The chat will start when you send the first message.
1Walipokuwa wanakaribia Yerusalemu walifika Bethfage na Bethania, karibu na mlima wa Mizeituni. Hapo aliwatuma wawili wa wanafunzi wake,[#11:1 Mahali penyewe hasa si dhahiri. Bethania: Huo ulikuwa mji yapata kilomita 3 kusini-mashariki ya mji wa Yerusalemu (taz Yoh 11:18). Mlima wa Mizeituni: Huki kilikuwa kilima upande wa mashariki wa mji Yerusalemu na ambacho kimehusishwa kwanza na kutekwa kwa mji wa Yerusalemu (2Sam 15:13-30) na baadaye pia kikawa kama ishara ya matumaini ya ushindi wa Mungu nyakati za mwisho (Zek 14:4).]
2akawaambia, “Nendeni katika kijiji kilicho mbele yenu. Mtakapokuwa mnaingia humo, mtakuta mwanapunda amefungwa, ambaye bado hajatumiwa na mtu. Mfungueni mkamlete.[#11:2 Matumizi yake hapa huenda yalihusishwa na hali ya unyenyekevu ya mfalme (Zek 9:9; Mat 21:5; Yoh 12:15).]
3Kama mtu akiwauliza, ‘Mbona mnafanya hivyo?’ Mwambieni, ‘Bwana anamhitaji na atamrudisha hapa mara.’”[#11:3 Taz 5:19. Wengine wanatafsiri Bwana hapa kwa neno “Mwenyewe” yaani kwa maana ya mwenye punda huyo.]
4Basi, wakaenda, wakamkuta mwanapunda barabarani amefungwa mlangoni. Walipokuwa wakimfungua,
5baadhi ya watu waliokuwa wamesimama hapo wakawauliza, “Kwa nini mnamfungua huyo mwanapunda?”
6Wanafunzi wakajibu kama Yesu alivyokuwa amewaambia; nao wakawaacha waende zao.
7Wakampelekea Yesu huyo mwanapunda. Wakatandika mavazi yao juu ya huyo mwanapunda na Yesu akaketi juu yake.
8Watu wengi wakatandaza mavazi yao barabarani; wengine wakatandaza matawi ya miti waliyoyakata mashambani.[#11:8 Kutandaza mavazi barabarani wakati wa tukio hilo ilikuwa kitendo cha kumkaribisha Yesu (rejea 2Fal 9:13) na chakumbusha maandamano ya sikukuu za Waisraeli.]
9Watu wote waliotangulia na wale waliofuata, wakapaza sauti zao wakisema, “Sifa! Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Bwana![#11:9 Tafsiri ya neno la Kiebrania “Hosana” ambalo awali lilikuwa na maana ya ombi. “Okoa tafadhali”, lakini baadaye neno likatumika katika mazingira ya kushangilia ushindi na kuimba sifa (taz Zab 118:25-26).]
10Ubarikiwe ufalme ujao wa baba yetu Daudi. Sifa kwa Mungu juu mbinguni!”
11Yesu aliingia mjini Yerusalemu akaenda moja kwa moja mpaka hekaluni, akatazama kila kitu kwa makini. Lakini kwa vile ilikwisha kuwa jioni, akaenda Bethania pamoja na wale kumi na wawili.[#11:11 Yahusu jengo mahsusi lililokuwa kitovu cha maisha ya kidini ya Wayahudi. Jengo lenyewe lilijengwa na Herode Mkuu ambaye aliishi yapata mwaka wa 37 K.K. mpaka mwaka wa 4 B.K. Baadaye, mnamo mwaka wa 70 B.K., jengo hilo liliteketezwa na Waroma (taz Luka 19:41-44).]
12Kesho yake, walipokuwa wanatoka Bethania, Yesu aliona njaa.
13Basi, akaona kwa mbali mtini wenye majani mengi. Akauendea ili aone kama ulikuwa na tunda lolote. Alipoufikia, aliukuta bila tunda lolote ila tu majani matupu, kwa vile hayakuwa majira yake ya matunda.[#11:13 Kidogo msemo huu unatatanisha: (a) Kama haukuwa wakati wa matunda mbona Yesu anatafuta matunda humo? (b) Na kama si wakati wa matunda kwa nini upatilizwe? Huenda kitendo hicho cha mtini na matunda ni ishara ya kitu kingine: yahusu wakuu wa Wayahudi waliokataa kupokea mafundisho ya Yesu na hawana matunda, hali walitakiwa kuwa nayo kila wakati. Kwa hiyo wanahukumiwa adhabu. Katika A.K. taifa la Israeli lililinganishwa na mtini: Yer 8:13; Hos 9:10,16-17; na pia katika A.J. (Luka 13:6-9).]
14Hapo akauambia mtini, “Tangu leo hata milele mtu yeyote asile matunda kwako.” Nao wanafunzi wake walisikia maneno hayo.
15Basi, wakafika Yerusalemu. Yesu akaingia hekaluni akaanza kuwafukuza nje watu waliokuwa wanauza na kununua vitu humo. Akazipindua meza za wale waliokuwa wakibadilishana fedha, na viti vya wale waliokuwa wakiuza njiwa.
16Hakumruhusu mtu yeyote kupitia hekaluni akichukua kitu.
17Kisha akawafundisha, “Imeandikwa: ‘Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa ajili ya mataifa yote!’ Lakini nyinyi mmeifanya kuwa pango la wanyang'anyi!”[#11:17 Isa 56:7.; #11:17 Yer 7:11.]
18Makuhani wakuu na waalimu wa sheria waliposikia hayo, walianza kutafuta njia ya kumwangamiza. Lakini walimwogopa kwa sababu umati wa watu ulishangazwa na mafundisho yake.
19Ilipokuwa jioni, Yesu na wanafunzi wake waliondoka mjini.
20Asubuhi na mapema, walipokuwa wanapita, waliuona ule mtini umenyauka wote, hata mizizi.
21Petro aliukumbuka, akamwambia Yesu, “Mwalimu, tazama! Ule mtini ulioulaani, umenyauka!”
22Yesu akawaambia, “Mwaminini Mungu.
23Nawaambieni kweli, mtu akiuambia mlima huu: ‘Ng'oka ukajitose baharini,’ bila kuona shaka moyoni mwake, ila akaamini kwamba mambo yote anayosema yanafanyika, atafanyiwa jambo hilo.[#11:23 Madhumuni ya maneno hayo ni kutilia mkazo kwamba, kwa imani, mambo yasiyowezekana huwezekana. Kuhusu maneno kama hayo juu ya imani, taz Mat 17:20; 1Kor 13:2.]
24Kwa hiyo nawaambieni, mnaposali na kuomba kitu, aminini kwamba mmekipokea, nanyi mtapewa.
25Mnaposimama kusali, msameheni kila mtu aliyewakosea chochote, ili Baba yenu aliye mbinguni awasamehe nyinyi makosa yenu.”[#11:25 Hati nyingine za kale zina aya 26. “Lakini msipowasamehe wengine hata Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe nyinyi makosa yenu” (taz Mat 6:14-15).]
27Basi, wakafika tena Yerusalemu. Yesu alipokuwa akitembea hekaluni, makuhani wakuu, waalimu wa sheria na wazee walimwendea,[#11:27-28 Swali la waalimu wa sheria na makuhani juu ya mamlaka ya Yesu limetokana na mambo hayo aliyotenda Yesu kama inavyosimuliwa katika aya 1-26.]
28wakamwuliza, “Unafanya mambo haya kwa mamlaka gani? Nani aliyekupa mamlaka ya kufanya mambo haya?”
29Lakini Yesu akawaambia, “Nitawaulizeni swali moja; mkinijibu, nami pia nitawaambia ninafanya mambo haya kwa mamlaka gani.
30Je, mamlaka ya Yohane ya kubatiza yalitoka mbinguni ama kwa watu? Nijibuni.”
31Wakaanza kujadiliana, “Tukisema, ‘Yalitoka mbinguni’, atatuuliza, ‘Basi, mbona hamkumsadiki?’
32Na tukisema, ‘Yalitoka kwa watu…’” (Waliogopa umati wa watu maana wote waliamini kwamba Yohane alikuwa kweli nabii.)
33Basi, wakamjibu Yesu, “Sisi hatujui.” Naye Yesu akawaambia, “Nami pia sitawaambieni ninafanya mambo haya kwa mamlaka gani.”