The chat will start when you send the first message.
1Ee Mwenyezi-Mungu, unitetee,
maana nimeishi bila hatia,
nimekutumainia wewe bila kusita.
2Unijaribu, ee Mwenyezi-Mungu, na kunipima;
uchunguze moyo wangu na akili zangu.
3Fadhili zako ziko mbele ya macho yangu,[#26:3 Mtunzi wa Zaburi daima (mbele ya macho yangu) ana tumaini kubwa kuhusu wema wake Mungu.]
ninaishi kutokana na uaminifu wako.
4Sijumuiki na watu wapotovu;
sishirikiani na watu wanafiki.
5Nachukia mikutano ya wabaya;
wala sitajumuika na waovu.
6Nanawa mikono yangu kuonesha sina hatia,[#26:6 Katika ibada hekaluni, makuhani walipaswa kunawa mikono na miguu kabla ya kutoa tambiko (Kut 30:18-21).]
na kuizunguka madhabahu yako, ee Mwenyezi-Mungu,
7nikiimba wimbo wa shukrani,
na kusimulia matendo yako yote ya ajabu.
8Ee Mwenyezi-Mungu, napenda makao yako,
mahali unapokaa utukufu wako.
9Usiniangamize pamoja na wenye dhambi,
wala usinitupe pamoja na wauaji,
10watu ambao matendo yao ni maovu daima,
watu ambao wamejaa rushwa.
11Lakini mimi ninaishi kwa unyofu;
unihurumie na kunikomboa.
12Mimi nimesimama mahali palipo imara;[#26:12 Lugha ya mfano kuashiria hali sahihi na imara mbele ya Mungu.]
nitamsifu Mwenyezi-Mungu katika kusanyiko kubwa.