Zekaria 1

Zekaria 1

Mungu anawaita watu wake wamrudie

1Mnamo mwezi wa nane wa mwaka wa pili wa utawala wa mfalme Dario wa Persia, neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia nabii Zekaria mwana wa Berekia, mjukuu wa Ido:[#1:1 Huyo alikuwa mfalme wa Persia mnamo miaka ya 522-486 K.K. Mwezi wa nane, mwaka wa pili, ni sawa na Oktoba - Novemba mwaka 520 (muda mfupi baada ya ujumbe wa kinabii wa nabii Hagai - taz Hag 1:1 maelezo).; #1:1 Jina hili katika Kiebrania lina maana ya Mwenyezi-Mungu hukumbuka. Zekaria huenda alikuwa wa familia ya kikuhani ambayo ilirejea Yerusalemu mwishoni mwa uhamisho wa Waisraeli kule Babuloni. Hapa anatajwa kama mwanawe Berekia lakini mahali pengine (Neh 12:16) anatajwa kama mwanawe Ido.; #1:1 Katika Isa 8:2 tuna “Zekaria mwana wa Yeberekia” ambaye bila shaka ni tofauti na huyu.; #1:1—8:23 Sehemu ya kwanza ya kitabu cha Zekaria ina mfululizo wa maono nane ya kinabii. Kwa maono hayo nabii anatangaza kurekebishwa kwa jumuiya ya Wayahudi baada ya matatizo ya uhamisho kule Babuloni na mzozo uliozuka wakati wa kurudi kutoka huko.]

2“Mimi Mwenyezi-Mungu nilichukizwa sana na wazee wenu.

3Basi, waambie watu kuwa mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nasema hivi: Nirudieni, nami nitawarudieni nyinyi.

4Msiwe kama wazee wenu ambao manabii waliwaambia waachane na mienendo yao miovu na matendo yao mabaya, lakini wao hawakunisikiliza wala hawakunitii mimi Mwenyezi-Mungu.[#1:4 Yahusu manabii waliohubiri kabla ya Waisraeli kupelekwa uhamishoni mnamo mwaka 586. Manabii hao walikwisha kufa, lakini mahubiri yao yalikuwa bado yana nguvu. Rejea Isa 45:22; Yer 18:11; 25:5; 35:15; Ezek 33:11.]

5Wazee wenu, wako wapi? Na manabii, je, wanaishi milele?

6Je, wazee wenu hawakupata adhabu kwa sababu ya kukataa maagizo yangu na amri nilizowapa kwa njia ya watumishi wangu manabii? Wakati huo, wao walitubu na kusema kuwa mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, nilikusudia kuwatenda kulingana na mienendo yao na matendo yao, na kweli ndivyo nilivyowatenda.”

Maono ya kwanza: Farasi

7Mnamo siku ya ishirini na nne ya mwezi wa kumi na moja, yaani mwezi wa Shebati, mwaka wa pili wa utawala wa Dario, neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia mimi nabii Zekaria mwana wa Berekia, mjukuu wa Ido, kama ifuatavyo:[#1:7 Yapata miezi mitatu baada ya ujumbe wa kwanza wa Zekaria (1:1).; #1:7-17 Kwa simulizi la maono haya nabii anatangaza kwamba nyakati mpya zinaanza, na ishara ya wakati huo mpya ni urekebishaji mpya wa Yerusalemu na hekalu (Zek 1:16-17).]

8Wakati wa usiku, nilimwona malaika amepanda farasi mwekundu. Malaika huyo alikuwa amesimama bondeni, katikati ya miti ya mihadasi. Nyuma yake kulikuwa na farasi wengine wekundu, wa kijivujivu na weupe.[#1:8 Makala ya Kiebrania inasema “mtu” (mwanamume), ambapo yawezekana kuwa ni “malaika” wa Mwenyezi-Mungu, na ambaye anatajwa kama “malaika” katika aya ya 11.; #1:8 Miti ya mihadasi ilikuwa daima na majani mabichi wakati wote na ilichukuliwa kuwa ni mfano wa rutuba. Kwa hiyo hapa panaashiria nyakati bora za rutuba kwa Waisraeli.; #1:8 Wafafanuzi wengine wanafikiri kwamba kwa rangi za hao farasi hapa, mwandishi anatumia lugha ya mfano kuhusu malaika ambao hukagua ulimwengu (aya 10). Tafsiri ya Kigiriki hapa, ina pia farasi wanne ambao ni weusi. Rejea Zek 6:2-3; Ufu 6:2-8. Idadi ya farasi wanaohusika si dhahiri; katika sura ya 6:2-3, tuna magari manne ya kukokotwa (mikokoteni) ambayo inakokotwa na kundi la farasi. Katika Ufu 6:2-8, mahali ambapo wazo hili linagusiwa, kuna farasi wanne (taz Ufu 6:2-8).]

9Basi, nikamwuliza, “Bwana, Farasi hawa wanamaanisha nini?” Malaika huyo aliyeongea nami akaniambia, “Nitakuonesha hao farasi wanamaanisha nini.

10Hawa ndio waliotumwa na Mwenyezi-Mungu kuikagua dunia.”

11Hao farasi wakamwambia huyo malaika wa Mwenyezi-Mungu aliyekuwa amesimama katikati ya miti ya mihadasi, “Tumeikagua dunia yote, nayo kweli imetulia.”[#1:11 Tafsiri hii inaonesha kwamba wanaosema ni hao farasi. Kuna wataalamu wengine ambao wanafikiri kwamba wanaosema ni “wapandafarasi” wanaohusika hapa. Lakini kama ilivyo katika lugha na maandishi ya maono, mtazamo wa tafsiri hii ni wa kupendelewa kulingana na mazingira ya maandishi. Hata farasi wanaongea!]

12Ndipo huyo malaika wa Mwenyezi-Mungu akasema, “Ee Mwenyezi-Mungu wa majeshi, kwa muda gani utaendelea kutokuwa na huruma juu ya mji wa Yerusalemu na miji ya nchi ya Yuda ambayo umeikasirikia kwa muda wa miaka sabini?”[#1:12 Msemo wa kukata tamaa na wa kilio, kumwomba Mungu achukue hatua ya kuwasaidia watu (Zab 6:3; 13:1; 74:10; 80:4; 94:4). Na, kuhusu “miaka sabini” itakumbukwa kwamba idadi hiyo ni sawa na muda ule wa uhamisho kule Babuloni (rejea Yer 25:11; 29:10, na taz Zek 7:5).]

13Mwenyezi-Mungu akampa huyo malaika jibu jema na lenye matumaini.

14Basi, huyo malaika akaniambia, “Unapaswa kutangaza kwa sauti kwamba Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: ‘Moyo wangu umejaa upendo kwa mji wa Yerusalemu, naam, kwa mlima Siyoni.

15Walakini nimechukizwa sana na mataifa ambayo yanastarehe. Kweli niliwakasirikia Waisraeli kidogo, lakini mataifa hayo yaliwaongezea maafa.

16Kwa hiyo, nasema mimi Mwenyezi-Mungu, naurudia mji wa Yerusalemu kwa huruma; humo itajengwa nyumba yangu, na ujenzi mpya wa mji utaanza.’”

17Kisha malaika huyo akaniambia nitangaze ujumbe huu mwingine: “Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: ‘Miji yangu itafurika tena fanaka. Mimi Mwenyezi-Mungu nitaufariji tena mji wa Siyoni; nitauteua mji wa Yerusalemu kuwa wangu.’”

Maono ya pili: Pembe

18Katika maono mengine, niliona pembe nne.

19Nami nikamwuliza yule malaika aliyezungumza nami, “Pembe hizi zinamaanisha nini?” Yeye akanijibu, “Pembe hizi zinamaanisha yale mataifa ambayo yaliwatawanya watu wa Yuda, Israeli na Yerusalemu.”

20Kisha, Mwenyezi-Mungu akanionesha wafuachuma wanne.[#1:20 Hawa wanawakilisha wale ambao ni wajumbe wa Mungu wanaopelekwa kuharibu maadui wa watu wake. Rejea Hag 2:21-22.]

21Nami nikauliza, “Watu hawa wanakuja kufanya nini?” Yeye akanijibu, “Watu hawa wamekuja kuyatisha na kuyaangamiza yale mataifa yenye nguvu ambayo yaliishambulia nchi ya Yuda na kuwatawanya watu wake.”

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania