The chat will start when you send the first message.
1Kwa hiyo, kwa kuwa Kristo aliteswa katika mwili wake, ninyi nanyi jivikeni nia hiyo hiyo kwa maana mtu aliyekwisha kuteswa katika mwili ameachana na dhambi.
2Kwa hivyo, haishi maisha yake yaliyobaki hapa duniani ili kutimiza tamaa mbaya za wanadamu, bali anaishi ili kutimiza mapenzi ya Mungu.
3Kwa maana wakati uliopita, mmetumia muda mwingi mkifanya yale wapagani hupenda kutenda: wakiishi katika uasherati, tamaa mbaya, ulevi, karamu za ulafi, vileo, ngoma mbaya, na ibada chukizo za sanamu.
4Wao hushangaa kwamba ninyi hamjiingizi pamoja nao katika maisha yao ya uovu uliopita kiasi, nao huwatukana ninyi.
5Lakini itawapasa wao kutoa maelezo kwake yeye aliye tayari kuwahukumu walio hai na waliokufa.
6Kwa kuwa hii ndiyo sababu Injili ilihubiriwa hata kwa wale waliokufa, ili wahukumiwe sawasawa na wanadamu wengine katika mwili, lakini katika roho waishi kulingana na Mungu aishivyo.
7Mwisho wa mambo yote umekaribia. Kwa hiyo kuweni na tahadhari, mkiwa na akili tulivu na kujidhibiti, mkikesha katika kuomba.
8Zaidi ya yote, dumuni katika upendo kwa maana upendo husitiri wingi wa dhambi.
9Kuweni wakarimu kila mtu na mwenzake pasipo manungʼuniko.
10Kila mmoja na atumie kipawa chochote alichopewa kuwahudumia wengine, kama mawakili waaminifu wa neema mbalimbali za Mungu.
11Yeyote asemaye hana budi kusema kama mtu asemaye maneno ya Mungu mwenyewe. Yeyote anayehudumu hana budi kuhudumu kwa nguvu zile anazopewa na Mungu, ili Mungu apate kutukuzwa katika mambo yote kupitia kwa Yesu Kristo. Utukufu na uweza una yeye milele na milele. Amen.
12Wapendwa, msione ajabu kwa yale mateso yanayotukia miongoni mwenu, kana kwamba ni kitu kigeni kinachowapata.
13Bali furahini kuwa mnashiriki katika mateso ya Kristo, ili mpate kufurahi zaidi wakati utukufu wake utakapofunuliwa.
14Mkitukanwa kwa ajili ya jina la Kristo, mmebarikiwa, kwa sababu Roho wa utukufu na wa Mungu anakaa juu yenu.
15Lakini asiwepo mtu yeyote miongoni mwenu anayeteswa kwa kuwa ni muuaji, au mwizi, au mhalifu wa aina yoyote, au anayejishughulisha na mambo ya watu wengine.
16Lakini ukiteseka kwa kuwa Mkristo, usihesabu jambo hilo kuwa ni aibu, bali mtukuze Mungu kwa sababu umeitwa kwa jina hilo.
17Kwa maana wakati umewadia wa hukumu kuanzia katika nyumba ya Mungu. Basi ikianzia kwetu sisi, mwisho wa hao wasiotii Injili ya Mungu utakuwaje?
18Basi,
“Ikiwa ni vigumu kwa mwenye haki kuokoka,
itakuwaje kwa mtu asiyemcha Mungu na mwenye dhambi?”
19Kwa hiyo, wale wanaoteswa kulingana na mapenzi ya Mungu, wajikabidhi kwa Muumba wao aliye mwaminifu, huku wakizidi kutenda mema.