The chat will start when you send the first message.
1Mfalme Yabini wa mji wa Hazori alipopata habari hizo, alipeleka ujumbe kwa mfalme Yobabu wa Madoni, mfalme wa Shimroni na mfalme wa Akshafi,[#11:1 Mfalme huyu alikuwa adui maarufu wa Waisraeli (taz Amu 4:2,23). Na mji “Hazori” ulikuwa mji maarufu sana wa watu wa Kanaani (taz Yos 11:10) kaskazini ya ziwa Genesareti. Machimbo ya vitu vya kale huko yanaonesha kwamba mji huo ulikuwa umeharibiwa mwishoni mwa karne ya 13 K.K. na kwamba wakati wa Solomoni ulijengwa tena na kuwa mji mkubwa wenye malango na kuta za ulinzi (taz 1Fal 9:15).]
2na kwa wafalme waliokuwa katika milima ya kaskazini, waliokuwa Araba ambayo ilikuwa kusini mwa Kinerethi, kwenye tambarare na waliokuwa Nafath-dori katika upande wa magharibi.
3Pia, alipeleka ujumbe kwa Wakanaani waliokuwa pande za mashariki na magharibi, kwa Waamori, Wahiti, Waperizi, Wayebusi ambao walikaa milimani na kwa Wahivi ambao walikaa chini ya mlima Hermoni katika nchi ya Mizpa.[#11:3 Kuna mahali kadhaa panapotajwa kwa jina hilo: Mispa ya Yuda — Kiebrania ni Mispa (15:38); Mispa kule Moabu (18:25-28); Mispa ya Gileadi (Mwa 31:49) na Mispa ya Benyamini (1Sam 7:16-17).]
4Basi, wakatoka wote na majeshi yao makubwa. Nao walikuwa wengi kama mchanga wa pwani pamoja na magari mengi na farasi wengi sana.
5Wafalme hawa wote wakaungana na kupiga kambi yao katika chemchemi ya Meromu ili wapigane na Waisraeli.
6Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua, “Usiwaogope hao, maana kesho, wakati kama huu, nitawaangamiza wote kwa kuwatia mikononi mwa Waisraeli; nanyi mtakata mishipa ya farasi wao na kuteketeza magari yao kwa moto.”
7Basi, ghafla kwenye chemchemi ya Meromu Yoshua pamoja na jeshi lake lote akawatokea na kuwashambulia.
8Mwenyezi-Mungu akawatia mikononi mwa Waisraeli, nao wakawachapa na kuwafukuza mpaka Sidoni Kuu na Misrefoth-maimu, hadi upande wa mashariki katika bonde la Mizpa. Waisraeli wakawapiga na kuwaua wote.[#11:8 Mji wa Sidoni ulikuwa mji wa kale na maarufu sana kama bandari ya Foinike, yapata kilomita 40 kutoka mji wa sasa wa Lebanoni uitwao sasa “Beirut” (taz Eze 27:8). Kulingana na Mwa 10:19, eneo la Kanaani lilienea kutoka Sidoni kaskazini mpaka Gaza kusini (taz aya 22). Na Misrefoth-maimu ulipakana na nchi ya Foinike (Yos 13:6).]
9Yoshua aliwakatakata mishipa farasi wao wote na kuyateketeza magari yao kwa moto, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwagiza.
10Yoshua alipokuwa anarudi, akauteka mji wa Hazori. Alimuua mfalme wake maana ndiye aliyekuwa kiongozi wa falme hizo zote.
11Kisha akauteketeza mji wa Hazori kwa moto na kuwaua wakazi wake wote, asimwache hata mtu mmoja.
12Pia aliiteketeza miji ile mingine yote kwa moto na kuwaua wafalme wao wote kama Mose, mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, alivyomwamuru.
13Lakini Waisraeli hawakuiteketeza miji iliyokuwa vilimani, isipokuwa tu mji wa Hazori ambao Yoshua aliuteketeza.
14Waisraeli wakachukua vitu vyote walivyoteka nyara na wanyama wa miji hiyo; lakini waliwaua wakazi wake wote, wala hawakumwacha hata mtu mmoja.
15Amri hii alipewa Mose, mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, naye Mose akamwamuru Yoshua ambaye aliitekeleza. Yoshua alitimiza kila jambo Mwenyezi-Mungu alilomwamuru Mose.
16Yoshua aliiteka nchi nzima: sehemu za milimani na sehemu zote za Negebu, eneo lote la Gosheni, nchi tambarare, nchi ya Araba, milima ya Israeli na sehemu zake zilizo tambarare;
17aliwateka na kuwaua wafalme wote wa nchi hizo kuanzia mlima uliokuwa mtupu wa Halaki karibu na Seiri mpaka Baal-gadi katika bonde la Lebanoni, kusini ya mlima Hermoni.
18Vita alivyopigana Yoshua na wafalme hawa wote vilichukua muda mrefu.
19Hakuna mji ambao ulifanya mapatano ya amani na Waisraeli, isipokuwa Gibeoni tu, ambamo waliishi Wahivi. Waisraeli waliiteka miji mingine yote kwa kupigana vita.
20Ilikuwa ni matakwa ya Mwenyezi-Mungu mwenyewe kuishupaza mioyo ya watu wa mataifa hayo ili wapigane. Alikusudia wasihurumiwe ila wateketezwe. Ndivyo Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose.[#11:20 Kama vile wakati wa Waisraeli kule Misri (Kut 4:1), Mungu alipomfanya Farao kuwa mkaidi, na hapa pia anaishupaza mioyo ya mataifa.]
21Wakati huo, Yoshua alikwenda, akawaangamiza Waanaki waliokuwa wanaishi katika milima huko Hebroni, Debiri, Anabu, nchi yote ya milima ya Yuda na Israeli. Yoshua aliwaangamiza watu hao pamoja na miji yao.[#11:21 Hawa walikuwa watu wa umbo kubwa na wenye nguvu (Hes 13:33 maelezo). Pengine wanasemekana kuwa wazawa wa majitu yanayotajwa katika Mwa 6:4 kama Wanefili.]
22Hakuna mtu wa kabila la Anaki ambaye alibakia katika nchi ya Israeli; walibaki wachache tu katika miji ya Gaza, Gathi na Ashdodi.[#11:22 Hiyo ilikuwa miji mikubwa ya Wafilisti kwenye mwambao wa Bahari ya Mediteranea. Miji hii pamoja na Askaloni na Ekroni inajulikana kama miji ya muungano wa Wafilisti. Lile jitu Goliathi (1Sam 17:4) lilitoka kule Gathi.]
23Basi, Yoshua akaitwaa nchi yote kulingana na yote yale Mwenyezi-Mungu aliyomwambia Mose. Yoshua akaikabidhi kwa Waisraeli iwe mali yao, wagawane kulingana na makabila yao. Kisha nchi nzima ikatulia, ikawa haina vita tena.