2 Wafalme 7

2 Wafalme 7

1Elisha akasema, “Sikiliza neno la Bwana . Hivi ndivyo asemavyo Bwana : Wakati kama huu kesho, kipimo kimoja cha unga mzuri kitauzwa kwa shekeli moja ya fedha, na vibaba viwili vya shayiri kwa shekeli moja ya fedha katika lango la Samaria.”[#7:1 Kipimo kimoja cha unga ni sawa na kilo 3.; #7:1 Shekeli moja ni sawa na gramu 11.]

2Yule afisa ambaye mfalme alikuwa anauegemea mkono wake akamwambia yule mtu wa Mungu, “Tazama, hata kama Bwana atafungua madirisha ya mbinguni, je, jambo hili litawezekana?”

Elisha akajibu, “Utaona kwa macho yako mwenyewe, lakini wewe hutakula chochote kati ya hivyo!”

Mwisho wa kuzingirwa

3Basi kulikuwa na watu wanne wenye ukoma katika ingilio la lango la mji. Wakaambiana, “Kwa nini tukae hapa hadi tufe?

4Tukisema, ‘Tutaingia mjini,’ mjini kuna njaa, nasi tutakufa humo. Tukikaa hapa, tutakufa. Kwa hiyo twende kambi ya Waaramu, tujisalimishe. Wakituacha hai, tutaishi; wakituua, basi na tufe.”

5Wakati wa mapambazuko, wakaondoka na kwenda kwenye kambi ya Waaramu. Walipofika mwanzo wa kambi, hapakuwa na mtu,

6kwa kuwa Bwana alilifanya jeshi la Waaramu lisikie sauti kama ya magari ya vita, farasi na jeshi kubwa, kiasi kwamba waliambiana, “Tazama, mfalme wa Israeli ameajiri mfalme wa Wahiti na mfalme wa Wamisri kuja kutushambulia sisi!”

7Kwa hiyo wakaondoka na kukimbia wakati wa giza la jioni na kuacha mahema yao, farasi wao na punda wao. Wakakimbia kuokoa maisha yao na kuacha kila kitu ndani ya kambi kama kilivyokuwa.

8Wale watu wenye ukoma walipofika mwanzoni mwa kambi, wakaingia kwenye mojawapo ya mahema. Wakala na kunywa, na kuchukua fedha, dhahabu na nguo, wakaenda kuvificha. Wakarudi na kuingia katika hema lingine, na kuchukua baadhi ya vitu kutoka ndani yake na kuvificha pia.

9Kisha wakaambiana, “Hili tunalolifanya sio jema. Hii ni siku ya habari njema, nasi tunakaa kimya. Tukisubiri hadi mapambazuko, maafa yatatupata. Twendeni mara moja tukatoe habari hizi katika jumba la mfalme.”

10Hivyo wakaenda mjini na kuwaita walinzi wa langoni, wakawaambia, “Tulienda katika kambi ya Waaramu lakini hapakuwa na mtu huko, hata sauti ya mtu yeyote, ila farasi na punda waliofungwa, na mahema yaliyoachwa kama yalivyokuwa.”

11Walinzi wa langoni wakatangaza habari ile kwa sauti kuu, na taarifa hii ikatolewa ndani ya jumba la mfalme.

12Mfalme akaamka usiku na kuwaambia maafisa wake, “Nitawaambia kile Waaramu walichotufanyia. Wanajua kwamba tuna njaa, hivyo wameacha kambi yao ili kujificha mashambani, wakifikiri, ‘Kwa hakika watatoka nje ya mji, nasi tutawakamata wakiwa hai na kuingia ndani ya mji.’ ”

13Mmoja wa maafisa wake akajibu, “Waamuru watu wachache wakawachukue farasi watano kati ya wale waliobaki katika mji. Hatima yao itakuwa kama ya Waisraeli wote walio hapa. Watakuwa tu kama Waisraeli hawa ambao wanangoja kifo. Hivyo tuwatumeni wajue kumetendeka nini.”

14Ndipo wakachagua magari mawili ya vita pamoja na farasi wake, naye mfalme akawatuma wafuatilie jeshi la Waaramu. Akawaamuru waendeshaji akisema, “Nendeni mkaone ni nini kilichotokea.”

15Wakawafuatia hadi Yordani, nao wakakuta barabara yote ikiwa imetapakaa mavazi na vyombo Waaramu walivyokuwa wamevitupa walipokuwa wakitoroka. Basi wale wajumbe wakarudi na kutoa taarifa kwa mfalme.

16Kisha watu wakatoka na kuteka nyara kambi ya Waaramu. Kwa hiyo kipimo cha unga mzuri kikauzwa kwa shekeli, na vipimo viwili vya shayiri kwa shekeli, kama vile Bwana alivyokuwa amesema.

17Basi mfalme alikuwa amemweka yule afisa ambaye mfalme alikuwa anauegemea mkono wake awe msimamizi wa lango. Nao watu wakamkanyaga walipoingia langoni, naye akafa, kama vile mtu wa Mungu alivyokuwa ametangulia kusema wakati mfalme alipofika nyumbani mwake.

18Ikatokea kama vile mtu wa Mungu alivyokuwa amemwambia mfalme: “Wakati kama huu kesho, kipimo kimoja cha unga mzuri kitauzwa kwa shekeli moja ya fedha, na vibaba viwili vya shayiri kwa shekeli moja ya fedha katika lango la Samaria.”

19Yule afisa alikuwa amemwambia yule mtu wa Mungu, “Tazama, hata kama Bwana atafungua madirisha ya mbinguni, je, jambo hili litawezekana?” Naye yule mtu wa Mungu alikuwa amemjibu, “Utaona kwa macho yako mwenyewe, lakini wewe hutakula chochote kati ya hivyo!”

20Ndivyo hasa ilivyotokea kwake, kwa kuwa watu walimkanyaga langoni, naye akafa.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.