The chat will start when you send the first message.
1Baadhi ya Mafarisayo na waalimu wa sheria waliokuwa wametoka Yerusalemu walikusanyika mbele ya Yesu.
2Waliona kwamba baadhi ya wanafunzi wake walikula mikate kwa mikono najisi, yaani bila kunawa.
3Maana Mafarisayo na Wayahudi wengine wote huzingatia mapokeo ya wazee wao: hawali kitu kabla ya kunawa mikono ipasavyo.[#7:3 Yaani vipengele na fafanuzi za sheria ambavyo Mafarisayo waliviona vyote kuwa vyapaswa kufuatwa (taz pia Gal 1:14).]
4Tena, hawali kitu chochote kutoka sokoni, mpaka wamekiosha kwanza. Kuna pia desturi nyingine walizozipokea toka zamani kama vile namna ya kuosha vikombe, sufuria na vyombo vya shaba.
5Basi, Mafarisayo na waalimu wa sheria wakamwuliza Yesu, “Kwa nini wanafunzi wako hawafuati mapokeo tuliyoyapokea kwa wazee wetu, bali hula chakula kwa mikono najisi?”
6Yesu akawajibu, “Wanafiki nyinyi! Nabii Isaya alitabiri sawa kabisa juu yenu alipoandika:
‘Mungu asema: Watu hawa, huniheshimu kwa maneno tu,
lakini mioyoni mwao, wako mbali nami.
7Kuniabudu kwao hakufai,
maana mambo wanayofundisha ni maagizo ya kibinadamu tu.’
8Nyinyi mnaiacha amri ya Mungu na kushikilia maagizo ya watu.”
9Yesu akaendelea kusema, “Nyinyi mnajua kuepa kwa ujanja sheria ya Mungu kwa ajili ya kufuata mapokeo yenu!
10Maana Mose aliamuru: ‘Waheshimu baba yako na mama yako,’ na, ‘Anayemtukana baba yake au mama yake, lazima afe’.[#7:10 Kut 20:12; Kumb 5:16.; #7:10 Kut 21:17; Lawi 20:9.]
11Lakini nyinyi mwafundisha, ‘Kama mtu anacho kitu ambacho angeweza kumsaidia nacho baba yake au mama yake, lakini akasema kwamba kitu hicho ni Korbani (yaani zawadi kwa Mungu),[#7:11 Neno la Kiebrania ambalo mwandishi Marko hapa, kama desturi yake, anatafsiri kuwa “zawadi” kwa Mungu. Vitu vilivyowekwa wakfu kwa Mungu haviwezi kutumiwa kwa shughuli nyingine na, kulingana na mapokeo ya waalimu wa Kiyahudi, haviwezi kutumiwa hata kwa kuwasaidia wazazi wao wenyewe. Hatuna mahali popote katika Biblia, licha ya mahali hapa, ambapo desturi hiyo inatajwa.]
12basi, halazimiki tena kumsaidia baba yake au mama yake’.
13Hivyo ndivyo mnavyodharau neno la Mungu kwa ajili ya mafundisho mnayopokezana. Tena mnafanya mambo mengi ya namna hiyo.”
14Yesu aliuita tena ule umati wa watu, akawaambia, “Nisikilizeni nyote, mkaelewe.
15Hakuna kitu kinachoingia ndani ya mtu kutoka nje kinachoweza kumtia mtu unajisi. Lakini kinachotoka ndani ya mtu ndicho kinachomtia mtu unajisi.”[#7:15 Au kumfanya mchafu kidini. Kadiri ya mafundisho ya Kiyahudi mtu ni lazima awe “safi” anapokwenda kuabudu; kwa sababu hiyo matendo fulanifulani yalimfanya mtu kuwa najisi au mchafu hata asiruhusiwe kuingia hekaluni (aya 18-23; taz Mat 15:11).; #7:15 Hati nyingine za kale zina aya 16: “Aliye na masikio na asikie”.]
17Alipouacha umati wa watu na kuingia nyumbani, wanafunzi wake walimwuliza maana ya huo mfano.
18Naye akawaambia, “Je, hata nyinyi hamwelewi? Je, hamwelewi kwamba kitu kinachomwingia mtu kutoka nje, hakiwezi kumtia unajisi,
19kwa maana hakimwingii moyoni, ila tumboni, na baadaye hutolewa nje chooni?” (Kwa kusema hivyo, Yesu alihalalisha vyakula vyote.)[#7:19 Mwandishi Marko hata hapa anafafanua zaidi msemo wa Yesu kwa kujazia maelezo hayo yaliyo katika mabano, ikiwa ni dhahiri kwamba maagizo ya Sheria kuhusu vyakula najisi hayawabani tena Wakristo (taz Mate 10:9-16).]
20Akaendelea kusema, “Kinachotoka ndani ya mtu ndicho kinachomtia unajisi.
21Maana kutoka ndani, moyoni mwa mtu, hutoka mawazo mabaya, uasherati, wizi, uuaji,[#7:21-22 Taz Rom 1:31 kuhusu orodha ya matendo yasiyofaa.]
22uzinzi, uchoyo, uovu, udanganyifu, ufisadi, wivu, kashfa, kiburi na upumbavu.
23Maovu hayo yote yatoka ndani ya mtu, nayo humtia mtu unajisi.”
24Yesu aliondoka hapo, akaenda wilaya ya Tiro. Huko aliingia katika nyumba moja na hakutaka mtu ajue; lakini hakuweza kujificha.[#7:24 Taz pia 3:8. Eneo hilo waliishi watu wasio Wayahudi.]
25Hapo mwanamke mmoja ambaye binti yake alikuwa na pepo, alisikia habari za Yesu. Basi, akaja akajitupa chini mbele ya miguu yake.
26Mama huyo alikuwa Mgiriki, mwenyeji wa Sirofoinike. Basi, akamwomba Yesu amtoe binti yake pepo mchafu.[#7:26 Sirofoinike ilikuwa eneo la pwani la mkoa wa Waroma wa Siria.]
27Yesu akamwambia, “Kwanza watoto washibe; kwa maana si vizuri kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.”[#7:27 Wayahudi wengine wakati huo waliwaita watu wasio Wayahudi “mbwa”. Yesu anatumia msemo huo kwa ufundi wa kimaandishi na kusababisha huyo mama aendelee na ombi lake ambalo Yesu anamkubalia (aya 28). Taz Mat 15:26 maelezo.]
28Lakini huyo mama akasema, “Ni kweli, Bwana; lakini hata mbwa walio chini ya meza hula makombo ya watoto.”
29Yesu akamwambia, “Kwa sababu ya neno hilo, nenda. Pepo amemtoka binti yako!”
30Basi, akaenda nyumbani kwake, akamkuta mtoto amelala kitandani, na pepo amekwisha mtoka.
31Kisha Yesu aliondoka wilaya ya Tiro, akapitia Sidoni, akafika ziwa Galilaya kwa kupitia nchi ya Dekapoli.
32Basi, wakamletea bubu kiziwi, wakamwomba amwekee mikono.
33Yesu akamtenga na umati wa watu, akamtia vidole masikioni, akatema mate na kumgusa ulimi.[#7:33 Rejea Marko 8:23; Yoh 9:6. Nyakati hizo mate yalitumiwa katika baadhi ya shughuli za kuponya.]
34Kisha akatazama juu mbinguni, akapiga kite, akamwambia, “Efatha,” maana yake “Funguka.”[#7:34 Neno la Kiaramu; taz maelezo ya 5:41.]
35Mara masikio yake yakafunguka na ulimi wake ukafunguliwa, akaanza kusema sawasawa.
36Yesu akawaamuru wasimwambie mtu juu ya jambo hilo. Lakini kadiri alivyowakataza, ndivyo walivyozidi kutangaza habari hiyo.[#7:36 Taz maelezo ya Marko 1:34.]
37Watu walishangaa sana, wakasema, “Amefanya yote vyema: amewajalia viziwi kusikia, na mabubu kusema!”