Zaburi 64

Zaburi 64

Sala ya kuomba ulinzi wa Mungu

1Usikie, ee Mungu, lalamiko langu;

yalinde maisha yangu na vitisho vya maadui.

2Unikinge na njama za waovu,

na ghasia za watu wabaya.

3Wananoa ndimi zao kama upanga,

wanafyatua maneno ya ukatili kama mishale.

4Toka mafichoni wamshambulia mtu mnyofu,

wanamshambulia ghafla bila kuogopa.

5Wanashirikiana katika nia yao mbaya;

wanapatana mahali pa kuficha mitego yao.

Wanafikiri: “Hakuna atakayeweza kuiona.”

6Hufanya njama zao na kusema:

“Sasa tumekamilisha mpango!

Nani atagundua hila zetu?”

Mipango ya siri imefichika moyoni mwa mtu!

7Lakini Mungu atawapiga mishale,[#64:7 Hao maadui (64:3) walishindwa kutambua kwamba Mungu anayo pia “mishale”.]

na kuwajeruhi ghafla.

8Atawaangamiza kwa sababu ya maneno yao;[#64:8 Au: Maneno yao yatawaangamiza. Namna hii ya kusema hutumika mara kwa mara katika vitabu au maandishi ya hekima.]

kila atakayewaona atatikisa kichwa.

9Hapo watu wote wataogopa;

watatangaza aliyotenda Mungu,

na kufikiri juu ya matendo yake.

10Waadilifu watafurahi kwa sababu ya Mwenyezi-Mungu,

na kukimbilia usalama kwake;

watu wote wanyofu wataona fahari.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania