Methali 30

Methali 30

Mawaidha ya Aguri

1Maneno ya Aguri, mwana wa Yake. Mawaidha ambayo mtu huyu alimwambia Ithieli, naam, Ithieli na Ukali.[#30—31 Sura mbili za mwisho za Kitabu cha Methali ni mkusanyo wa methali au misemo ya hekima ya watu ambao hawajulikani pengine katika Biblia: Aguri na Mama wa Lemueli. Methali nyingi za sura 30 ni orodha ya maelezo, na zile za sura 31 ni mawaidha kwa mfalme nazo zinaeleza mke mzuri ni wa namna gani.; #30:1 Jina Aguri linapatikana hapa tu katika Biblia; kadhalika na jina Ukali halitajwi pengine katika Biblia.; #30:1 Neno “Mawaidha” limechukuliwa na wengine kuwa ni jina la mahali “Masa” na kama ni hivyo Aguri angekuwa na uhusiano na mahali hapo ambapo inadhaniwa kuwa ni mahali kaskazini ya Arabia ambapo waliishi mababu wa Ishmaeli (Mwa 25:12-18). Na kuhusu “Ithieli … Ithieli na Ukali” wengine wanatafsiri: “Mungu hayuko nami, Mungu hayuko nami; sijiwezi!” Makala ya Kiebrania si dhahiri hapa. Tafsiri ya Kigiriki ya Septuajinta (LXX) hali kadhalika na Vulgata hazitambui Ithieli na Ukali kuwa majina.]

2Mimi ni mpumbavu mno, wala si mtu;

nayo akili ya binadamu sina.

3Sijajifunza hekima,

wala sijui kitu juu ya Mungu Mtakatifu.

4Ni nani aliyepanda juu mbinguni akashuka chini?[#30:4 Hapa tuna mfululizo wa maswali ambayo yote majibu yake ni “Hayupo binadamu awezaye kufanya vitu hivyo”. Zingatia maswali ya Mungu kwa Yobu (38:1—39:30); taz pia Yoh 3:13.]

Ni nani aliyekamata upepo mkononi?

Ni nani aliyefunga maji katika kitambaa?

Ni nani aliyeiweka mipaka yote ya dunia?

Jina lake ni nani? Na ni nani jina la mwanawe?

Niambie kama wajua!

5Maneno yote ya Mungu ni ya kuaminika;

yeye ni ngao yao wote wanaomkimbilia.

6Usiongeze neno katika maneno yake,

asije akakukemea, nawe ukaonekana mwongo.

7Mambo haya mawili nakuomba ee Mungu,

wala usinikatalie kabla sijafa:

8Uniondolee uongo na udanganyifu;

usinipe umaskini wala utajiri;

unipatie chakula ninachohitaji,

9nisije nikashiba nikakukana;

nikasema, “Mwenyezi-Mungu ni nani?”

Au nisije nikawa maskini nikaiba,

na kulikufuru jina lako ee Mungu wangu.

10Usimchongee mtumwa kwa bwana wake,[#30:10 Nyakati hizo watu wenye watumwa waliwatendea watumwa kama watoto na ilikuwa rahisi kuwaadhibu hata kama sababu ya adhabu haikuthibitiwa.]

asije akakulaani, ukaonekana una hatia.

11Kuna watu ambao huwalaani baba zao,

wala hawana shukrani kwa mama zao.

12Kuna watu ambao hujiona kuwa wema,

kumbe bado hawajatakaswa uchafu wao.

13Kuna na wengine — kiburi ajabu!

hudharau kila kitu wanachokiona.

14Kuna watu ambao meno yao ni kama upanga,

na magego yao ni kama visu.

Wako tayari kuwatafuna maskini wa nchi,

na wanyonge walio miongoni mwa watu!

Methali za kialfabeti

15Mruba anao binti wawili wasemao, “Nipe, nipe!”[#30:15 “Mruba” ni namna ya mmea wenye matunda meupe; hapa unatumika aghalabu kama mfano wa tamaa. Na kuhusu “vitu vitatu … vinne” huu ni mtindo wa kisanii wa mtunzi wa methali wa kupamba anachotaka kusema. Mtindo huo anautumia katika methali zake zote tangu 30:15 mpaka ya 30:31.]

Kuna vitu vitatu ambavyo kamwe havishibi,

naam, vitu vinne visivyosema, “Imetosha!”

16Kuzimu,

tumbo la mwanamke lisilozaa,

ardhi isiyoshiba maji,

na moto usiosema, “Imetosha!”

17Kama mtu akimdhihaki baba yake,

na kudharau utii kwa mama yake,

kunguru wa bondeni watamdonoa macho,

na kuliwa na tai.

18Kuna mambo matatu yaliyo ya ajabu kwangu,

naam, mambo manne nisiyoyaelewa:

19njia ya tai angani,

njia ya nyoka mwambani,

njia ya meli baharini,

na kinachomvuta mwanamume kwa mwanamke.

20Mwenendo wa mwanamke mwasherati ni hivi:[#30:20 Kuhusu hatari inayohusika kwa mwanamke huyo taz 2:16-19. Maneno “hula, akapangusa mdomo” yanatumika hapa kimfano kwa maana ya kufanya kitendo cha kujamiiana (taz pia 9:17).]

yeye hula, akajipangusa mdomo,

na kusema, “Sijafanya kosa lolote!”

21Kuna mambo matatu ambayo huitetemesha dunia,

naam, mambo manne ambayo haiwezi kuyastahimili:

22mtumwa anayekuwa mfalme;

mpumbavu anayeshiba chakula;

23mwanamke asiyependwa anayeolewa;

na mjakazi achukuapo nafasi ya bibi yake.

24Kuna viumbe vinne vidogo sana duniani,

lakini vina akili sana:

25sisimizi: wadudu wasio na nguvu,

lakini hujihifadhia chakula wakati wa kiangazi;

26pelele: wanyama wasio na uwezo,

lakini hujitengenezea makao miambani;

27nzige: hawana mfalme,

lakini wote huenda pamoja kwa vikosi;

28mjusi: waweza kumshika mkononi,[#30:25-28 Viumbe vidogo vinavyosifika kwa uwezo wao: sisimizi kwa bidii yao ya kufanya kazi (6:6-8); pelele kwa kuweza kuishi katika mazingira magumu ya miamba jangwani (Zab 104:18); nzige kwa kuweza kuruka pamoja katika jeshi kubwa (Yoe 1:4) na mjusi (au buibui) kwa uwezo wa kuingia hata ndani ya ikulu.]

lakini huingia katika ikulu.

29Kuna viumbe vitatu vyenye mwendo wa kupendeza,

naam, kuna viumbe vinne vyenye mwendo mzuri;

30simba: mnyama mwenye nguvu kuliko wote,

wala hamwogopi mnyama mwingine yeyote;

31jogoo aendaye kwa maringo;

tena beberu;

na mfalme mbele ya watu wake.

32Kama umekuwa mpumbavu hata ukajisifu,

au kama umekuwa unapanga maovu,

chunga mdomo wako.

33Maana ukisukasuka maziwa utapata siagi,

ukimpiga mtu pua atatoka damu;

kadhalika kuchochea hasira huleta ugomvi.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania