Tobiti 7

Tobiti 7

Nyumbani kwa Ragueli

1Walipowasili mjini Ekbatana, Tobia akamwambia Rafaeli, “Ndugu yangu Azaria, nipeleke mara moja kwa Ragueli.” Malaika akamwongoza kijana nyumbani kwa Ragueli, Wakamkuta Ragueli ameketi kando ya mlango wa uani. Basi wakamsalimia kwanza naye Ragueli akawajibu, “Wasalaam! Karibuni ndugu zangu.” Kisha Ragueli akawaingiza wageni ndani.

2Mara akamwuliza mkewe, Edna, “Hebu ona jinsi kijana huyu anavyofanana na binamu yangu Tobiti!”

3Edna akawauliza walikotoka nao wakasema, “Sisi ni wa kabila la Naftali, lakini sasa tumo uhamishoni mjini Ninewi huko Ashuru.”

4Edna akasema, “Mnamjua ndugu yetu Tobiti?” Wakajibu, “Naam! Tunamjua sana.” Naye akauliza, “Je hajambo?”

5Wakajibu, “Ni mzima, tena hajambo,” Kisha Tobia akaongeza, “Tobiti ni baba yangu.”

6Ragueli aliposikia hivyo, akaruka na kumbusu Tobia huku machozi yanamtoka kwa furaha.

7Halafu akasema, “Mungu akubariki, mwanangu. Baba yako ni mtu mwema na muungwana. Inasikitisha kwamba mtu mnyofu na mkarimu kama yeye amekuwa kipofu!” Kisha akamkumbatia Tobia, na kupangusa machozi.

8Naye mkewe akamlilia Tobiti; hali kadhalika na Sara binti yake.

Basi, Ragueli aliwakaribisha kwa furaha Tobia na Rafaeli, akawachinjia kondoo dume. Wageni walipomaliza kuoga na saa ya chakula ilipowadia, Tobia akamwambia Rafaeli, “Ndugu yangu Azaria! Je, utamwambia Ragueli sasa anipe dada yangu Sara?”

9Ragueli akamwambia Tobia, “Kula na unywe, ufurahi;

10hakuna mtu mwingine aliye na haki ya kumwoa Sara; hakuna mwingine ila wewe. Mimi sina uhuru wa kumtoa kwa mtu mwingine kwa sababu kimila wewe ndiwe jamaa wa karibu zaidi. Lakini ni lazima nikuambie ukweli mwanangu.

11Nimekwisha mwoza kwa wanaume saba mpaka sasa, wote jamaa zangu. Kila mmoja wao alifariki usiku wa harusi, mara alipoingia chumbani kwa bibiarusi. Basi, kwa sasa mwanangu, kula na unywe.”

Tobia akajibu, “Sipendi hata kusikia juu ya kula na kunywa mpaka utakapotoa uamuzi wako juu yangu.”

12Ragueli akajibu, “Haya basi! Nitakupa umwoe kama sheria ya Mose inavyodai. Mungu mwenye huruma amepanga ndoa hii! Basi, mchukue awe mke wako. Toka sasa nyinyi ni mume na mke. Sara ni wako leo na hata milele. Mungu mwenye rehema awalinde salama usiku wa leo, na azidi kuwapenda.”[#7:12 Taz 6:12.]

Sherehe za ndoa

13Kisha, Ragueli akamwita binti yake. Alipoingia ndani, akamshika mkono Sara na kumkabidhi kwa Tobia huku anatamka baraka, “Namkabidhi kwako, kwa mujibu wa sheria ya Mose. Nenda naye salama nyumbani kwa baba yako. Mungu wa mbinguni awajalie safari nzuri katika amani.”[#7:13 Kitendo hiki kinaelezwa kama kitendo cha kidini, kitendo kinacholingana na sheria na pia ni kitendo rasmi.]

14Kisha Ragueli akamgeukia mkewe akamwomba ampe karatasi ya kuandikia. Basi, akaandika hati ya mapatano ya ndoa na hivyo akamtoa binti yake awe mke wa Tobia kwa mujibu wa sheria ya Mose.

15Baada ya hayo wakaanza kula na kunywa.

16Kisha Ragueli alimwita mkewe, akamwambia, “Dada! Tayarisha kile chumba cha pili, halafu umpeleke Sara huko.”

17Basi, Edna akatandika kitanda kama alivyokuwa ameagizwa akampeleka binti yake huko chumbani. Sara akaanza kulia. Lakini mama yake akamfuta machozi akisema,

18“Usiogope binti yangu. Nina hakika Bwana wa mbingu ataigeuza huzuni yako kuwa furaha! Jipe moyo binti yangu!” Kisha Edna akatoka chumbani.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania