Marko 10

Marko 10

Kuhusu talaka

(Mat 19:1-12; Luka 16:18)

1Yesu alitoka hapo akaenda mkoani Yudea, hata ng'ambo ya mto Yordani. Umati wa watu ukamwendea tena, naye akawafundisha tena kama ilivyokuwa desturi yake.

2Basi, Mafarisayo wakamwendea, na kwa kumjaribu wakamwuliza, “Je, ni halali mume kumpa mkewe talaka?”

3Yesu akawajibu, “Mose aliwapa maagizo gani?”

4Nao wakasema, “Mose aliagiza mume kumpatia mkewe hati ya talaka na kumwacha.”

5Yesu akawaambia, “Mose aliwaandikia amri hiyo kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu.

6Lakini tangu kuumbwa ulimwengu, Mungu aliumba mwanamume na mwanamke.

7Hivyo mwanamume atawaacha baba yake na mama yake, ataungana na mke wake,

8nao wawili watakuwa mwili mmoja. Kwa hiyo, wao si wawili tena bali mwili mmoja.

9Basi, alichounganisha Mungu, binadamu asitenganishe.”

10Walipoingia tena ndani ya nyumba, wanafunzi wake walimwuliza juu ya jambo hilo.

11Naye akawaambia, “Anayemwacha mkewe na kuoa mwingine, anazini dhidi ya mkewe.[#10:11-12 Taz Mat 5:32; 19:9; Luka 16:18; 1Kor 7:10-11. Kwa jumla, mtazamo na msimamo wa Yesu kuhusu uzinzi ni tofauti sana na ule wa Wayahudi ambao walifikiri uzinzi unatendwa na mwanamke dhidi ya mwanamume na sio pia mwanamume dhidi ya mwanamke (Kumb 22:22).]

12Na mwanamke anayemwacha mumewe na kuolewa na mwingine anazini.”

Yesu anawabariki watoto wadogo

(Mat 19:13-15; Luka 18:15-17)

13Watu walimletea Yesu watoto wadogo ili awaguse, lakini wanafunzi wakawakemea.[#10:13 Yamaanisha awape baraka (10:16; taz pia Mwa 48:14-16).]

14Yesu alipoona hivyo, alikasirika akawaambia, “Waacheni hao watoto waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana ufalme wa Mungu ni kwa ajili ya watu walio kama watoto hawa.

15Nawaambieni kweli, mtu yeyote asiyeupokea ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hataingia humo.”[#10:15 Kuhusu kuwa kama mtoto mdogo taz Mat 18:3; na rejea Marko 9:37 juu ya kuwapokea watoto wa namna hiyo.]

16Kisha akawapokea watoto hao, akawawekea mikono, akawabariki.

Mtu aliyekuwa tajiri

(Mat 19:16-30; Luka 18:18-30)

17Yesu alipoanza tena safari yake, mtu mmoja alimjia mbio, akapiga magoti mbele yake, akamwuliza, “Mwalimu mwema, nifanyeje niupate uhai wa milele?”

18Yesu akamjibu, “Mbona unaniita mwema? Hakuna aliye mwema ila Mungu peke yake.

19Unazijua amri: ‘Usizini, Usiue, Usiibe, Usitoe ushahidi wa uongo, Usidanganye, Waheshimu baba yako na mama yako.’”[#10:19 Taz Kut 20:12-16; Kumb 5:16-20. Ingawaje “usidaganye” haimo katika idadi ya amri kumi kama zijulikanavyo, inachukuliwa kuwa namna nyingine ya ile amri ya usiibe. Rejea Kumb 24:14; Yak 5:4.]

20Naye akamjibu, “Mwalimu, hayo yote nimeyazingatia tangu ujana wangu.”

21Yesu akamtazama, akampenda, akamwambia, “Umepungukiwa na kitu kimoja: nenda ukauze kila kitu ulicho nacho, uwape maskini hizo fedha, nawe utakuwa na hazina mbinguni, kisha uje unifuate.”

22Aliposikia hayo, alisikitika, akaenda zake akiwa na huzuni, kwa maana alikuwa na mali nyingi.

23Yesu akatazama pande zote, akawaambia wanafunzi wake, “Jinsi gani itakavyokuwa vigumu kwa matajiri kuingia katika ufalme wa Mungu!”

24Wanafunzi walishangazwa na maneno yake. Yesu akawaambia tena, “Watoto wangu, ni vigumu sana kuingia katika ufalme wa Mungu!

25Ni rahisi zaidi ngamia kupenya katika tundu la sindano, kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.”[#10:25 Msemo wa methali ulio na maana ya jambo lisilowezekana (aya 27).]

26Wanafunzi wake wakashangaa sana wakaulizana, “Ni nani basi, atakayeweza kuokoka?”

27Yesu akawatazama, akawaambia, “Kwa binadamu haiwezekani, lakini kwa Mungu si hivyo, maana kwa Mungu mambo yote huwezekana.”

28Petro akamwambia, “Na sisi je? Tumeacha yote, tukakufuata!”

29Yesu akasema, “Kweli nawaambieni, kila mtu aliyeacha nyumba, au ndugu, au dada, au mama, au baba, au watoto au mashamba kwa ajili yangu na kwa ajili ya Habari Njema,

30atapokea mara mia zaidi wakati huu wa sasa: nyumba, ndugu, dada, mama, watoto na mashamba pamoja na mateso; na katika wakati ujao atapokea uhai wa milele.[#10:30 Marko ndiye peke yake anayeongeza hapa “mateso” kama mojawapo ya tuzo watakazopata wafuasi waaminifu wa Yesu (taz Mat 19:29; Luka 18:30).]

31Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho, na walio wa mwisho watakuwa wa kwanza.”

Yesu anasema mara ya tatu kuhusu kifo na ufufuo wake

(Mat 20:17-19; Luka 18:31-34)

32Basi, walikuwa njiani kwenda juu Yerusalemu, na Yesu alikuwa anawatangulia. Wanafunzi wake walijawa na hofu, na watu waliofuata waliogopa. Yesu akawachukua tena kando wale kumi na wawili, akaanza kuwaambia yale yatakayompata:

33“Sikilizeni! Tunakwenda Yerusalemu, na huko Mwana wa Mtu atakabidhiwa kwa makuhani wakuu na waalimu wa sheria, nao watamhukumu auawe na kumkabidhi kwa watu wa mataifa.[#10:33 Hapa kwa maana ya wakuu wa Waroma.]

34Nao watamdhihaki; watamtemea mate, watampiga mijeledi na kumuua. Lakini baada ya siku tatu atafufuka.”

Ombi la Yakobo na Yohane

(Mat 20:20-28)

35Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo, walimwendea Yesu wakamwambia, “Mwalimu, tunataka utufanyie kitu tutakachokuomba.”[#10:35 Taz 1:19,29; 3:17; 5:37; 9:2; 13:3; 14:33.]

36Yesu akawauliza, “Mnataka niwafanyie nini?”

37Wakamjibu, “Uturuhusu kuketi mmoja upande wako wa kulia na mwingine upande wako wa kushoto katika utukufu wako.”[#10:37 Wafuasi wa Yesu walitazamia kwamba Yesu angeanzisha utawala wa kidunia ambao ungekuwa na nyadhifa mbalimbali na heshima. Upande wa kulia … upande wa kushoto: nafasi za heshima na mamlaka (taz Zab 110:1).]

38Yesu akawaambia, “Hamjui mnaomba nini! Je, mnaweza kunywa kikombe nitakachokunywa, au kubatizwa kama nitakavyobatizwa?”[#10:38 Taz Luka 12:50; Yoh 18:11. Msemo wa mfano wenye maana ya mateso na kifo cha Yesu (rejea 14:36; Yoh 18:11). Ubatizo hapa ni lugha ya mfano ikiwa na maana ya kifo (taz Luka 12:50).]

39Wakamjibu, “Tunaweza.” Yesu akawaambia, “Kikombe nitakachokunywa mtakinywa kweli, na mtabatizwa kama nitakavyobatizwa.[#10:39 Taz Mat 20:23 maelezo. Yakobo mwanawe Zebedayo aliuawa na Herode Agripa mwaka 42 B.K. (Mate 12:2), na kulingana na mapokeo ya Kikristo naye Yohane aliuawa mwanzoni mwa karne ya pili katika utawala wa mfalme mkuu wa Roma Trayano.]

40Lakini ni nani atakayeketi kulia au kushoto kwangu si wajibu wangu kupanga bali nafasi hizo watapewa wale waliotayarishiwa.”

41Wale wanafunzi wengine kumi waliposikia hayo, walianza kuchukizwa na Yakobo na Yohane.

42Hivyo, Yesu akawaita, akawaambia, “Mnajua kwamba wale wanaofikiriwa kuwa watawala wa mataifa huwatawala watu wao kwa mabavu, na wakuu hao huwamiliki watu wao.

43Lakini kwenu isiwe hivyo, ila anayetaka kuwa mkubwa kati yenu, sharti awe mtumishi wenu.

44Anayetaka kuwa wa kwanza, sharti awe mtumishi wa wote.

45Maana Mwana wa Mtu hakuja kutumikiwa, ila kutumikia, na kutoa maisha yake kuwa fidia ya watu wengi.”[#10:45 Rejea Isa 53:5-6,11-12; Yoh 10:11; 1Tim 2:5-6. Fidia: Mwanzoni neno “fidia” lilikuwa na maana ya kitu kilichotolewa au kilichotakiwa kutolewa ili kukomboa kitu fulani au hata mtu (taz kwa mfano Kut 21:8,30; Lawi 25:47-52; Hes 3:45-51) na baadaye neno hilo lilitumika kuhusu kukombolewa kwa watu wa Mungu na Yesu Kristo (k.m. Rom 3:23-25a; 1Tim 2:5-6; 1Pet 1:18-19). Kuhusu Yesu kutoa maisha yake kuwa fidia ya watu wengi taz Isa 52:13—53:12 sehemu ambayo inajulikana kama ya Mtumishi wa Bwana anayeteseka.]

Yesu anamponya kipofu Bartimayo

(Mat 20:29-34; Luka 18:35-43)

46Basi, wakafika Yeriko, naye Yesu alipokuwa anatoka katika mji huo akiwa na wanafunzi wake pamoja na umati mkubwa wa watu, kipofu, mwana wa Timayo aitwaye Bartimayo, alikuwa ameketi kando ya barabara, anaomba maskini.[#10:46 Mji katika bonde la Mto Yordani yapata kilomita 10 magharibi mwa mto Yordani na kaskazini mwa Bahari ya Chumvi.]

47Aliposikia kwamba ni Yesu wa Nazareti aliyekuwa anapita mahali hapo, alianza kupaza sauti, “Yesu, Mwana wa Daudi, nihurumie!”[#10:47 Maneno haya ni jina la sifa la Masiha; taz Mat 9:27 maelezo.]

48Watu wengi walimkemea ili anyamaze, lakini yeye akazidi kupaza sauti, “Mwana wa Daudi, nihurumie!”

49Yesu alisimama, akasema, “Mwiteni.” Basi, wakamwita huyo kipofu, wakamwambia, “Jipe moyo! Simama, anakuita.”

50Naye akatupilia mbali vazi lake, akaruka juu, akamwendea Yesu.

51Yesu akamwuliza, “Unataka nikufanyie nini?” Huyo kipofu akamwambia, “Mwalimu, naomba nipate kuona.”

52Yesu akamwambia, “Nenda, imani yako imekuponya.” Mara huyo kipofu akaweza kuona, akamfuata Yesu njiani.[#10:52 Au, Imani yako imekuokoa: Mat 9:22; Marko 5:34.]

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania