Zaburi 95

Zaburi 95

Utenzi wa kumsifu Mungu

1Njoni tumwimbie Mwenyezi-Mungu,

tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!

2Twende mbele zake na shukrani;

tumshangilie kwa nyimbo za sifa.

3Maana Mwenyezi-Mungu, ni Mungu mkuu;

yeye ni Mfalme mkuu juu ya miungu yote.

4Vilindi vyote vya dunia vimo mikononi mwake,

vilele vya milima ni vyake.

5Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;

kwa mikono yake aliiumba nchi kavu.

6Njoni tusujudu na kumwabudu;

tumpigie magoti Mwenyezi-Mungu, Muumba wetu!

7Maana yeye ni Mungu wetu,

nasi ni watu wa kundi lake,

ni kondoo wake anaowachunga.

Laiti leo mngesikiliza sauti yake:

8“Msiwe wakaidi kama kule Meriba,

kama walivyokuwa kule Masa jangwani,

9wazee wenu waliponijaribu na kunipima,

ingawa walikuwa wameona mambo niliyowatendea.

10Kwa miaka arubaini nilichukizwa nao,

nikasema: ‘Kweli, hawa ni watu waliopotoka!

Hawajali kabisa njia zangu!’

11Basi, nilikasirika, nikaapa:

‘Hawataingia mahali pangu pa pumziko!’”

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania