Waweza kunguruma kwa sauti kama yangu?

10“Basi, jioneshe kuwa na fahari na ukuu,

ujipambe kwa utukufu na fahari.

11Wamwagie watu hasira yako kuu;

mwangalie kila mwenye kiburi na kumwangusha.

12Mwangalie kila mwenye kiburi na kumporomosha,

uwakanyage waovu mahali walipo.

13Wazike wote pamoja ardhini;

mfunge kila mmoja kwa kifungo cha kifo.

14Hapo nitakutambua,

kwamba nguvu yako mwenyewe imekupa ushindi.

15“Liangalie lile dude Behemothi,[#40:15 Mnyama wa hadithi za kale ambaye anasimuliwa kwa sifa zinazofanana na za kiboko.]

nililoliumba kama nilivyokuumba wewe.

Hilo hula nyasi kama ng'ombe,

16lakini mwilini lina nguvu ajabu,

na misuli ya tumbo lake ni imara.

17Huufanya mkia wake mgumu kama mwerezi,

mishipa ya mapaja yake imeshonwa pamoja.

18Mifupa yake ni mabomba ya shaba,

viungo vyake ni kama pao za chuma.

19“Hilo ni la kwanza la ajabu kati ya viumbe vyangu!

Ni mimi Muumba wake niwezaye kulishinda.

20Milima wanamocheza wanyama wote wa porini

hutoa chakula chake.

21Hujilaza chini ya vichaka vya miiba,

na kujificha kati ya matete mabwawani.

22Hujisitiri katika vivuli vya vichaka vya miiba

na vya miti iotayo kando ya vijito.

23Mto ukifurika haliogopi,

halitishiki hata mto Yordani ukilifurikia kinywani.

24Nani awezaye kuliziba macho na kuliteka?

Nani awezaye kulitoboa pua kwa mtego?

25Je, waweza kuvua dude Lewiyathani kwa ndoana,[#40:25 Au, “mamba”. Taz Yobu 3:8.; #40:25 Baadhi ya tafsiri zinaanza sura 40:1 hapa.]

au kuufunga ulimi wake kwa kamba?

26Je, unaweza kulitia kamba puani mwake,

au kulitoboa taya kwa kulabu?

27Je, wadhani litakusihi uliachilie?

Je, litazungumza nawe kwa upole?

28Je, litafanya mapatano nawe,

ulichukue kuwa mtumishi wako milele?

29Je, utacheza nalo kama ndege,

au kulifunga kamba licheze na wajakazi wako?

30Wadhani wavuvi watashindania bei yake?

Je, wafanyabiashara watathubutu kulikata na kugawana?

31Je, waweza kuichoma ngozi yake kwa mikuki,

au kichwa chake kwa mfumo wa kuvua samaki?

32Jaribu tu kuligusa, uone cha mtema kuni;

Kamwe hutarudia tena kufanya hivyo!

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania