The chat will start when you send the first message.
1Pigeni tarumbeta huko Siyoni;
pigeni baragumu juu ya mlima mtakatifu!
Tetemekeni enyi wakazi wa Yuda,
maana siku ya Mwenyezi-Mungu inakuja,
naam, siku hiyo iko karibu!
2Hiyo ni siku ya giza na huzuni;
siku ya mawingu na giza nene.
Jeshi kubwa la nzige linakaribia
kama giza linalotanda milimani.
Namna hiyo haijapata kuweko kamwe
wala haitaonekana tena
katika vizazi vyote vijavyo.
3Kama vile moto uteketezavyo
jeshi hilo laharibu kila kitu mbele yake
na kuacha nyuma kila kitu kinateketezwa;
kabla hawajapita, nchi ni kama bustani ya Edeni,
lakini wakisha pita, ni jangwa tupu.
Hakuna kiwezacho kuwaepa!
4Wanaonekana kama farasi,
wanashambulia kama farasi wa vita,
5Wanaporukaruka kwenye vilele vya milima,
wanarindima kama magari ya farasi,
wanavuma kama mabua makavu motoni.
Wamejipanga kama jeshi kubwa
tayari kabisa kufanya vita.
6Wakaribiapo, watu hujaa hofu,
nyuso zao zinawaiva.
7Wanashambulia kama mashujaa wa vita;
kuta wanazipanda kama wanajeshi.
Wote wanakwenda mbele moja kwa moja,
bila hata mmoja wao kubadilisha njia.
8Hakuna amsukumaye mwenziwe;
kila mmoja anafuata mkondo wake.
Wanapita kati ya vizuizi vya silaha,
wala hakuna kiwezacho kuwazuia.
9Wanauvamia mji,
wanapiga mbio ukutani;
wanaziparamia nyumba na kuingia,
wanapenya madirishani kama wezi.
10Nchi inatetemeka mbele yao,
mbingu zinatikisika.
Jua na mwezi vyatiwa giza,
nazo nyota zinaacha kuangaza.
11Mwenyezi-Mungu anaamuru jeshi lake kwa sauti;
askari wake ni wengi mno,
wanaomtii hawahesabiki.
Siku ya Mwenyezi-Mungu kweli ni kuu na ya kutisha sana!
Nani atakayeweza kuistahimili?
12“Lakini hata sasa,”
nasema mimi Mwenyezi-Mungu,
“Nirudieni kwa moyo wote,
kwa kufunga, kulia na kuomboleza.
13Msirarue mavazi yenu kuonesha huzuni
bali nirudieni kwa moyo wa toba.”
Mrudieni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu;
yeye amejaa neema na huruma;
hakasiriki upesi, ni mwingi wa fadhili;
daima yu tayari kuacha kuadhibu.
14Huenda Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atabadili nia[#2:14 Rejea Amo 5:15; Yona 3:9; Sef 2:3. Uamuzi wa kusamehe ni wa Mungu peke yake. Tendo la binadamu la kutubu haliwezi kuhimiza uamuzi wa kimungu, ila linampa binadamu tumaini la kupata huruma yake Mungu (rejea 2Sam 12:22; Omb 3:29).]
na kuwapeni baraka ya mazao,
mkamtolea sadaka za nafaka na kinywaji.
15Pigeni tarumbeta huko Siyoni!
Toeni amri watu wafunge;
itisheni mkutano wa kidini.
16Wakusanyeni watu wote,
wawekeni watu wakfu.
Waleteni wazee,
wakusanyeni watoto,
hata watoto wanyonyao.
Bwana arusi na bibi arusi
na watoke vyumbani mwao.
17Kati ya madhabahu na lango la hekalu,[#2:17 Hiyo madhabahu au mahali pa kutambikia ni ile ya shaba ambapo watu waliteketeza kafara walizomtolea Mungu (2Nya 4:1).]
makuhani, wahudumu wa Mwenyezi-Mungu,
walie na kuomba wakisema:
“Wahurumie watu wako, ee Mwenyezi-Mungu.
Usiyaache mataifa mengine yatudharau
na kutudhihaki yakisema,
‘Yuko wapi basi Mungu wao?’”
18Ndipo Mwenyezi-Mungu akaipenda nchi yake
akawahurumia watu wake.
19Alisikiliza, akajibu sala zao; akasema,
“Sasa nitawapeni tena nafaka,
sitawafanya mdharauliwe tena na mataifa.
20Nitawaondoa hao adui watokao kaskazini,[#2:20 Kwa wingi, maadui wa Waisraeli kama vile Waashuru na Wababuloni waliwavamia walitoka kaskazini (Yer 1:14-15; 4:6; 6:1; Eze 26:7; 38:6,15; 39:2). Eneo hilo liliwatisha Waisraeli na lilikuwa mfano wa nguvu za kutisha.]
nitawafukuza mpaka jangwani;
askari wa mbele nitawatupa katika Bahari ya Chumvi
na wale wa nyuma katika Bahari ya Mediteranea.
Watatoa uvundo na harufu mbaya,
hao ambao wamefanya maovu makubwa.
21“Usiogope, ewe nchi,
bali furahi na kushangilia,
maana Mwenyezi-Mungu ametenda makuu.
22Msiogope, enyi wanyama.
malisho ya nyikani yamekuwa mazuri,
miti inazaa matunda yake,
mizabibu na mitini zinazaa kwa wingi.
23“Furahini, enyi watu wa Siyoni,
shangilieni kwa sababu ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu,
maana amewapeni mvua za masika,
amewapeni mvua ya kutosha:
mvua za masika na mvua za vuli kama hapo awali.
24Mahali pa kupuria patajaa nafaka,
mashinikizo yatafurika divai na mafuta.
25Nitawarudishia miaka ile iliyoliwa na nzige,
kila kitu kilicholiwa na tunutu, parare na matumatu,
hilo jeshi kubwa nililowaletea!
26Mtapata chakula kingi na kutosheka;
mtalisifu jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu,
aliyewatendea mambo ya ajabu.
Watu wangu, kamwe hawatadharauliwa tena.
27Mtatambua kwamba mimi nimo miongoni mwenu,
enyi Waisraeli;
kwamba mimi Mwenyezi-Mungu,
ndimi Mungu wenu wala hakuna mwingine.
Watu wangu, kamwe hawatadharauliwa tena.
28“Kisha hapo baadaye
nitaimimina roho yangu juu ya binadamu wote.
Watoto wenu wa kike na wa kiume watatabiri,
wazee wenu wataota ndoto,
na vijana wenu wataona maono.
29Hata juu ya watumishi wa kiume na wa kike,
nitaimimina roho yangu wakati huo.
30“Nitatoa ishara mbinguni na duniani;
kutakuwa na damu, moto na minara ya moshi.
31Jua litatiwa giza,
na mwezi utakuwa mwekundu kama damu,
kabla ya kufika siku ya Mwenyezi-Mungu,
siku iliyo kuu na ya kutisha.
32Hapo watu wote watakaoomba kwa jina la Mwenyezi-Mungu wataokolewa.[#2:32 Rejea Mate 2:17-21 na maelezo yake.]
Maana katika mlima Siyoni na Yerusalemu,
watakuwako watu watakaosalimika,
kama nilivyosema mimi Mwenyezi-Mungu.