The chat will start when you send the first message.
1Basi huko Samaria walikuwepo wana sabini wa nyumba ya Ahabu. Kwa hiyo Yehu akaandika barua na kuzituma Samaria: kwa maafisa wa Yezreeli, kwa wazee, na kwa walezi wa watoto wa Ahabu. Akasema,
2“Mara tu barua hii itakapokufikia, kwa kuwa wana wa bwana wako wapo pamoja nawe, nawe una magari ya vita na farasi, mji wenye ngome na silaha,
3mchague mwenye uwezo zaidi kati ya wana wa bwana wako, na umweke kwenye kiti cha utawala cha baba yake. Kisha upigane kwa ajili ya nyumba ya bwana wako.”
4Lakini wakaogopa sana na kusema, “Ikiwa wafalme wawili hawakuweza kupambana na Yehu, sisi tutawezaje?”
5Basi msimamizi wa jumba la mfalme, mtawala wa mji, na wazee na walezi wakatuma ujumbe huu kwa Yehu: “Sisi tu watumishi wako, na tutafanya kila kitu utakachosema. Hatutamteuwa mtu yeyote kuwa mfalme. Wewe fanya uonalo kuwa ni bora.”
6Kisha Yehu akawaandikia barua ya pili, akisema, “Ikiwa ninyi mko upande wangu na mtanitii mimi, twaeni vichwa vya wana wa bwana wenu, na mnijie huku Yezreeli kesho wakati kama huu.”
Wakati huo wana sabini wa mfalme walikuwa wakiishi pamoja na viongozi wa mji wa Samaria, waliokuwa wakiwalea.
7Hiyo barua ilipowafikia, watu hawa wakawachukua wale wana sabini wa mfalme na kuwachinja wote. Wakaweka vichwa vyao ndani ya makapu na kumpelekea Yehu huko Yezreeli.
8Mjumbe alipofika, akamwambia Yehu, “Wameleta vichwa vya wana wa mfalme.”
Ndipo Yehu akaagiza, “Viwekeni malundo mawili katika ingilio la lango la mji hadi asubuhi.”
9Kesho yake asubuhi, Yehu akatoka nje. Akasimama mbele ya watu wote na akasema, “Hamna hatia. Ni mimi niliyepanga njama dhidi ya bwana wangu na kumuua, lakini ni nani aliyewaua wote hawa?
10Fahamuni basi kwamba, hakuna neno ambalo Bwana amesema dhidi ya nyumba ya Ahabu ambalo halitatimia. Bwana amefanya lile aliloahidi kupitia mtumishi wake Eliya.”
11Hivyo Yehu akaua kila mtu huko Yezreeli aliyekuwa amebaki wa nyumba ya Ahabu, ikiwa ni pamoja na wakuu wake, rafiki zake wa karibu, na makuhani wake. Hakuacha yeyote anusurike.
12Kisha Yehu akaondoka kuelekea Samaria. Alipokuwa njiani karibu na nyumba ya kukatia manyoya ya kondoo, yaani Beth-Ekedi ya wachunga kondoo,
13Yehu akakutana na watu wa jamaa ya Ahazia mfalme wa Yuda, akauliza, “Ninyi ni nani?”
Wao wakasema, “Sisi ni jamaa ya Ahazia, nasi tumeshuka kuwasalimu jamaa ya mfalme na ya mama malkia.”
14Yehu akaagiza, “Wakamateni wakiwa hai!” Kwa hiyo wakawachukua wakiwa hai, watu arobaini na wawili, na kuwachinja kando ya kisima cha Beth-Ekedi. Hakuacha yeyote anusurike.
15Baada ya kuondoka hapo, alimkuta Yehonadabu mwana wa Rekabu, aliyekuwa akienda kumlaki. Yehu akamsalimu na kusema, “Je, moyo wako ni mnyofu kwangu kama moyo wangu ulivyo kwako?”
Yehonadabu akajibu, “Ndiyo.”
Yehu akasema, “Kama ndivyo, nipe mkono wako.” Yeye akampa mkono, naye Yehu akampandisha kwenye gari lake la vita.
16Yehu akasema, “Twende pamoja ukaone wivu wangu kwa ajili ya Bwana .” Hivyo wakasafiri pamoja kwenye gari lake la vita.
17Yehu alipofika Samaria, akawaua wale wote waliokuwa wamesalia wa jamaa ya Ahabu, akawaangamiza, sawasawa na neno la Bwana alilosema kupitia Eliya.
18Kisha Yehu akawaleta watu wote pamoja na kuwaambia, “Ahabu alimtumikia Baali kidogo. Lakini Yehu atamtumikia zaidi.
19Sasa waiteni manabii wote wa Baali, watumishi wake wote na makuhani wake wote. Hakikisheni kwamba hakuna hata mmoja atakayekosekana, kwa sababu ninaenda kutoa kafara kubwa sana kwa Baali. Yeyote atakayeshindwa kuja hataendelea kuishi.” Lakini Yehu alifanya hivyo kwa hila ili apate kuwaangamiza watumishi wote wa Baali.
20Yehu akasema, “Itisheni kusanyiko kwa heshima ya Baali.” Basi wakatangaza jambo hilo.
21Kisha Yehu akapeleka ujumbe katika Israeli yote, nao watumishi wote wa Baali wakaja, hakuna hata mmoja ambaye hakufika. Wakasongamana ndani ya hekalu la Baali hadi likajaa tangu mlango hadi mwisho wake.
22Naye Yehu akamwambia yule aliyekuwa mtunza chumba cha mavazi, “Leta majoho kwa ajili ya watumishi wote wa Baali.” Basi akawaletea majoho.
23Kisha Yehu na Yehonadabu mwana wa Rekabu wakaingia ndani ya hekalu la Baali. Yehu akawaambia watumishi wa Baali, “Tazameni kila mahali mhakikishe kwamba hakuna hata mtumishi mmoja wa Bwana aliye hapa pamoja nanyi, ila ni watumishi wa Baali tu.”
24Kwa hiyo wakaingia ndani ili kutoa kafara na sadaka ya kuteketezwa. Wakati huu, Yehu alikuwa amewaweka watu wake themanini akiwa amewapa onyo kwamba, “Ikiwa mmoja wenu atamwachia mtu yeyote ninayemweka mikononi mwenu atoroke, itakuwa uhai wako kwa uhai wake.”
25Mara baada ya Yehu kutoa sadaka ya kuteketezwa, akawaamuru walinzi na maafisa: “Ingieni ndani, waueni; asitoroke hata mmoja.” Basi wakawakatakata kwa upanga. Walinzi na maafisa wakazitupa zile maiti nje, kisha wakaingia mahali pa ndani pa ibada katika hekalu la Baali.
26Wakaileta ile nguzo ya kuabudiwa nje ya hekalu la Baali, na wakaichoma moto.
27Wakabomoa ile nguzo ya kuabudiwa ya Baali pamoja na hekalu la Baali, nao watu wakapafanya kuwa choo hadi leo.
28Kwa hiyo Yehu akaangamiza kuabudiwa kwa Baali katika Israeli.
29Hata hivyo, Yehu hakuziacha dhambi za Yeroboamu mwana wa Nebati, ambazo alikuwa amesababisha Israeli kuzitenda, yaani kuabudu ndama za dhahabu huko Betheli ya Dani.
30Bwana akamwambia Yehu, “Kwa kuwa umefanya vyema kwa kutimiza yaliyo sawa machoni pangu, na umetenda kwa nyumba ya Ahabu yale yote niliyokuwa nimekusudia kutenda, wazao wako wataketi kwenye kiti cha utawala cha Israeli hadi kizazi cha nne.”
31Lakini Yehu hakuwa mwangalifu kushika sheria za Bwana , Mungu wa Israeli, kwa moyo wake wote. Hakuziacha dhambi za Yeroboamu, ambazo alikuwa amesababisha Israeli kuzitenda.
32Katika siku hizo, Bwana akaanza kupunguza ukubwa wa Israeli. Hazaeli akawashinda Waisraeli sehemu zote za nchi yao
33mashariki mwa Yordani, katika nchi yote ya Gileadi (eneo la Gadi, Reubeni na Manase), kutoka Aroeri karibu na Bonde la Arnoni kupitia Gileadi hadi Bashani.
34Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Yehu, yote aliyofanya na mafanikio yake yote, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli?
35Yehu akalala na baba zake, akazikwa huko Samaria. Naye Yehoahazi mwanawe akawa mfalme baada yake.
36Muda Yehu aliotawala Israeli huko Samaria ulikuwa miaka ishirini na nane.