The chat will start when you send the first message.
1Wana wa manabii wakamwambia Elisha, “Tazama, mahali hapa tunapokutana nawe ni padogo sana kwetu.
2Twendeni Yordani, ambapo kila mmoja wetu anaweza kupata nguzo moja, nasi tujenge huko mahali petu pa kuishi.”
Naye akawaambia, “Nendeni.”
3Kisha mmoja wao akasema, “Je, tafadhali, huwezi kufuatana na watumishi wako?”
Elisha akajibu, “Nitakuja.”
4Naye akaenda pamoja nao.
Basi wakaenda Yordani, nao wakaanza kukata miti.
5Mmoja wao alipokuwa anakata mti, shoka lilitumbukia kwenye maji. Akalia, “Ee bwana wangu, shoka lilikuwa la kuazima!”
6Mtu wa Mungu akauliza, “Je, liliangukia wapi?” Alipomwonesha mahali penyewe, Elisha akakata kijiti na kukitupa mahali pale, nalo shoka likaelea.
7Akasema, “Lichukue.” Kisha yule mtu akanyoosha mkono wake, akalichukua.
8Wakati huo mfalme wa Aramu alikuwa akipigana vita na Israeli. Baada ya kukubaliana na maafisa wake, akasema, “Nitapiga kambi yangu mahali fulani na fulani.”
9Mtu wa Mungu akatuma ujumbe kwa mfalme wa Israeli: “Jihadhari usije ukapita mahali pale, kwa sababu Waaramu wanashuka huko.”
10Kwa hiyo mfalme wa Israeli akatuma neno la tahadhari mahali pale alikokuwa ameelekezwa na mtu wa Mungu. Mara kwa mara Elisha alimwonya mfalme kwamba watu wawe macho kwenye maeneo kama hayo.
11Hili lilimfadhaisha sana mfalme wa Aramu. Akawaita maafisa wake, akawauliza, “Je, hamtaniambia ni nani miongoni mwenu aliye upande wa mfalme wa Israeli?”
12Mmoja wa maafisa wake akasema, “Mfalme bwana wangu, hakuna hata mmoja wetu. Lakini Elisha, yule nabii aliye Israeli, humwambia mfalme wa Israeli hata yale maneno unayozungumza katika chumba chako cha kulala.”
13Mfalme akaagiza akisema, “Nendeni, mkatafute aliko, ili niweze kutuma watu kumkamata.” Taarifa ikarudi kwamba, “Yuko Dothani.”
14Ndipo akatuma farasi na magari ya vita na jeshi lenye nguvu huko. Walienda usiku na kuuzunguka mji.
15Kesho yake asubuhi na mapema, mtumishi wa mtu wa Mungu alipoamka na kutoka nje, jeshi, pamoja na farasi na magari ya vita, likawa limeuzunguka mji. Mtumishi wake akasema, “Ole wetu, bwana wangu! Tutafanya nini?”
16Nabii akajibu, “Usiogope. Wale walio pamoja nasi ni wengi kuliko wale walio pamoja nao.”
17Kisha Elisha akaomba, “Ee Bwana , mfumbue macho huyu mtumishi ili apate kuona.” Ndipo Bwana akayafumbua macho ya yule mtumishi, naye akatazama na kuona vilima vimejaa farasi na magari ya vita yaliyowaka moto yamemzunguka Elisha pande zote.
18Adui waliposhuka kumwelekea, Elisha akamwomba Bwana : “Wapige watu hawa kwa upofu.” Basi Mungu akawapiga kwa upofu, kama Elisha alivyoomba.
19Elisha akawaambia, “Hii sio njia yenyewe, na huu sio huo mji. Nifuateni mimi, nami nitawapeleka kwa huyo mtu mnayemtafuta.” Naye akawapeleka Samaria.
20Baada ya kuingia mjini, Elisha akasema, “Bwana , yafungue macho ya watu hawa ili wapate kuona.” Ndipo Bwana akayafungua macho yao, na walipotazama, kumbe hapo ndipo walipojikuta, ndani ya Samaria.
21Wakati mfalme wa Israeli aliwaona, akamuuliza Elisha, “Je, baba yangu, niwaue?”
22Naye akajibu, “Usiwaue. Je, utawaua watu uliowateka kwa upanga wako mwenyewe na upinde wako? Wape chakula na maji ili wapate kula na kunywa, na kisha wamrudie bwana wao.”
23Basi akawaandalia karamu kubwa, na baada ya kula na kunywa, akawaaga nao wakarudi kwa bwana wao. Hivyo, vikosi kutoka Aramu vikakoma kuvamia nchi ya Israeli.
24Baada ya kitambo kidogo, Ben-Hadadi mfalme wa Aramu akaandaa jeshi lake lote akapanda kwenda kuizingira Samaria.
25Kukawa na njaa kuu katika mji. Samaria ilizingirwa kwa muda mrefu, kiasi kwamba kichwa cha punda kiliuzwa kwa shekeli themanini za fedha, na robo ya kibaba cha mavi ya njiwa kiliuzwa kwa shekeli tano za fedha.[#6:25 Shekeli 80 za fedha ni sawa na kilo moja.; #6:25 Robo ya kibaba ni sawa na lita 0.3.; #6:25 Shekeli 5 ni sawa na gramu 55.]
26Mfalme wa Israeli alipokuwa anapita juu ya ukuta, mwanamke mmoja akamlilia, “Bwana wangu mfalme, nisaidie!”
27Mfalme akajibu, “Ikiwa Bwana hakusaidii, nitakutolea wapi msaada? Je, ni kwenye sakafu ya kupuria? Au ni kwenye shinikizo la kukamulia zabibu?”
28Kisha akamuuliza, “Kwani kuna nini?”
Yule mwanamke akamjibu, “Huyu mwanamke aliniambia, ‘Mtoe mwanao ili tupate kumla leo, na kesho tutamla mwanangu.’
29Basi tukampika mwanangu na kumla. Siku iliyofuata nikamwambia, ‘Mtoe mwanao ili tupate kumla.’ Lakini akawa amemficha.”
30Mfalme aliposikia maneno ya yule mwanamke, akararua mavazi yake. Naye alipoendelea kutembea ukutani, watu wakamtazama, na ndani ya mavazi yake alikuwa amevaa gunia mwilini mwake.
31Akasema, “Mungu na aniadhibu vikali zaidi ikiwa kichwa cha Elisha mwana wa Shafati kitabaki juu ya mabega yake leo!”
32Wakati huu, Elisha alikuwa ameketi ndani ya nyumba yake, akiwa pamoja na wazee. Mfalme akatuma mjumbe kumtangulia, lakini kabla hajafika, Elisha akawaambia wale wazee, “Hammwoni huyu muuaji jinsi anavyotuma mtu kukata kichwa changu? Tazama, wakati mjumbe huyo atakapofika, fungeni mlango na mzuieni asiingie. Je, vishindo vya nyayo za bwana wake haviko nyuma yake?”
33Alipokuwa angali bado anazungumza nao, mjumbe akamfikia. Naye mfalme akasema, “Maafa haya yanatoka kwa Bwana . Kwa nini niendelee kumngoja Bwana zaidi?”