The chat will start when you send the first message.
1Hili ndilo lililotokea wakati wa utawala wa Mfalme Ahasuero, yule aliyetawala majimbo mia moja na ishirini na saba (127) kutoka Bara Hindi hadi Kushi.
2Wakati huo Mfalme Ahasuero alitawala kwenye kiti chake cha ufalme katika ngome ya mji wa Shushani.
3Katika mwaka wa tatu wa utawala wake, alifanya karamu kwa ajili ya wakuu wake wote pamoja na maafisa. Akawaalika viongozi wa jeshi wa Uajemi na Umedi, wana wa wafalme na wakuu wa majimbo.
4Kwa muda wa siku mia moja na themanini mfalme alionesha utajiri mwingi wa ufalme wake, fahari na utukufu wa enzi yake.
5Siku hizo zilipopita, mfalme alifanya karamu kwa muda wa siku saba, katika bustani ya ndani katika jumba la kifalme, kwa ajili ya watu wote kuanzia mdogo hadi mkubwa, waliokuwa katika ngome ya mji wa Shushani.
6Bustani ilikuwa na mapazia ya kitani nyeupe na buluu, yaliyofungiwa kamba za kitani nyeupe na kitambaa cha zambarau, kwenye pete za fedha juu ya nguzo za marumaru. Kulikuwa na viti vya dhahabu na vya fedha vilivyokuwa vimewekwa kwenye ile sakafu iliyotengenezwa kwa mawe ya rangi, marumaru, lulumizi na mawe mengine ya thamani.
7Vyombo vya dhahabu vilitumika kwa watu kunywea mvinyo, kila kimoja tofauti na kingine, naye mfalme akatoa mvinyo kwa wingi kwa kadiri ya ukarimu wake.
8Kwa amri ya mfalme kila mgeni aliruhusiwa kunywa alichotaka, kwa kuwa mfalme alitoa maagizo kwa watumishi wote kugawa mvinyo kila mtu kwa jinsi alivyotaka.
9Malkia Vashti pia akawafanyia wanawake karamu katika jumba la kifalme la Mfalme Ahasuero.
10Siku ya saba, wakati Mfalme Ahasuero alikuwa amesisimka roho yake kwa mvinyo, aliamuru matowashi saba waliokuwa wakimhudumia, yaani Mehumani, Biztha, Harbona, Bigtha, Abagtha, Zethari na Karkasi,
11kumleta Malkia Vashti mbele ya mfalme akiwa amevaa taji lake la kifalme, ili aoneshe uzuri wake kwa watu na wakuu, kwa kuwa alikuwa ni mzuri kumtazama.
12Lakini wakati watumishi walipotoa amri ya mfalme, Malkia Vashti alikataa kuja. Ndipo mfalme alighadhibika, na hasira yake ikawaka.
13Kwa kuwa ilikuwa desturi ya mfalme kupata ushauri kwa wataalamu katika mambo ya sheria na haki, alizungumza na watu wenye busara, ambao walijua nyakati,
14nao waliokuwa karibu na mfalme ni Karshena, Shethari, Admatha, Tarshishi, Meresi, Marsena na Memukani, wakuu saba wa Uajemi na Umedi waliokuwa na nafasi ya pekee kwa mfalme nao walikuwa na vyeo vya juu kabisa katika utawala wake.
15Mfalme akauliza, “Kulingana na sheria, Malkia Vashti anapaswa kutendewa nini? Malkia hakutii amri ya Mfalme Ahasuero ambayo matowashi walimpelekea.”
16Kisha Memukani akajibu mbele ya mfalme na wakuu, “Malkia Vashti si kwamba amemkosea mfalme tu bali pia amewakosea wakuu wote na watu wa himaya yote ya Mfalme Ahasuero.
17Kwa maana tendo hili la malkia litajulikana kwa wanawake wote, kwa hiyo watawadharau waume zao na kusema, ‘Mfalme Ahasuero aliagiza Malkia Vashti aletwe mbele yake, lakini alikataa.’
18Siku ya leo, wanawake wa wakuu wa Uajemi na Umedi ambao wamesikia kuhusu tabia ya malkia watawatendea wakuu wote wa mfalme vivyo hivyo. Hapatakuwa na mwisho wa dharau na ugomvi.
19“Kwa hiyo, kama itampendeza mfalme, atoe amri ya kifalme na iandikwe katika sheria ya Uajemi na Umedi, ambayo haitabadilika, kwamba Vashti kamwe asije tena mbele ya Mfalme Ahasuero. Pia mfalme na atoe hiyo nafasi yake ya umalkia kwa mwanamke mwingine aliye bora kuliko yeye.
20Kisha mbiu hii ya mfalme itakapotangazwa katika himaya yake iliyo kubwa sana, wanawake wote watawaheshimu waume zao, kuanzia mdogo hadi mkubwa.”
21Mfalme na wakuu wake walipendezwa na shauri hili, hivyo basi mfalme akafanya kama Memukani alivyopendekeza.
22Alipeleka barua katika sehemu zote za ufalme wake, kwa kila jimbo kwa maandishi yake mwenyewe na kwa kila watu katika lugha yao wenyewe, akitangaza kwa msemo wa kila watu kwamba inampasa kila mwanaume kuwa mtawala wa nyumba yake mwenyewe.