The chat will start when you send the first message.
1Usikie sala yangu, ee Mwenyezi-Mungu,
na kilio changu kikufikie.
2Usijifiche mbali nami wakati wa taabu!
Unitegee sikio lako,
unijibu upesi wakati ninapokuomba!
3Siku zangu zapita kama moshi;
mifupa yangu yaungua kama katika tanuri.
4Nimepondwa moyoni kama nyasi na kunyauka;
sina hata hamu ya chakula.
5Kutokana na kusononeka kwangu,
nimebaki mifupa na ngozi.
6Nimekuwa kama ndege wa jangwani;
kama bundi kwenye mahame.
7Ninalala macho wazi,
kama ndege mkiwa juu ya paa.
8Mchana kutwa maadui zangu wananisimanga,
wanaonidhihaki hutumia jina langu kulaania.
9Majivu yamekuwa chakula changu,[#102:9 Katika Biblia mara nyingi “majivu” yanatumika kama mfano wa maombolezo na huzuni na kwa sababu hiyo mstari huu wa kwanza wa aya hii ni sambamba kimaana na mstari wa pili.]
machozi nayachanganya na kinywaji changu,
10kwa sababu ya ghadhabu na hasira yako,
maana umeniokota na kunitupilia mbali.
11Maisha yangu ni kama kivuli cha jioni;
ninanyauka kama nyasi.
12Lakini wewe, ee Mwenyezi-Mungu, watawala milele;
jina lako lakumbukwa vizazi vyote.
13Wewe utainuka na kuurehemu mji wa Siyoni;
maana wakati umefika wa kuutendea mema;
wakati wake uliopangwa umefika.
14Watumishi wako wanauthamini sana,
ujapokuwa magofu sasa;
wanauonea huruma,
ingawa umeharibika kabisa.
15Mataifa yataliheshimu jina la Mwenyezi-Mungu;
wafalme wote duniani wataogopa utukufu wake.
16Mwenyezi-Mungu ataijenga upya Siyoni,
na kuonekana alivyo mtukufu.
17Ataikubali sala ya fukara;
wala hatayakataa maombi yao.
18Andika jambo hili kwa ajili ya vizazi vijavyo;
watakaozaliwa baadaye wamsifu Mwenyezi-Mungu.
19Kwamba aliangalia chini kutoka patakatifu pake juu,
Mwenyezi-Mungu aliangalia dunia kutoka mbinguni,
20akasikia lalamiko la wafungwa;[#102:20 Labda hapa “wafungwa” ni wale watu waliopelekwa uhamishoni na ambao katika aya 17 wanaitwa fukara yaani wasio na kitu na labda bila makao.]
akawaachilia huru waliohukumiwa kuuawa.
21Hivyo watu watatangaza jina la Mwenyezi-Mungu huko Siyoni;
sifa zake zitatangazwa huko Yerusalemu,
22wakati mataifa yatakapokusanyika pamoja
na falme zitakutana kumwabudu Mwenyezi-Mungu.
23Mungu amenipunguzia nguvu ningali kijana;
ameyafupisha maisha yangu.
24Ee Mungu wangu, usinichukue sasa
wakati ningali bado kijana.
Ee Mwenyezi-Mungu wewe wadumu milele.
25Wewe uliiumba dunia zamani za kale,[#102:25 Hapa Mwanazaburi anakumbusha kwa kifupi simulizi lile refu la kuumbwa ulimwengu katika Mwa 1:3-10.]
mbingu ni kazi ya mikono yako.
26Hizo zitatoweka, lakini wewe wabaki;
hizo zitachakaa kama vazi.
Utazitupilia mbali kama nguo,
nazo zitapotelea mbali.
27Lakini wewe ni yuleyule daima,
na maisha yako hayana mwisho.
28Watoto wa watumishi wako watakaa salama;
wazawa wao wataimarishwa mbele yako.