The chat will start when you send the first message.
1Nasema ukweli tupu; nimeungana na Kristo nami sisemi uongo. Dhamiri yangu ikiongozwa na Roho Mtakatifu inanithibitishia jambo hili pia.[#9:1 Taz 2:14-15 ambapo Paulo anaeleza “dhamira” kama sheria iliyoandikwa ndani ya moyo wa binadamu. Hapa Paulo anasema kwamba Roho Mtakatifu anatenda kama mwalimu wake akiongea na dhamiri yake na kuunda mawazo yake ya ndani.; #9:1—11:36 Katika sura hizi za 9-11 Paulo anazungumzia mada ya uhusiano wa taifa la Israeli na mpango wa Mungu wa wokovu. Paulo anafafanua kusitasita kwa Wayahudi kupokea Injili kama sehemu ya mpango mpana na kwamba jambo hilo linakuza si tu upendo na utawala mkuu wa Mungu. Kutokuamini kwao ni jambo la muda tu na hali hiyo itaongoza mwishowe katika wokovu wa watu wa mataifa na pia wa Wayahudi.]
2Nataka kusema hivi: nina huzuni kubwa na maumivu yasiyopimika moyoni mwangu
3kwa ajili ya ndugu zangu walio wa taifa langu! Kama ingekuwa kwa faida yao, ningekuwa radhi kulaaniwa na kutengwa na Kristo.[#9:3 Yaani Wayahudi. Paulo (jina lake la Kiyahudi lilikuwa Saulo) alikuwa Myahudi.]
4Hao ndio watu wa Israeli ambao Mungu aliwateua wawe watoto wake, akawashirikisha utukufu wake; alifanya nao maagano, akawapa sheria yake, imani ya kweli na ahadi zake.[#9:4 Paulo anajenga hoja yake juu ya Mungu alivyowatendea Waisraeli walipotoka Misri wakielekea Kanaani (taz Kut 19:4-6 n.k.). Agano la Mungu na Waisraeli lina sehemu mbili: agano na Abrahamu na wazawa wake (Mwa 12:1-3) na agano lake na Mose mlimani Sinai, agano ambalo lilielezwa katika sheria (Kut 19-20).]
5Wao ni wajukuu wa mababu, naye Kristo, kadiri ya ubinadamu wake, ametoka katika ukoo wao. Mungu atawalaye juu ya yote, na atukuzwe milele! Amina.
6Sisemi kwamba ahadi ya Mungu imebatilika; maana si watu wote wa Israeli ni wateule wa Mungu.
7Wala si wazawa wote wa Abrahamu ni watoto wake wa kweli. Ila, kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Wazawa wake watatokana na Isaka.”
8Ndiyo kusema, si wale waliozaliwa kimaumbile ndio watoto wa Mungu, bali wale waliozaliwa kutokana na ahadi ya Mungu ndio watakaoitwa watoto wake.[#9:8 Yahusu wazawa wa Abrahamu kwa kupitia Ishmaeli ambaye alikuwa mtoto wake Abrahamu na Hagari (taz Gal 4:22-23).]
9Maana ahadi yenyewe ni hii: “Wakati maalumu nitarudi, naye Sara atapata mtoto.”
10Tena si hayo tu, ila pia Rebeka naye alipata mapacha kwa baba mmoja, yaani Isaka, babu yetu.[#9:10 Taz habari za Yakobo na Esau katika Mwa 25:19-34; 27:1-40.]
11Lakini, ili Mungu aonekane kwamba anao uhuru wa kuchagua, hata kabla wale ndugu hawajazaliwa na kabla hawajaweza kupambanua jema na baya,
12Rebeka aliambiwa kwamba yule mtoto wa kwanza atamtumikia yule wa nyuma. Hivyo uchaguzi wa Mungu unategemea jinsi anavyoita mwenyewe, na si matendo ya binadamu.
13Kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: “Yakobo nilimpenda, lakini Esau nilimchukia.”
14Basi, tuseme nini? Je, Mungu amekosa haki? Hata kidogo!
15Maana alimwambia Mose: “Nitamhurumia mtu yeyote ninayetaka kumhurumia; nitamwonea huruma mtu yeyote ninayetaka.”
16Kwa hiyo, yote hutegemea huruma ya Mungu, na si bidii au mapenzi ya mtu.
17Maana Maandiko Matakatifu yasema hivi kwa Farao: “Nilikufanya mfalme ili kwa njia yako, uwezo wangu ujulikane, na jina langu litangazwe popote duniani.”
18Ni wazi basi, kwamba Mungu humhurumia yeyote anayetaka kumhurumia, na akipenda kumfanya mtu awe mkaidi, hufanya hivyo.[#9:18-20 Hapa Paulo anataka kutilia mkazo kwamba Mungu anaweza kufanya apendavyo na kwamba kila kitu kiko chini ya mamlaka yake.]
19Labda utaniuliza: “Ikiwa mambo yako hivyo, Mungu anawezaje kumlaumu mtu? Nani awezaye kuyapinga mapenzi yake?”
20Lakini, ewe binadamu, u nani hata uthubutu kumhoji Mungu? Je, chungu chaweza kumwuliza mfinyanzi wake: “Kwa nini umenitengeneza namna hii?”[#9:20 Vyungu, mabakuli n.k. vilikuwa vyombo vilivyofinyangwa, yaani watu walitumia namna ya udongo kuviunda. Katika shughuli ya kuviunda, mfinyanzi aliweza kurudia mara kwa mara kuunda chombo chake kama hakikutokea alivyotaka. Picha hiyo Paulo anaiona kuwa mwafaka kabisa kuelezea kazi ya Mungu kuhusu viumbe vyake (taz Isa 29:16; 45:9. Taz pia Yer 18:6; Hek 15:7; Sira 33:13).]
21Mfinyanzi anaweza kuutumia udongo apendavyo na kufinyanga vyungu viwili kwa udongo uleule; kimoja kwa matumizi ya heshima, na kingine kwa matumizi ya kawaida.
22Hivyo ndivyo ilivyo kwa Mungu. Alitaka kuonesha ghadhabu yake na kujulisha uwezo wake. Basi, alikuwa na saburi sana, akiwavumilia wale ambao walikuwa lengo la ghadhabu yake, ambao walistahili kuangamizwa.
23Alitaka pia kudhihirisha wingi wa utukufu wake ambao alitumiminia sisi tulio lengo la huruma yake; sisi ambao alikwisha kututayarisha kuupokea utukufu wake.[#9:23 Matumizi ya “utukufu” hapa huenda yanamaanisha kujionesha kwake Mungu pamoja na utukufu wake na kama Mungu mwenye huruma kwa watu wake.]
24Maana sisi ndio hao aliowaita, si kutoka miongoni mwa Wayahudi tu bali pia kutoka kwa watu wa mataifa mengine.
25Maana ndivyo asemavyo katika kitabu cha Hosea:
“Wale waliokuwa ‘Si watu wangu’
nitawaita: ‘Watu wangu!’
Naye ‘Sikupendi’
ataitwa: ‘Mpenzi wangu!’
26Na pale walipoambiwa:
‘Nyinyi si wangu’
hapo wataitwa:
‘Watoto wa Mungu aliye hai.’”
27Naye nabii Isaya, kuhusu Israeli anapaza sauti: “Hata kama wazawa wa Israeli ni wengi kama mchanga wa pwani, ni wachache tu watakaookolewa;[#9:27 Taz Isa 10:22-23 kadiri ya tafsiri ya Septuajinta. Na kuhusu “wachache” taz Rom 11:5 maelezo.]
28maana, Bwana ataitekeleza upesi hukumu yake kamili juu ya ulimwengu wote.”
29Ni kama Isaya alivyosema hapo awali: “Bwana wa majeshi asingalituachia baadhi ya watoto wa Israeli, tungalikwisha kuwa kama Sodoma, tungalikwisha kuwa kama Gomora.”[#9:29 Mungu aliteketeza kabisa miji hii kwa sababu ya dhambi za wakazi wake (taz Mwa 18:16—19:29).]
30Basi tuseme nini? Watu wa mataifa ambao hawakutafuta wafanywe waadilifu, wamejaliwa kuwa waadilifu, kwa njia ya imani,
31hali watu wa Israeli ambao walitafuta sheria ya kuwafanya kuwa waadilifu, hawakuipata.
32Kwa nini? Kwa sababu walitegemea matendo yao badala ya kutegemea imani. Walijikwaa juu ya jiwe la kujikwaa[#9:31-32 Hapa Paulo anasema juu ya Yesu Kristo. Taz pia Marko 12:10; 1Pet 2:6-8.]
33kama yasemavyo Maandiko Matakatifu:
“Tazama, nitaweka huko Siyoni jiwe likwazalo,
mwamba utakaowafanya watu waanguke.
Lakini atakayemwamini hataaibishwa!”