Yobu 5

Yobu 5

1“Ita sasa, uone kama kuna wa kukuitikia.

Ni yupi kati ya watakatifu utakayemwita?

2Ama kweli hangaiko humuua mpumbavu,

na wivu humwangamiza mjinga.

3Nimepata kuona mpumbavu akifana,

lakini ghafla nikayalaani makao yake.

4Watoto wake hawana usalama;

hudhulumiwa mahakamani,

na hakuna mtu wa kuwatetea.

5Mazao yake huliwa na wenye njaa,

hata nafaka iliyoota kati ya miiba;

wenye tamaa huuonea shauku utajiri wake.

6Kwa kawaida mateso hayatoki mavumbini

wala matatizo hayachipui udongoni.

7Bali binadamu huzaliwa apate taabu,[#5:7 Au, kwa tafsiri nyingine yamkini, “binadamu ndiye mwenye kusababisha taabu”.]

kama cheche za moto zirukavyo juu.

8“Kama ningekuwa wewe ningemgeukia Mungu,

ningemwekea yeye Mungu kisa changu,

9yeye atendaye makuu yasiyochunguzika,

atendaye maajabu yasiyohesabika.

10Huinyeshea nchi mvua,

hupeleka maji mashambani.

11Huwainua juu walio wanyonge,

wenye kuomboleza huwapa usalama.

12Huvunja mipango ya wenye hila,

matendo yao yasipate mafanikio.

13Huwanasa wenye hekima kwa werevu wao,[#5:12-13 Rejea 1Kor 3:19 ambapo msemo huu unakaririwa; taz pia 5:2-7.]

mipango ya wajanja huikomesha mara moja.

14Hao huona giza wakati wa mchana,

adhuhuri hupapasapapasa kama vile usiku.

15Lakini Mungu huwaokoa yatima wasiuawe,

huwanyakua fukara mikononi mwa wenye nguvu.

16Hivyo maskini wanalo tumaini,

nao udhalimu hukomeshwa.

17“Heri mtu yule ambaye Mungu anamrudi![#5:17 Kukubali kuonywa na Mungu ni fadhila ambayo inapendelewa sana na maandishi ya Methali. Rejea Meth 3:1-12; 13:1; 15:5,10,12,32; taz pia Zab 94:12 na Ebr 12:5-6.]

Hivyo usidharau Mungu Mwenye Nguvu anapokuadhibu.

18Kwani yeye huumiza na pia huuguza;[#5:18 Lugha inayomfananisha Mungu na daktari au muuguzi anayeponya majeraha; sawa kabisa na lugha ya Hos 6:1.]

hujeruhi, na kwa mkono wake huponya.

19Atakuokoa katika maafa zaidi ya mara moja;[#5:19 Kiebrania kina “atakuokoa katika sita … na katika saba”. Msemo huo ni wa kimfano yaani, atakuokoa tena na tena au daima, tarakimu saba ikiwa ni utimilifu wa jambo. Taz Mwa 4:23-24 maelezo.]

katika balaa la mwisho, uovu hautakugusa.

20Wakati wa njaa atakuokoa na kifo,

katika mapigano makali atakuokoa.

21Utakingwa salama na mashambulio ya ulimi,

wala hutaogopa maangamizi yajapo.

22Maangamizi na njaa vijapo, utacheka,

wala hutawaogopa wanyama wakali wa nchi.

23Nawe utaafikiana na mawe ya shambani,

na wanyama wakali watakuwa na amani nawe.

24Utaona nyumbani mwako mna usalama;

utakagua mifugo yako utaiona yote ipo.

25Utaona pia wazawa wako watakuwa wengi,

wengi kama nyasi mashambani.

26Utafariki ukiwa mkongwe mtimilifu,

kama mganda wa ngano ya kupurwa iliyoiva vizuri.

27Basi huu ndio utafiti wetu; tena ni ukweli;

uusikie na kuuelewa kwa faida yako.”

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania