The chat will start when you send the first message.
1Afadhali maskini aishiye kwa unyofu,
kuliko mtu mpotovu wa maneno na mpumbavu.
2Haifai mtu kuwa bila akili;
mwenda harakaharaka hujikwaa.
3Mtu akijiangamiza kwa upumbavu wake,
huielekeza hasira yake dhidi ya Mwenyezi-Mungu.
4Mali huvuta marafiki wengi wapya,
lakini maskini huachwa bila rafiki.
5Shahidi mwongo hataacha kuadhibiwa;[#19:5 Methali inakataza utumiaji vibaya wa maneno, aghalabu kuacha kusema ukweli na kusema kinyume chake. Rejea pia Meth 6:19; 19:9; 12:17-18; 25:18. Amri ya Mungu pia imekataza kusema uongo (Kut 20:16).]
asemaye uongo hataepa adhabu.
6Watu wengi hujipendekeza kwa wakuu;
kila mtu hutaka kuwa rafiki ya mtu mkarimu.
7Maskini huchukiwa na ndugu zake;
marafiki zake ndio zaidi: humkimbia!
Hata awabembeleze namna gani hatawapata.
8Ajipatiaye hekima anaipenda nafsi yake;
anayezingatia busara atastawi.
9Shahidi mwongo hatakosa kuadhibiwa;
asemaye uongo ataangamia.
10Haifai kwa mpumbavu kuishi kwa anasa,[#19:10 Inawezekana madhumuni ya msemo huo ni kuonesha kwamba maisha ya jamii yanapaswa kulingana na mpango au utaratibu wa hekima uliowekwa na Mungu hivyo kwamba mpumbavu hana nafasi katika mpango huo (1:29-32). Tena mtumwa hakutakiwa kutawala wakuu isipokuwa kama huyo mkuu alikuwa mpumbavu au aliwatendea vibaya watu wake wakaasi.]
tena ni vibaya zaidi mtumwa kuwatawala wakuu.
11Mwenye busara hakasiriki upesi;
kusamehe makosa ni fahari kwake.
12Ghadhabu ya mfalme ni kama ngurumo ya simba,
lakini wema wake ni kama umande juu ya majani.
13Mtoto mpumbavu ni balaa kwa baba yake;
na ugomvi wa mke ni kama matone ya mvua yasiyoisha.
14Nyumba na mali ni urithi apatao mtu kwa wazee wake,
lakini mke mwenye busara hutoka kwa Mwenyezi-Mungu.
15Uzembe ni kama usingizi mzito;
mtu mvivu atateseka kwa njaa.
16Anayeshika amri anasalimisha maisha yake;
anayepuuza agizo atakufa.
17Anayemsaidia maskini anamkopesha Mwenyezi-Mungu;[#19:17 Methali inatilia mkazo wajibu wa kumsaidia maskini (14:21,31; 17:5; 21:13; 22:9,16).]
Mwenyezi-Mungu atamlipa kwa tendo lake jema.
18Mrudi mwanao kungali bado na tumaini,
lakini usimwadhibu kiasi cha kumwangamiza.
19Mtu wa hasira kali lazima apate adhabu;
ukimwachia mara moja itakubidi kumwachia tena.
20Sikiliza shauri na kupokea mafundisho,
upate hekima ya kukufaa siku zijazo.
21Kichwani mwa mtu mna mipango mingi,
lakini anachokusudia Mwenyezi-Mungu ndicho kitakachofanyika.
22Kinachotakiwa kwa mtu ni uaminifu;
afadhali mtu maskini kuliko mtu mwongo.
23Kumcha Mwenyezi-Mungu kunaleta uhai;[#19:23 Rejea 9:10 na 1:7 maelezo.]
amchaye hujaliwa pumziko la kutosheleza,
wala hatapatwa na baa lolote.
24Mvivu ni kama mtu atiaye mkono katika sahani ya chakula,
lakini hana nguvu ya kuuinua hadi mdomoni.
25Mwadhibu mwenye mzaha naye mjinga atapata akili;
mwonye mwenye busara naye atapata maarifa.
26Anayemdhulumu baba yake na kumfukuza mama yake,[#19:26 Heshima kwa wazazi ni jambo linalotakiwa katika Biblia na tamaduni za mataifa mengi zinashikilia hivyo. Kuhusu amri ya kuwaheshimu wazazi taz Kut 20:12; Kumb 5:16.]
ni mtoto asiyefaa na mpotovu.
27Mwanangu, ukiacha kusikiliza mafundisho,
utapotea mara mbali na maneno ya hekima.
28Shahidi asiyefaa kitu huidhihaki haki;
na kinywa cha mwovu hubugia uovu.
29Adhabu iko tayari kwa wenye mzaha,
mijeledi imetayarishwa kuchapa migongo ya wapumbavu.