Amosi 3

Amosi 3

Mashahidi waitwa dhidi ya Israeli

1Sikilizeni neno hili alilosema Bwana dhidi yenu, enyi watu wa Israeli, dhidi ya jamaa nzima niliowapandisha toka Misri:

2“Ni ninyi tu niliowachagua

kati ya jamaa zote za dunia;

kwa hiyo nitawaadhibu

kwa ajili ya dhambi zenu zote.”

3Je, watu wawili hutembea pamoja

wasipokubaliana kufanya hivyo?

4Je, simba hunguruma katika kichaka

wakati hana mawindo?

Aweza kuvuma katika pango

wakati ambao hajakamata chochote?

5Je, ndege aweza kuanguka kwenye mtego ulio ardhini

ambapo hajategewa chambo?

Je, mtego unaweza kufyatuka toka ardhini

wakati hakuna chochote cha kunasa?

6Je, tarumbeta inapopigwa mjini kujulisha hatari,

watu hawatetemeki?

Mji unapopatwa na maafa,

je, si Bwana amesababisha?

7Hakika Bwana Mwenyezi hatafanya neno lolote

bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake.

8Simba amenguruma:

je, ni nani ambaye hataogopa?

Bwana Mwenyezi ametamka:

je, ni nani awezaye kukosa kutoa unabii?

9Tangazeni katika ngome za Ashdodi

na katika ngome za Misri:

“Kusanyikeni juu ya milima ya Samaria;

angalieni wingi wa wasiwasi ulio ndani yake,

na uonevu ulio miongoni mwa watu wake.”

10Bwana asema: “Hawajui kutenda lililo jema,

wale ambao hujilundikia nyara

na vitu vilivyotekwa katika ngome zao.”

11Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi:

“Adui ataizingira nchi;

ataangusha chini ngome zenu

na kuteka nyara maboma yenu.”

12Hili ndilo asemalo Bwana :

“Kama vile mchungaji aokoavyo kinywani mwa simba

vipande viwili tu vya mfupa wa mguu

au kipande cha sikio,

hivyo ndivyo Waisraeli watakavyookolewa,

wale wanaokaa Samaria

kwenye kingo za vitanda vyao,

na katika Dameski

kwenye viti vyao vya fahari.”

13“Sikia hili na ushuhudie dhidi ya nyumba ya Yakobo,” asema Bwana, Bwana Mungu wa majeshi.

14“Siku nitakapomwadhibu Israeli kwa sababu ya dhambi zake,

nitaharibu madhabahu za Betheli;

pembe za madhabahu zitakatiliwa mbali

na kuanguka chini.

15Nitabomoa nyumba ya wakati wa masika,

pamoja na nyumba ya wakati wa kiangazi;

nyumba zilizonakshiwa kwa pembe za ndovu

na majumba makubwa ya fahari yatabomolewa,”

asema Bwana .

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.