The chat will start when you send the first message.
1Tena Daudi akakusanya vijana wenye uwezo wote wa Israeli: watu elfu thelathini.
2Yeye na watu wake wote wakatoka Baala ya Yuda kulipandisha Sanduku la Mungu kutoka huko, linaloitwa kwa Jina, naam, jina la Bwana wa majeshi, anayeketi kwenye kiti cha enzi kati ya makerubi walio juu ya hilo Sanduku.[#6:2 yaani Kiriath-Yearimu]
3Wakaweka hilo Sanduku la Mungu juu ya gari jipya la kukokotwa na kulileta kutoka nyumba ya Abinadabu, iliyokuwa juu ya kilima. Uza na Ahio, wana wa Abinadabu, walikuwa wakiongoza hilo gari jipya la kukokotwa
4likiwa na Sanduku la Mungu juu yake, naye Ahio alikuwa anatembea akiwa mbele yake.
5Daudi na nyumba yote ya Israeli walikuwa wanacheza mbele za Bwana kwa nguvu zao zote, kwa nyimbo, vinubi, zeze, matari, kayamba na matoazi.
6Walipofika kwenye uwanja wa kupuria nafaka wa Nakoni, Uza akanyoosha mkono na kulishika Sanduku la Mungu kwa sababu maksai walijikwaa.
7Hasira ya Bwana ikawaka dhidi ya Uza kwa sababu ya kitendo chake cha kukosa heshima, kwa hiyo Mungu akampiga akafia papo hapo kando ya Sanduku la Mungu.
8Ndipo Daudi akakasirika kwa sababu ghadhabu ya Bwana ilifurika dhidi ya Uza, hivyo hadi leo mahali hapo panaitwa Peres-Uza.
9Daudi akamwogopa Bwana siku ile, akasema, “Ni jinsi gani Sanduku la Bwana litakavyoweza kunijia?”
10Hakuwa radhi kulichukua Sanduku la Bwana kwake katika Mji wa Daudi. Badala yake akalipeleka kwenye nyumba ya Obed-Edomu, Mgiti.
11Sanduku la Bwana likakaa katika nyumba ya Obed-Edomu, Mgiti, kwa miezi mitatu, naye Bwana akambariki pamoja na nyumba yake yote.
12Kisha Mfalme Daudi akaambiwa, “Bwana ameibariki nyumba ya Obed-Edomu pamoja na kila alicho nacho, kwa sababu ya Sanduku la Mungu.” Basi Daudi akateremka na kulipandisha Sanduku la Mungu kutoka nyumba ya Obed-Edomu hadi Mji wa Daudi kwa shangwe.
13Wale waliokuwa wamebeba Sanduku la Bwana walipotembea hatua sita, Daudi alitoa dhabihu fahali na ndama aliyenoneshwa.
14Daudi, akiwa amevaa kizibau cha kitani, alicheza mbele za Bwana kwa nguvu zake zote,
15wakati yeye na nyumba yote ya Israeli walipopandisha Sanduku la Bwana kwa shangwe na sauti za tarumbeta.
16Sanduku la Bwana lilipokuwa linaingia Mji wa Daudi, Mikali binti Sauli akachungulia dirishani. Naye alipomwona Mfalme Daudi akirukaruka na kucheza mbele za Bwana , akamdharau moyoni mwake.
17Wakaleta Sanduku la Bwana na kuliweka mahali pake ndani ya hema ambalo Daudi alikuwa amelisimamisha kwa ajili yake, naye Daudi akatoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani mbele za Bwana .
18Baada ya kumaliza kutoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani, Daudi akawabariki watu katika jina la Bwana wa majeshi.
19Kisha akatoa mkate, andazi la tende na andazi la zabibu kavu kwa kila mtu katika mkutano wote wa Waisraeli, wanaume kwa wanawake. Nao watu wote wakaenda nyumbani.
20Daudi aliporudi ili kuwabariki watu wa nyumbani mwake, Mikali binti Sauli akatoka nje kumlaki, akamwambia, “Tazama jinsi mfalme wa Israeli alivyojibainisha mwenyewe leo kwa kuvua mavazi yake machoni pa vijakazi wa watumishi wake, vile mtu asiye na adabu angefanya!”
21Daudi akamwambia Mikali, “Nilifanya hivyo mbele za Bwana ambaye alinichagua mimi badala ya baba yako au mwingine yeyote kutoka nyumba yake aliponiweka niwe mtawala wa Israeli, watu wa Bwana . Kwa hiyo nitacheza mbele za Bwana .
22Nitakuwa asiye na heshima kuliko sasa, nami nitajishusha machoni pangu mwenyewe. Lakini kwa hawa vijakazi uliosema habari zao nitaheshimiwa.”
23Naye Mikali binti Sauli hakuwa na watoto hadi siku ya kufa kwake.