Zaburi 15

Zaburi 15

Rafiki ya Mungu

1Nani ee Mwenyezi-Mungu atakayekaa hemani mwako?

Nani atakayeishi juu ya mlima wako mtakatifu?

2Ni mtu aishiye bila lawama,

atendaye daima yaliyo mema,

asemaye ukweli kutoka moyoni;

3ni mtu asiyesengenya watu,

asiyemtendea uovu rafiki yake,

wala kumfitini jirani yake;

4ni mtu anayewadharau wafisadi,

lakini huwaheshimu wamchao Mwenyezi-Mungu;

ni mtu asiyegeuza kiapo chake hata kikimtia hasara;

5asiyekopesha fedha yake kwa riba,

wala kupokea rushwa kumdhulumu asiye na hatia.

Mtu atendaye hayo,

kamwe hatatikisika.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania