The chat will start when you send the first message.
1Ole wenu ninyi mnaostarehe na kuridhika katika Sayuni,
na ninyi mnaojisikia salama juu ya Mlima Samaria,
ninyi watu mashuhuri wa taifa lililoendelea kuliko mataifa mengine,
ambao watu wa Israeli wanawategemea!
2Nendeni Kalne mkaone kutoka huko;
mwende hadi Hamathi iliyo kuu,
kisha mshuke hadi Gathi ya Wafilisti.
Je, wao ni bora kuliko falme zenu mbili?
Je, nchi yao ni kubwa kuliko yenu?
3Mnaiweka mbali siku iliyo mbaya
na kuleta karibu utawala wa kuogofya.
4Ninyi mnalala juu ya vitanda vilivyofunikwa kwa pembe za ndovu,
na kujinyoosha juu ya viti vya fahari.
Mnajilisha kwa wana-kondoo wazuri
na ndama walionenepeshwa.
5Ninyi mnapiga vinubi kama Daudi,
huku mkitunga nyimbo za vinanda mbalimbali.
6Mnakunywa mvinyo kwa bakuli zilizojazwa,
na mnajipaka mafuta mazuri,
lakini hamhuzuniki kwa maangamizi ya Yusufu.
7Kwa hiyo mtakuwa miongoni mwa watu wa kwanza kwenda uhamishoni;
karamu zenu na kustarehe kutakoma.
8Bwana Mwenyezi ameapa kwa nafsi yake mwenyewe: Bwana Mungu wa majeshi asema:
“Nachukia kiburi cha Yakobo,
nachukia ngome zake;
nitautoa mji wao na kila kitu
kilicho ndani yake.”
9Kama watu kumi watabaki katika nyumba moja, wao pia watakufa.
10Kama jamaa ambaye atachoma miili akija ili kuitoa nje ya nyumba, na kumuuliza yeyote ambaye bado anajificha humo, “Je, yuko mtu yeyote pamoja nawe?” Naye akisema, “Hapana,” ndipo atakaposema, “Nyamaza! Haturuhusiwi kutaja jina la Bwana .”
11Kwa kuwa Bwana ameamuru,
naye atabomoa jumba kubwa vipande vipande
na nyumba ndogo vipande vidogo vidogo.
12Je, farasi wanaweza kukimbia
kwenye miamba iliyochongoka?
Je, mtu aweza kulima kwa maksai huko?
Lakini mmegeuza haki kuwa sumu
na matunda ya uadilifu kuwa uchungu:
13ninyi mnaoshangilia kushindwa kwa Lo-Debari
na kusema, “Je, hatukuteka Karnaimu
kwa nguvu zetu wenyewe?”
14Maana Bwana Mungu wa majeshi asema,
“Nitainua taifa dhidi yenu, ee nyumba ya Israeli,
nalo litawatesa kuanzia Lebo-Hamathi
hadi Bonde la Araba.”