The chat will start when you send the first message.
1Nilimwona Bwana akiwa amesimama kando ya madhabahu, naye akasema:
“Piga vichwa vya nguzo
ili vizingiti vitikisike.
Viangushe juu ya vichwa vya watu wote;
na wale watakaosalia nitawaua kwa upanga.
Hakuna yeyote atakayekimbia,
hakuna atakayetoroka.
2Wajapojichimbia chini hadi kwenye vina vya Kuzimu,[#9:2 Kuzimu kwa Kiebrania ni Sheol , yaani Shimo lisilo na mwisho.]
kutoka huko mkono wangu utawatoa.
Wajapopanda juu hadi kwenye mbingu,
kutoka huko nitawashusha.
3Wajapojificha juu ya kilele cha Karmeli,
huko nitawawinda na kuwakamata.
Wajapojificha uso wangu
katika vilindi vya bahari,
huko nako nitaamuru joka kuwauma.
4Wajapopelekwa uhamishoni na adui zao,
huko nako nitaamuru upanga uwaue.
Nitawakazia macho yangu kwa mabaya
wala si kwa mazuri.”
5Bwana, Bwana wa majeshi,
yeye agusaye dunia nayo ikayeyuka,
na wote wanaoishi ndani yake wakaomboleza:
nayo nchi yote huinuka kama Mto Naili,
kisha hushuka kama mto wa Misri;
6yeye ambaye hujenga jumba lake la kifalme katika mbingu
na kuisimika misingi yake juu ya dunia,
yeye aitaye maji ya bahari
na kuyamwaga juu ya nchi:
Bwana ndilo jina lake.
7“Je, Waisraeli,
ninyi si sawa kwangu kama Wakushi?”
asema Bwana .
“Je, sikuleta Israeli kutoka Misri,
Wafilisti kutoka Kaftori,
na Washamu kutoka Kiri?
8“Hakika macho ya Bwana Mwenyezi
yako juu ya ufalme wenye dhambi.
Nami nitauangamiza
kutoka uso wa dunia:
hata hivyo sitaiangamiza kabisa
nyumba ya Yakobo,”
asema Bwana .
9“Kwa kuwa nitatoa amri,
na nitaipepeta nyumba ya Israeli
miongoni mwa mataifa yote,
kama vile nafaka ipepetwavyo katika ungo,
na hakuna hata punje moja itakayoanguka chini.
10Watenda dhambi wote miongoni mwa watu wangu
watauawa kwa upanga,
wale wote wasemao,
‘Maafa hayatatupata wala kutukuta.’
11“Katika siku ile
“Nitalisimamisha hema la Daudi lililoanguka.
Nitakarabati mahali palipobomoka
na kujenga upya magofu yake,
na kuijenga kama ilivyokuwa awali,
12ili wapate kuyamiliki mabaki ya Edomu,
na mataifa yote yale yanayobeba Jina langu,”
asema Bwana ambaye atafanya mambo haya.
13“Siku zinakuja,” asema Bwana ,
“wakati mvunaji atatanguliwa na mkulima,
naye mpanzi atatanguliwa na yeye akamuaye zabibu.
Divai mpya itadondoka kutoka milimani,
na kutiririka kutoka vilima vyote.
14Nitawarejesha tena watu wangu Israeli waliohamishwa;
wataijenga tena miji iliyoachwa magofu,
nao wataishi ndani yake.
Watapanda mizabibu na kunywa divai yake;
watalima bustani na kula matunda yake.
15Nitaipanda Israeli katika nchi yao wenyewe,
hawatangʼolewa tena
kutoka nchi niliyowapa,”
asema Bwana Mungu wenu.