2 Wafalme 12

2 Wafalme 12

Yoashi akarabati Hekalu

1Katika mwaka wa saba wa utawala wa Yehu, Yoashi alianza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka arobaini. Mama yake aliitwa Sibia, kutoka Beer-Sheba.

2Yoashi akafanya yaliyo mema machoni pa Bwana miaka yote ambayo Yehoyada kuhani alikuwa akimwelekeza.

3Hata hivyo mahali pa juu pa kuabudia hapakuondolewa. Watu waliendelea kutoa kafara na kufukiza uvumba huko.

4Yoashi akawaambia makuhani, “Kusanyeni fedha zote zitakazoletwa kama sadaka takatifu kwenye Hekalu la Bwana , yaani fedha zilizokusanywa watu walipohesabiwa, fedha zilizopokelewa kutokana na nadhiri za watu binafsi, na fedha zilizoletwa kwa hiari hekaluni.

5Kila kuhani na apokee fedha kutoka kwa mmoja wa watunza hazina, nazo zitumike kukarabati uharibifu wowote unaoonekana katika Hekalu.”

6Lakini ikawa kufikia mwaka wa ishirini na tatu wa utawala wake Mfalme Yoashi, makuhani walikuwa bado hawajalikarabati Hekalu.

7Kwa hiyo Mfalme Yoashi akamwita Yehoyada kuhani na makuhani wengine, akawauliza, “Kwa nini hamtengenezi uharibifu uliofanyika hekaluni? Msichukue fedha zaidi kutoka kwa watunza hazina wenu kwa ajili ya matumizi yenu, lakini kuanzia sasa ni lazima fedha yote itumike kwa ajili ya kukarabati Hekalu.”

8Makuhani wakakubali kuwa hawatakusanya tena fedha kutoka kwa watu na kwamba hawatakarabati Hekalu wenyewe.

9Yehoyada kuhani akachukua kisanduku na akatoboa tundu kwenye kifuniko chake. Akakiweka kando ya madhabahu upande wa kulia unapoingia hekaluni mwa Bwana . Makuhani waliolinda ingilio wakaweka ndani ya kisanduku fedha zote ambazo zililetwa katika Hekalu la Bwana .

10Kila mara walipoona kuwa kuna kiasi kikubwa cha fedha ndani ya kisanduku, mwandishi wa mfalme na kuhani mkuu walikuja, wakazihesabu fedha hizo zilizoletwa katika Hekalu la Bwana , na kuziweka katika mifuko.

11Walipothibitisha kiasi cha hizo fedha, waliwapa watu walioteuliwa kusimamia kazi katika Hekalu. Kwa fedha hizo, wakawalipa wale watu waliofanya kazi katika Hekalu la Bwana : maseremala na wajenzi,

12waashi na wakata mawe. Walinunua mbao na mawe ya kuchongwa kwa ajili ya ukarabati wa Hekalu la Bwana , na kulipia gharama nyingine zote za kulitengeneza.

13Fedha zilizoletwa kwenye Hekalu hazikutumiwa kutengenezea masinia ya fedha, mikasi ya kusawazishia tambi, mabakuli ya kunyunyizia, tarumbeta wala vyombo vingine vyovyote vya dhahabu au fedha kwa ajili ya Hekalu la Bwana ;

14zililipwa kwa wafanyakazi, ambao walizitumia kwa kukarabati Hekalu.

15Wao hawakudai hesabu ya fedha kutoka kwa wale waliowapa ili kuwalipa wafanyakazi, kwa sababu walifanya kwa uaminifu wote.

16Fedha zilizopatikana kutokana na sadaka za hatia na sadaka za dhambi hazikuletwa katika Hekalu la Bwana ; zilikuwa mali ya makuhani.

17Basi Hazaeli mfalme wa Aramu akapanda kuishambulia Gathi, akaiteka. Kisha akageuka ili kuishambulia Yerusalemu.

18Lakini Yoashi mfalme wa Yuda akavichukua vyombo vyote vitakatifu vilivyowekwa wakfu na baba zake, yaani Yehoshafati, Yehoramu na Ahazia, wafalme wa Yuda, na vyombo vyake vyote ambavyo alikuwa ameviweka wakfu, pamoja na dhahabu yote iliyokuwa katika hazina za Hekalu la Bwana na katika jumba la kifalme; akazipeleka kwa Hazaeli mfalme wa Aramu, ambaye hatimaye aliondoka Yerusalemu.

19Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Yoashi na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda?

20Maafisa wake wakapanga njama dhidi yake, nao wakamuua Yoashi huko Beth-Milo, kwenye barabara inayoteremka kuelekea Sila.

21Maafisa waliomuua walikuwa Yozabadi mwana wa Shimeathi, na Yehozabadi mwana wa Shomeri. Akafa na akazikwa na baba zake katika Mji wa Daudi. Naye Amazia mwanawe akawa mfalme baada yake.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.