The chat will start when you send the first message.
1Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema, “Tazama, namtuma mjumbe wangu anitangulie kunitayarishia njia. Bwana mnayemtafuta atalijia hekalu lake ghafla. Mjumbe mnayemtazamia kwa hamu kubwa atakuja na kutangaza agano langu.”[#3:1 Mjumbe huyu ambaye anatayarisha njia ya Bwana (Isa 40:3) anatambuliwa kuwa ni Elia (taz 4:5) na Yohane Mbatizaji (Mat 11:3-14; Marko 1:2; Luka 1:76; 7:27).; #3:1 Tafsiri nyingine yamkini: “Mjumbe wa agano” ambapo hapa yamkini ni dokezo kiasi fulani kwa “Bwana” (Mwa 16:7-16; 18:1-2,17,22).]
2Lakini ni nani atakayestahimili siku hiyo atakapokuja? Ni nani atakayesimama kustahimili atakapotokea? Yeye ni kama moto mkali usafishao chuma; ni kama sabuni ya dobi.[#3:2 Rejea Isa 13:6; Eze 30:2-3; Yoe 1:15; 2:11; Amo 5:18-20; 8:9-14; Sef 1:14-18; Ufu 6:17.]
3Yeye atakuja kuhukumu kama mtu asafishaye na kutakasa fedha. Atawasafisha wazawa wa Lawi, kama mtu afuavyo dhahabu au fedha, mpaka wamtolee Mwenyezi-Mungu tambiko zinazokubalika.
4Hivyo, tambiko za watu wa Yuda na wa Yerusalemu zitampendeza Mwenyezi-Mungu kama za watu wa kale; kama katika miaka ya zamani.
5Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema: “Kisha nitawakaribia ili kuwahukumu. Sitasita kutoa ushahidi dhidi ya wachawi, wazinzi, watoa ushahidi wa uongo, wanaowapunja waajiriwa, wanaowadhulumu wageni na wale wasionicha mimi.
6“Mimi ni Mwenyezi-Mungu, mimi sibadiliki. Lakini nyinyi, nyinyi wazawa wa Yakobo hamjatoweka bado.[#3:6 Rejea Hes 23:19; Ebr 13:8; Yak 1:17.]
7Tangu wakati wa wazee wenu, mmezidharau kanuni zangu wala hamkuzifuata. Basi, mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu Mkuu nasema: nirudieni, nami nitawageukieni. Lakini nyinyi mnauliza, ‘Tutakurudia namna gani?’ Nami nawaulizeni,[#3:7 Rejea Isa 55:7; Zek 1:3; Yak 4:8. Taz pia Yer 3:1 maelezo.]
8Je, ni sawa mtu kumdanganya Mungu? La! Lakini nyinyi mnanidanganya! Walakini nyinyi mwauliza: ‘Tunakudanganya kwa namna gani?’ Naam! Mnanidanganya kuhusu zaka na tambiko zenu.
9Nyinyi na taifa lenu lote mmelaaniwa kwa sababu ya kunidanganya.
10Leteni ghalani mwangu zaka yote, ili nyumbani mwangu kuwe na chakula cha kutosha. Kisha mwaweza kunijaribu. Nijaribuni namna hiyo nanyi mtaona kama sitayafungua madirisha ya mbinguni na kuwatiririshia baraka tele.[#3:10 Kuhusu zaka na matoleo mengine rejea Lawi 27:30; Hes 18:21-24; Kumb 12:6; 14:22-29; Neh 13:12. Taz pia Zab 50:7-15; Isa 43:23.]
11Wadudu waharibifu nitawakemea wasiyaharibu tena mazao yenu. Mizabibu yenu mashambani haitaacha kuzaa matunda. Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nimesema.
12Ndipo mataifa yote yatawaita nyinyi watu waliobarikiwa, maana nchi yenu itakuwa nchi ya furaha. Mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu Mkuu nimesema.”
13Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Maneno yenu yamekuwa mzigo kwangu. Hata hivyo mnasema, ‘Tumesema nini dhidi yako?’
14Nyinyi mmesema, ‘Kumtumikia Mungu hakuna faida. Kuna faida gani kuyatii maagizo ya Mwenyezi-Mungu wa majeshi, au kujaribu kumwonesha kuwa tumekosa mbele yake kwa kutembea kama watu wanaoomboleza?
15Tuonavyo sisi, ni kwamba, wenye kiburi ndio wenye furaha daima. Watu waovu, licha ya kustawi, hata wanapomjaribu Mungu, hawapati adhabu.’”
16Ndipo watu wanaomcha Mwenyezi-Mungu walipozungumza wao kwa wao, naye Mwenyezi-Mungu akasikia mazungumzo yao. Mbele yake kikawekwa kitabu ambamo iliandikwa kumbukumbu ya wale wanaomcha na kumheshimu.[#3:16 Ili kulikabili tatizo au suala la mateso ya watu waadilifu na kufana kwa watu waovu, jibu ni kwamba Mungu anacho kitabu ambacho kimeandikwa wale wanaomheshimu. Rejea Kut 32:32; Zab 69:28; Dan 12:1; Ufu 3:5; 13:8; 17:8. Taz pia utangulizi wa kitabu cha Yobu.]
17Iliandikwa hivi: Mwenyezi-Mungu asema: “Hao watakuwa watu wangu. Watakuwa urithi wangu maalumu siku ile nitakapoinuka kufanya ninalokusudia. Sitawadhuru kama vile baba asivyomdhuru mwanawe anayemtumikia.
18Hapo ndipo mtakapotambua tena tofauti iliyopo kati ya waadilifu na waovu; naam, kati ya mtu anayemtumikia Mungu na asiyemtumikia.”